Sababu za Mkoa wa Kagera kuongoza kwa malaria nchini

Jamii Africa
Akina mama na watoto wao wakiwa wameshika neti za kuzuia malaria walizopatiwa na Mfuko wa Kupambana na Ukimwi, TB na Malaria Duniani. Picha kwa hisani ya Global mfuko huo.

*Kiwango cha malaria kwa watoto wenye miezi sita hadi 59 ni takribani mara tatu ya wastani wa kitaifa

Zaujia Swalehe

Dar es Salaam. Wengi tunaufahamu mkoa wa Kagera. Mkoa huo, uliopo Kaskazini Magharibi mwa Tanzania wenye wakazi wapatao milioni 2 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, unafahamika kwa mengi ikiwemo sehemu mojawapo kuzungukwa na Ziwa Victoria.

Mbali na Ziwa Victoria, pia umebarikiwa kuwa na mito midogo midogo, misitu na vichaka vikubwa huku baadhi vikiwemo karibu na makazi ya watu.

Kama ilivyo mikoa mingine ya ukanda wa ziwa, hali ya hewa ya mkoa huu ni ile ya kitropiki yaani hali yenye joto ambavyo huufanya mkoa kuwa miongoni mwa ile iliyobarikiwa kuwa na mvua kubwa.

Hata hivyo, baraka hiyo siyo wakati wote ni njema. Wataalamu wanaeleza kuwa hali hiyo ni miongoni mwa sababu zilizofanya Kagera kuwa ni mkoa unaongoza kuwa na Malaria nchini, jambo linalotishia afya za wakazi wa mkoa huo hususan watoto.

Ripoti ya utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na viashiria vya malaria ya mwaka 2015-2016 inaonesha kuwa mkoa huo unaongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha Malaria kwa watoto wenye umri wa miezi sita hadi 59 kwa asilimia 41, takriban mara tatu juu ya wastani wa ugonjwa huo nchini.

Katika ripoti hiyo, asilimia 14 ya watoto wenye miezi sita hadi 59 walikutwa na malaria jambo linaloonyesha kuwa ugonjwa huo unazidi kupungua kwa kasi.

                                                          Chanzo; Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS)

“Kiwango cha malaria kinapungua kwa kasi kadri utajiri unavyoongezeka kutoka asilimia 23 kutoka kwa watoto walio katika kaua maskini kabisa hadi asilimia moja kwa watoto walio katika kaya tajiri,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Lakini pamoja na maendeleo hayo, Kagera inafuatiwa na Geita, Kigoma, Morogoro na Ruvuma kwa kuwa na kiwango cha juu cha malaria.

Hata wakati Kagera ikiongoza kwa malaria, kuna mikoa kumi nchini ikiwa na kiwango cha chini cha malaria mingi ikiwa kutoka Zanzibar. Sehemu kubwa ya mikoa kiwango cha malaria kipo chini ya asilimia moja.

Baadhi ya wakazi wa Kagera wanaeleza kuwa ugonjwa huo ulianza kuwasumbua sana na kuua watoto mkoani humo toka miaka ya 1990 hususani kipindi cha mvua za El-nino.

Mkazi wa mkoa huo aliyejitambulisha kwa jina moja la Paul anasema kuwa giza  linapoingia mbu huwa wengi sana ambao sehemu kubwa hutokea kwenye madimbwi.

 “Giza likianza kuingia kundi la mbu hutawala utasema nyuki wako kwenye mzinga,” anasema Paul.

 “Nakumbuka kipindi hicho cha Mvua za El-nino hakuna familia ambayo haikupata msiba kutokana na ugonjwa wa Malaria, watoto wengi walifariki kipindi hicho.”

Sera ya Afya ya mwaka 2007 nchini inatambua kuwa Watanzania wengi wanakabiliwa na magonjwa makubwa matatu ukiwemo wa Malaria.

Wakati Serikali ya awamu iliyopita chini ya Rais Jakaya Kikwete ikitajwa kujitahidi katika kupambana na ugonjwa huo mkoani Kagera, Serikali ya awamu ya tano inanyooshewa kidole kwa kutofanya jitihada za kutosha.

Mathalani inatajwa kuwa Serikali ya awamu ya nne ilijitahidi kupeleka dawa za kupulizia majumbani ingawa zoezi hilo lilikabiliwa na changamoto zikiwemo za watu kukosa imani na zoezi hilo. Lakini kwa sasa huduma hiyo haifanywi mara kwa mara.

Pia, kuna tatizo la uelewa miongoni mwa wananchi wa mkoa huo. Bado wakazi wa mkoa huo hawajitokezi kwa wingi kwenda hospitali kupatiwa tiba ya malaria jambo linalosababisha baadhi hususan watoto kupoteza maisha.

Lakini wengine hawatumii vyandarua ambavyo vingesaidia kuwakinga dhidi ya mbu waenezao malaria.

Kama ilivyo mikoa mingine, Kagera pia inakabiliwa na changamoto lukuki upungufu wa vituo vya afya na wahudumu huku ukosefu wa dawa ukiwa ni tatizo kubwa.

Mganga Mkuu wa Kagera Dkt. Thomas Rutachunzibwa anakiri uwepo wa kiwango kikubwa cha malaria mkoani kwake lakini haraka akashauri jitihada za dhati zifanyike ili kuondoa hali hiyo.

 “Juhudi za ziada zinatakiwa zitiliwe kutatua janga hili katika mkoa huu na Taifa kwa ujumla. Hili linawezekana kwani takribani mikoa kumi inaonekana kuwa na asilimia chache kabisa za kiwango cha malaria, mbinu zilizotumika huko zitumike na huku pia ili kuokoa maisha ya watoto,” anasema Dkt. Rutachunzibwa.

Kuhusu sababu za kuwepo kwa kiwango hicho cha Malaria mkoani humo, Mganga mkuu huyo alisema apewe muda ilia atoe majibu sahihi hata hivyo alipopigiwa simu baadae hakuweza kupokea tena simu.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ambaye licha ya kupigiwa simu kwa siku kadhaa ili kupata maelezo yake juu ya jambo hili, hakuweza kupokea simu hizo.

Hata Fikra Pevu ilipomtafuta Naibu wake Dkt. Hamisi Kigwangwala nae hakuweza kupokea simu na hata alipotumiwa ujumbe kwa njia ya simu hakujibu.

Jitihada bado zinaendelea kuwatafuta viongozi hao ili watolee ufafanuzi zaidi juu ya baadhi ya mikoa nchini kuwa na kiwango kikubwa cha Malaria kwa watoto huku mingine ikiwa na kiwango kidogo.

Hata hivyo, Paul anasema wakazi wa Kagera wengi hulala na neti kwa misimu, kipindi cha joto hawalali na neti kabisa hii nayo inaweza kuchangia maambikizi ya ugonjwa huo.

Pia anaishauri serikali izidishe juhudi katika kupambana na ugonjwa huo mkoani huko kwa kuboresha Huduma za Afya na kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi.

Katika jitihada za  kupambana na ugonjwa huu unaoua watu wengi duniani, ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2015/2016 inasema ugonjwa wa Malaria unaendelea kupungua siku hadi siku duniani huku Bara la Afrika likiongoza kwa vifo hususani kwa watoto kwa asilimia 90.  

Nalo Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya watoto (UNICEF) linasema kuwa watoto takribani milioni moja hufariki kwa malaria barani Afrika.

Hivyo basi Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi zilizoridhia Malengo ya Maendeleo Endelevu Duniani (SDG)  yakiwa na lengo la kuimarisha afya bora kwa rika zote haina budi kuhakikisha inajipanga ipasavyo ili kutokomeza vifo hivi vya Malaria kwa watu wote wakiwemo watoto

Hii inaenda sambamba na kutimiza malengo ya Taifa ya kupunguza vifo vya watoto ifikapo 2025.

Hata hivyo, Serikali pekee haiwezi kufanikisha hili bila ushiriki wa wadau wengine wakiwemo wananchi wenyewe na sekta binafsi.

Wadau wa afya waneleza kuwa Serikali na Sekta binafsi zishirikiane kwa ukaribu katika kuendeleza sekta ya Afya ili kutokomeza ugonjwa huu wa Malaria na mengine yanayopunguza nguvukazi ya Taifa na maendeleo yake.

Kwa umoja inawezekana Ikumbukwe kuwa waoto ni Taifa la kesho tuwatunze leo watutunze kesho.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *