Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inakusudia kuchunguza utajiri na ulipaji wa kodi wa Askofu Mkuu, Zachary Kakobe wa kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (F.G.B.F) ili kuihakikishia serikali mapato.
Hatua hiyo ya TRA inakuja siku chache baada ya ujumbe wa video unaosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ukimuonesha Askofu Zachary Kakobe akisikika akisema “mimi sihitaji hela, nina hela kuliko serikali nimewaambia waandishi wa habari hakuna wa kunihonga mimi wala hakuna wa kunipa hela yoyote. Hata waziri hana aje nitamkopesha”.
Fikra Pevu imetafuta mahubiri hayo na kugundua kuwa aliyatoa Agosti, 2014 wakati wa kuadhimisha miaka ya 25 ya kuanzishwa kwa kanisa hilo.
Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere amesema wamepokea kwa unyenyekevu mkubwa kauli inayodhaniwa kuwa ya Askofu Kakobe na wameanzisha mchakato wa kuchunguza utajiri wake ili mamlaka hiyo ipate haki yake ikiwemo kodi inayotozwa kutoka taasisi mbalimbali.
“Kama mtu ana hela kuliko serikali, kama ambavyo tunajua serikali yetu inatoa huduma inanunua ndege, imejenga standard gauge, inajenga barabara, inatoa elimu bure, inalipa mishahara kwa watumishi wa umma, inalipia madawa hospitalini, inalipa na kutoa huduma za ulinzi na usalama kwa wananchi. Lakini Serikali hiyo tunaambiwa inazidiwa hela na Askofu Kakobe basi ni jambo jema”, amesema Kichere.
Amebainisha kuwa katika hatua za awali wamegundua hakuna kumbukumbu zozote zinazoonyesha Askofu Kakobe kulipa kodi licha ya yeye kujitangaza kuwa ana pesa kuliko serikali.
"Kuna Matajiri tunawafahamu lakini hawaizidi serikali kwa pesa, tumeona wamekuwa wakilipa kodi na kuonekana kwenye kumbukumbu zetu lakini huyu tajiri Askofu Kakobe si miongoni mwao. Hivyo basi sisi watu wa kodi tunataka tujiridhishe tu kuhusu swala la kodi kuhusiana na Askofu Kakobe na utajiri wake", amesema Kichere
Hata hivyo Kamishana huyo amesema kwa mujibu wa sheria taasisi za dini hazilipi kodi kutokana na mapato ya sadaka lakini kodi inaweza kupatikana kwenye shughuli nyingine za taasisi hizo.
"Tunaelewa kwa mujibu wa sheria sadaka haitozwi kodi, ila tunafahamu taasisi za dini huwa zina shughuli nyingine za kiuchumi, huenda Askofu Kakobe na yeye akawa na shughuli nyingine zinampatia hela mpaka akawa na pesa nyingi kuliko Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania", amesema Kichere.
Askofu Mkuu, Zachary Kakobe wa kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (F.G.B.F)
Uamuzi huo wa TRA unakuja siku chache baada ya mahubiri aliyoyatoa Askofu Kakobe siku ya Krismasi kwenye kanisa lake la FGBF Mwenge Dar es Salaam na kuzungumzia masuala ya utawala bora na mwenendo wa siasa za Tanzania huku akiwataka viongozi wa serikali kutafakari maisha yao na kumrudia Mungu kwa kutubu dhambi walizofanya. Sehemu ya mahubiri hayo inaeleza kuwa,
“Leo ni siku ya watawala wa Tanzania kutubu, tumeanza kuona misingi ya amani ya nchi yetu ikitikiswa, amani iliyojengwa kwa gharama kubwa na waasisi wetu; tumeanza kuona nchi hii ni ya chama kimoja, na huu ni uovu”
Askofu Kakobe aliungana na viongozi wengine wa dini nchini kutumia ibada za Siku kuu ya Krismasi kukosoa baadhi ya mambo yanayoendelea nchini, ikiwamo uhuru wa kutoa maoni na viongozi kukubali kukosolewa.
Mahubiri hayo ya viongozi wa dini yaliibua mjadala mpana miongoni mwa wananchi ambapo wengine wakiwasifia viongozi hao kwa kuongea ukweli ili nchi ipone, lakini baadhi ya watu waliona mahubiri hayo ni kejeli na kubeza juhudi za serikali ya awamu ya tano za kupambana na rushwa.
Hata hivyo, Askofu Kakobe hajajitokeza kuzungumzia hatua hiyo ya TRA kutaka kumchunguza kwa kile kinachotajwa utajiri alionao na masuala ya ulipaji kodi.
Serikali yatoa tamko
Mjadala huo uliendelea kuibua hisia tofauti kutoka kwa wanachama wa vyama vya siasa na kutengeneza mpasuko wa kifikra miongoni mwa wananchi hasa wale wanaotumia mitandao ya kijamii.
Kutokana na sintofahamu hiyo, serikali ilitoa taarifa kuwaonya viongozi wa dini wanaotumia mahubiri yao kuchambua masuala ya kisiasa, ikiwataka kuheshimu msingi wa uanzishwaji wa taasisi zao la sivyo taasisi zao zitafutwa.
Taarifa ilitolewa Desemba 28 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali mstaafu Projest Rwegasira imesema taasisi za dini zinapaswa kuzingatia sheria na masharti ya kuanzishwa kwake ambayo yapo kwenye Katiba za taasisi husika na kuacha kuzungumzia mambo ya siasa kwenye nyumba za ibada ikiwemo kuwasifu au kuwakosoa wanasiasa.
“Kazi yao wao ni kueneza dini, kueneza neno la Mungu, si kuingia mambo ya siasa, kushambulia viongozi wa Serikali wanakuwa wamekwenda kinyume cha malengo ya usajili wao. Nashauri na nimewaambia, waachane na mambo ya siasa waende katika dini kwani kuna tatizo gani?
“Kama Serikali inakwenda vibaya watumie majukwaa yao kuzungumza na si kutumia nyumba za ibada yanayounganisha waumini kuzungumza siasa na tulichokifanya sasa ni kuwakumbusha tu na hakuna yeyote aliyechukuliwa hatua,” amesema.
Kauli ya serikali yawaibua wanasiasa
Taarifa hiyo ya serikali iliibua mjadala zaidi miongoni mwa wananchi wakihoji mipaka ya dini na siasa katika ustawi wa jamii.
Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe ametofautiana na Serikali akisema viongozi wa dini wanapaswa kuachwa watimize wajibu wao wa kukosoa. “Kesho tutazitaka taasisi za dini zihamasishe amani, maendeleo, zipongeze ‘Its important’ (ni muhimu) kukubali kukosolewa,” ameandika Bashe katika akaunti ya Twitter na kuongeza kuwa,
“Taasisi za dini zina haki kutoa maoni yao juu ya siasa, uchumi na masuala yote ya kijamii, viongozi wa dini wana nafasi yao.”
Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole akihojiwa na kituo cha televisheni cha Azam kuhusu onyo hilo amesema viongozi wa dini hawajazuiwa kutoa maoni lakini wanapaswa kutumia lugha za staha na zisizo za kichochezi.
“Wako wazi kusema chochote kwa mujibu wa Katiba za nchi, sheria zetu… anayesema mtu kazuiliwa kuzungumza uhuru wake wa maoni atakuwa na matatizo mengine, ninachokifahamu kuzungumza kauli za matusi ni makosa,” amesema Polepole.
Licha ya matamko mbalimbali ya viongozi wa dini na serikali, mjadala unaendelea kuhusu kutenganisha dini na siasa ikizingatiwa kuwa dini imekuwa na mafungamano ya karibu na wanasiasa. Pia taasisi za dini zimekuwa zikitoa huduma za kijamii ambazo zinatumiwa na wananchi ambao wako chini ya maongozi ya kisiasa.
Inawezekana kutenganisha dini na siasa?
Akihojiwa mwaka 2012 na gazeti la New York Times, Kardinali Timothy Dolan wa kanisa Katoliki nchini Marekani, alisema, “Haiwezekani kuzitenganisha, na mtu yeyote anayesema inawezekana labda anadanganya au hajafikiri sawasawa”.
Anasema ameshauriwa na watu wengi wakimtaka asichanganye mahubiri yake na siasa lakini anawaambia kutokana na historia ya binadamu dini na siasa haviwezi kutengana kwa sababu asili ya binadamu ni ujima (communal beings) na hatuwezi kuishi kila mtu peke yake.
Anaongeza kuwa kila jambo linalotufanya sisi tuitwe binadamu limetokana na jamii tunazoishi kuanzia ngazi ya familia. Binadamu anatofautishwa na viumbe wengine kwasababu ana milango 5 ya fahamu inayompa uwezo wa kufanya maamuzi. Siasa ni jinsi tunavyopangilia maisha ya kila siku.
Anasisitiza kuwa amekuwa akiambiwa akae mbali na masuala ya siasa lakini jibu lake ni kuwa haiwezekani kwa sababu wanasiasa ni waumini wa dini hizo. Akitolea mfano wa kifo cha Yesu Mnazareti anaeleza kuwa kifo hicho kilikuwa cha kisiasa. Yesu alikuwa akihubiri kweli na kutetea haki za wanyonge; wakati mwingine akiwakosoa watawala akiwemo Mfalme Kaisaria wa dola ya Rumi ambaye alikuwa na mamlaka ya kiungu katika kutawala kwake.
Anamalizia kusema dini na siasa vinategemeana, uwepo wa siasa safi ni mafanikio ya taasisi imara za dini. Kutenganisha dini na siasa ni kujaribu kuondoa nguzo muhimu zinazongoza jamii.