Rais John Magufuli amesema hazima ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda inaweza isifanikiwe ikiwa tatizo la upatikanaji wa umeme wa uhakika halitatatuliwa ili kuchochea uzalishaji wa bidhaa za kilimo na viwandani.
Akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa kituo cha kufua umeme cha Kinyerezi II (240 MV CCPP) kilichopo Segerea jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amesema nishati ya umeme ni muhimu katika shughuli za uzalishaji lakini umeme unaozalishwa nchini haukidhi ongezeko la mahitaji ya wateja wote waliounganishwa na wale ambao wanatarajiwa kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa.
“Nishati ya umeme ni injini muhimu mno na muhimili muhimu katika ukuzaji wa uchumi na ustawi wa maisha wa binadamu. Umeme unachochea shughuli za uzalishaji na hivyo kutoa fursa za ajira na kuboresha maisha ya watu”, alisema Rais na kubainisha kuwa,
“Hazima na dhamira yetu ya kujenga uchumi wa viwanda haiwezi kutimia bila kuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika na kwasababu hiyo inatia moyo pamoja na matatizo tuliyonayo hali ya umeme nchini sio mbaya sana”.
Mahitaji halisi ya umeme ya Tanzania kwa sasa ni megawati 1400, ambapo hayatoshelezi mahitaji yote hasa wakati huu serikali inapotekeleza sera ya uchumi wa viwanda na kwamba hatua muhimu zisipochukuliwa kubuni vyanzo mbadara vya uzalishaji hatuwezi kutokomeza umaskini na kukuza pato la taifa.
“Mahitaji ya umeme nchini hivi sasa yanakadiriwa kufikia Megawati 1,400 lakini kwa kujumlisha Megawati hizi ambazo zipo sasa tunazalisha Megawati 1,513. Haya ni mafanikio makubwa ambayo hatuna budi kujipongeza. Ni wazi kuwa jitihada kubwa na za makusudi zinahitajika ili tuweze kuwa na umeme unaokidhi mahitaji ya uchumi wa sasa”, alisema Rais.
Kituo cha kufua umeme wa gesi cha Kinyerezi II ni muendelezo wa jitihada za serikali kuzalisha umeme wa gesi kutoka Mtwara ambako gesi hiyo inachimbwa ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yameathiri uzalishaji wa umeme wa maji kwenye mabwawa makubwa ya Kidatu na Nyumba ya Mungu.
Uzalishaji wa ememe umeathiriwa na upungufu wa maji hasa nyakati za Kiangazi ambapo Mito inayomwaga maji katika Mabwawa hayo hukauka kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo, ufugaji na uvuvi.
Mathalani, Kituo cha umeme cha Nyumba ya Mungu, kina uwezo wa kuzalisha umeme wa Megawati 8 ambao huingizwa kwenye Gridi ya Taifa lakini hadi kufikia mwishoni mwa Januari mwaka huu kituo hicho kilikuwa kinazalisha Megawati 3.5 hadi 4 tofauti na uwezo wake wa kuzalisha Megawati 8 kwa saa 24.
Kutokana na gharama kubwa za uzalishaji wa umeme nchini zimesababisha bei ya umeme iwe juu na kuwa kikwazo kwa watanzania kupata nishati hiyo muhimu kwa shughuli za uchumi. Hata wale waliounganishwa bado wanakabiliwa na changamoto za kukatika mara kwa mara kwa umeme katika maeneo yao.
Kulingana na takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ni asilimia 36.6 ya watanzania ndio wameunganishiwa umeme katika nyumba zao hii ikiwa na maana kuwa zaidi ya asilimia 60 ya watanzania hawapati umeme na kulazimika kutumia mafuta ya taa, kuni, mkaa kama vyanzo vya nishati ambavyo sio rafiki kwa mazingira.
Kwa muktadha huo, miti itaendelea kukatwa na kuathiri mwenendo wa mvua na maji yanayohitajika katika uzalishaji wa umeme wa maji (hydro-power) ambao unategemewa kwa kiasi kikubwa nchini na kuwakosesha watanzania wengi huduma hiyo.
Tatizo liko wapi?
Inaelezwa kuwa tatizo la umeme sio la Tanzania pekee bali nchi zote za Afrika. Watu milioni 600 hasa wanaotoka vijijini ambao ni sawa na watu 2 kati 3 katika nchi za Afrika hawapati huduma ya umeme.
Uzalishaji wa umeme katika bara hilo uko chini ya kiwango kilichowekwa duniani; kwasasa umefikia 100 gigawatts ambao ni robo (1/3) ya umeme unaozalishwa India. Uhaba na bei kubwa za umeme ndio kikwazo cha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya jamii katika bara hilo.
Tatizo la umeme linachochewa zaidi na fursa chache kwa wawekezaji binafsi kupewa nafasi ya kushiriki kwenye uzalishaji na usambazaji umeme.
Nchi nyingi za Afrika zinategemea umeme wa maji
Kulingana na ripoti ya Benki ya Dunia (2017) inaeleza kuwa katika nchi nyingi za Afrika, kampuni zinazomilikiwa na serikali bado zinasimamia mchakato wa kufadhili, kujenga, kuendesha na kuunganisha wateja kwenye gridi ya umeme ya taifa na kwa sehemu kubwa sekta binafsi yenye mtaji na teknolojia haihusishwi moja kwa moja katika uzalishaji huo.
Serikali za nchi za Afrika zinawekeza Dola za Marekani 12 bilioni kwenye nishati kila mwaka, lakini zilitakiwa kuwekeza Dola 33 bilioni mwaka 2015 na zitahitaji Dola 63 bilioni mwaka 2040. Ikiwa sekta binafsi haitapewa nafasi, uwezekano wa Afrika kuondokana na tatizo la umeme utakuwa mdogo.
Kukabiliana na changamoto ya uwekezaji, Benki ya Dunia inashauri Serikali za Afrika ziingie ubia na sekta binafsi ili kuongeza nguvu ya uzalishaji umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali.
Uwekezaji huo kutoka sekta binafsi unaweza kutumika kubuni vyanzo vingine vya umeme ambavyo havina gharama, kuimarisha usambazaji na kusaidia katika uzalishaji wa umeme kupitia nishati jadidifu ya Gesi, Upepo na Jua.
Sekta hiyo itaongeza ushindani, ujuzi, kuimarisha utendaji na uwazi katika sekta ya nishati. Ili hazima hiyo ifanikiwe. Serikali za Afrika zinashauriwa kubadili sera na sheria ili kuvutia wawekezaji kufanya mageuzi ya nishati ya Afrika.
“Yeyote mwenye nia ya kuwekeza ambaye haji kutukomoa. Ambaye anakuja kwaajili ya kushirikiana na Tanzania tunamruhusu aje. Sio ule uwekezaji wa siku za nyuma tuliouzoea wa kulipa macapacity charges (gharama za uzalishaji) ni marufuku kuuleta katika nchi yetu”, alisema Rais Magufuli wakati wa uzinduzi wa kituo cha kufua umeme wa gesi cha Kinyerezi II.