Sababu za kukosa usingizi wakati wa ujauzito na tiba yake

Jamii Africa

Jukumu la kutunza familia ni la wazazi wote wawili yaani mwanaume na mwanamke. Lakini majukumu ya mwanamke huongezeka pale anapopata ujauzito, hulazimika kumlea mtoto aliyepo tumboni mpaka azaliwe salama.

Katika kipindi chote cha ujauzito, mama mwanamke  hupitia mabadiliko mbalimbali ikiwemo matatizo ya kukosa usingizi wa uhakika. Kulinga na utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wanawake wajawazito wamewahi kupata matatizo ya usingizi angalau mara moja katika uzazi wao.

Kwa upande mmoja, mjamzito hujisikia kuchoka muda mwingi na kuhitaji kumpumzika au kulala lakini upande wa pili hapati usingizi. Jambo lingine ni kuwa mabadiliko yanayotokea mwilini hasa yale yanayosababishwa na homoni yanamuweka mwanamke katika wakati mgumu kuhimili ujauzito. Kwa muktadha huo, usingizi huwa suluhisho, lakini baadhi yao hukosa kabisa usingizi.

Kwanini  hali hiyo hujitokeza kwa mjamzito?, hizi ndizo sababu hasa za kukosa usingizi wakati wa ujauzito:

Kucheza kwa mtoto

Wakati wa wiki za mwisho za ujauzito, michezo ya mtoto kwenye tumbo la uzazi inaweza kuvuruga usingizi wa mama. Kila mtoto anapogeuka, mama huamka toka usingizini na inakuwa sio rahisi kupata usingizi tena.

 

Mkazo/Msongo wa mawazo

Ujauzito unaweza kuongeza kiwango cha mkazo na msongo wa mawazo, hasa pale mwanamke anapowaza siku ya kujifungua au maumivu anayoyapata. Hali hiyo ikiendelea kwa muda mrefu inaweza kumuondolea mjamzito usingizi wakati wa usiku.

 

Maumivu kwenye miguu

Wakati wa ujauzito, maumivu ya miguu ni tatizo la kawaida. Hali hiyo hujitokeza zaidi mwezi wa sita wa ujauzito na kuendelea kwasababu ya kuongezeka kwa uzito wa mtoto na damu kutokupenya vizuri kwenye miguu. Wakati mwingine miguu huvimba, wanawake wengine kipindi hicho hushindwa hata kutembea na kulazimika kukaa muda mwingi.

Maumivu ya miguu wakati wa usiku yanaweza kuvuruga usingizi na kumfanya mjamzito kuwa macho kutokana na hali isiyo ya kawaida anayoipata kwenye miguu.

 

Kukojoa mara kwa mara

Wakati wa ujauzito ni jambo la kawaida kukojoa mara kwa mara. Na kama mwili unataka kutoa mkojo wakati usiku, mjamzito hana hiari zaidi ya kumka na kwenda kukojoa.

Ikiwa vipindi kwenda kukojoa vitatokea mara kwa mara, mama hawezi kupata usingizi wa uhakika na bora. Hali hii pia husababisha tatizo la kukosa usingizi (insomnia). Hili tatizo hujitokeza zaidi katika wiki za mwisho za ujauzito.

 

Chakula

Wakati mwingi, aina ya chakula anachokula mwanamke wakati wa ujauzito kina mchango mkubwa wa kumfanya akose usingizi. Kama anakunywa kahawa, kuvuta sigara na kutumia pombe muda mfupi kabla ya kulala, uwezekano wa kukosa usingizi ni mkubwa sana.

Inashauriwa mama mjamzito kuepuka vyakula vinavyoweza kuhatarisha afya yake. Ni vema kumuona daktari kwa ushauri zaidi juu ya matumizi ya vyakula wakati wa ujauzito.

 

Ndoto za vitisho

Ikiwa mjamzito anapata  ndoto za kutisha au usingizi wa mang’amung’amu, atashtuka mara kwa mara kutoka usingizini. Ndoto hizo kwa sehemu kubwa huchangia tatizo la kukosa usingizi. Nini kinasababisha ndoto hizo? Msongo wa mawazo au mkazo, pia mawazo kuhusu mambo yajayo, afya ya mtoto na hofu ambazo zote zinaweza kuwa chanzo cha kukosa usingizi.

 

Ukuaji wa mtoto tumboni

Kadri mimba inavyozidi kuwa kubwa, ndivyo tumbo la mjamzito hungezeka. Hali hii inaweza kuwa changamoto kwa mwanamke kulala vizuri kwasababu hulazimika kulala upande mmoja.

Hata hivyo, ni muhimu sana kumuona daktari wako, ikiwa utapata dalili zozote za kukosa usingizi ili kupata ushauri wa kitabibu utakaokusaidia kuwa na afya njema wakati wote wa ujauzito na kuhakikisha mtoto anazaliwa salama.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *