‘Scorpion’ aliyemtoboa macho Said Mrisho ahukumiwa jela miaka 7 na kulipa fidia ya milioni 30

Jamii Africa
Mahakama imemhukumu Salum Njwete maarufu kama 'Scorpion' kwenda jela miaka 7 na faini ya Milioni 30 kwa kumtoboa macho, Said Mrisho - Ametozwa faini hiyo kama fidia kwa Said Mrisho aliyepoteza macho yake katika tukio hilo la aina yake - Scorpion alikamatwa mnamo mwezi Oktoba mwaka 2016 kwa tuhuma za kumtoboa macho, kumchoma kisu na kumpora Mfanyabiashara Said Ally katika maeneo ya Buguruni
  • Aliyetobolewa macho kupewa fidia milioni 30
  • Hakimu asema rufaa iko wazi kwa mtu ambaye hajaridhika

Mahakama ya Wilaya ya  Ilala imemhukumu Salum Njwete maarufu kwa jina la ‘Scorpion’ kifungo cha miaka saba na kulipa fidia ya milioni 30 kwa kosa la kujeruhi na wizi wa kutumia silaha.

Hukumu hiyo imesomwa mbele ya Hakimu, Flora Haule ambapo imemkuta na hatia ya kujeruhi ikiwemo kumtoboa macho kinyozi Said Mrisho na unyang’anyi wa kutumia silaha. Hapo awali mahakama ilimfutia Salum kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha baada ya upande wa mashtaka kuomba shtaka hilo liondolewe mahakamani kwasababu hawana nia ya kuendelea na kesi hiyo.

Kutokana na maombi hayo, Hakimu aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo, Adelf Sachore alikubaliana na ombi hilo kwa kuzingatia kifungu namba 91 kifungu kidogo cha kwanza cha sheria ambacho kinampa Mamlaka Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuondoa shtaka mahakamani muda wowote ili mradi kama kesi hiyo haijatolewa hukumu.

Kifungu hicho pia kinampa Mamlaka DPP kumshtaki upya mshtakiwa huyo kama ana nia ya kuendesha shtaka hilo. Upande wa mashtaka ulifungua kesi mpya  yenye mashtaka mawili ambapo kesi hiyo ilihamishiwa kwa Hakimu Flora Haule ambaye leo ametoa huku hiyo ya kifungo cha miaka saba na faini ya milioni 30 kwa mshtakiwa ambapo anapaswa kulipa haraka iwezekanavyo.

Kesi hiyo iliipata umaarufu ikizingatiwa kuwa mshtakiwa ‘Scorpion’ ni mwalimu wa Sanaa ya kujihami, 'Martial arts', msanii wa filamu za maagizo na mshindi wa shindano la Dume Challenge mwaka 2012. 

Katika kesi hiyo, Njwete alikuwa anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni unyang’anyi wa kutumia silaha na kumjeruhi Said Mrisho kwa kumchoma kisu sehemu mbalimbali za mwili zikiwemo, tumboni na mabegani na kisha kumtoboa macho na kumsababishia upofu, kitendo anachodaiwa kutenda Septemba 6, mwaka 2016 katika eneo la Buguruni Sheli, jijini Dar es Salaam.

Pia anadaiwa alifanya tukio la unyang’anyi ambapo aliiba cheni ya Silva yenye uzito wa gramu 34 ikiwa na thamani ya Sh 60,000, simu ya mkononi na fedha taslimu Shilingi 330,000 vyote vikiwa na thamani ya Sh 474,000 mali ya Said Mrisho.

                        Salum Njwete 'Scorpion' aliyeva kanzu akirudishwa rumande chini ya ulinzi wa polisi katika moja ya kesi Mahakama ya Wilaya ya Ilala

Kufuatia tukio hilo  Said Mrisho ambaye mpaka sasa hana uwezo wa kuona baada ya kutobolewa macho yake yote mawili ameamriwa na mahakama kulipwa faini ya milioni 30  kama namna ya fidia. 

Hakimu Haule amesema katika hukumu hiyo Mahakama ilijikita sehemu kuu tatu ikiwemo kama mlalamikaji, Said Mrisho  amepata majeraha ya hatari pamoja na kama Scorpion alitumia unyang’anyi wa kutumia silaha. Pia Hakimu alitoa ruhusa kwa mtu yoyete ambaye hajaridhika na hukumu hiyo kukata rufaa.

“Faini ilipwe wakati unatumikia kifungo, pia ni ruksa kukata rufaa kwa upande wowote kama haujaridhika,” amesema, Hakimu  Flora Haule.

Hata hivyo Said Mrisho ameonekana kutoridhishwa na hukumu hiyo ya miaka 7 na kusema ni ndogo hivyo atapeleka ombi lake kwa Rais John Magufuli.

“Hiyo milioni 30 ni ndogo sana, na kwahiyo miaka saba ni hukumu ndogo sana. Yaani inaniumiza sana na watoto wangu sifikirii nitafanya nini kwasababu sina ubunifu wa kufanya chochote nikiwa katika mazingira haya”, amesema Said Mrisho wakati akihojiwa na waandishi wa habari mara baada ya hukumu hiyo kusomwa na Mahakama ya Wilaya ya Ilala na kuongeza kuwa,

“Kwa hili sidhani kama nitaishia hapa, nitafika kwa Mhe. Rais, nitafika kwa Mhe. Mkuu wa Mkoa nitawaeleza kwa hili siwezi kukubaliana nao wameniharibia maisha sana".

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *