Sekta ya fedha yatakiwa kuongeza ubunifu kuwafikia wajasiriamali

Jamii Africa

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Florens Luoga imeitaka sekta ndogo ya benki kuongeza ubunifu kwa kutoa mikopo ya muda mfupi na mrefu ili kuboresha biashara za wajasiriamali nchini.

Prof. Luoga ametoa wito huo kufuatia kuwepo kwa changamoto katika sekta hiyo ikiwemo  ukosefu wa uwekezaji wa miradi ya maendeleo kwenye viwanda, kilimo na miundombinu na  mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati.

“Kuna kiwango cha chini cha upatikanaji wa huduma za bima za kilimo, gharama kubwa za huduma za fedha, mifumo hafifu ya kuwalinda  watumiaji wa huduma za fedha, ukosefu wa elimu ya fedha kwa wananchi na wananchi wengi kutofikiwa na huduma za fedha” amesema Prof. Luoga.

Ni asilimia 8.6 tu ya nguvu kazi ya wananchi waishio vijijini wanapata huduma za benki ikilinganishwa na asilimia 32.1 ya nguvu kazi kwa wanaoishi mijini.

Serikali ilifanya maboresho ya sekta ya fedha  katika eneo la ubinafsishaji wa benki za serikali kurekebisha na kutunga sera na sheria mbalimbali hadi kufikia desemba, 2017 ili kuweka misingi ya kuwezesha ukuaji, ushindani na ufanisi katika sekta ya fedha.

“Maboresho ya Sekta ya Fedha yamesaidia ongezeko la idadi ya benki na taasisi za fedha kufikia 54, kampuni za bima 31, kampuni zilizoorodheshwa kwenye soko la hisa 27, taasisi za huduma ndogo za fedha takriban 450, mifuko na program za Serikali 34, vikundi vya kifedha vya kijamii takribani 30,019 katika mikoa 18 ya Tanzania bara na uanzishwaji wa soko la bidhaa” amesema Prof. Luoga.

Mazingira rafiki ya utendaji wa taasisi za fedha ni kichocheo kwa sekta binafsi kuwekeza katika uchumi wa viwanda, kuongeza uzalishaji wa bidhaa zitakazouzwa nje ya nchi na hatimaye kukuza uchumi wa Taifa na kupunguza umasikini wa kipato kwa wananchi.

Aidha, serikali inandaa mpango mkakati wa maendeleo ya sekta ya fedha, unaolenga kuongeza upatikanaji wa huduma jumuishi za fedha, kulinda watumiaji wa huduma za fedha, upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu, uthabiti wa sekta ya fedha, kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kudhibiti utakatishaji wa fedha haramu na kuweka mazingira wezeshi ya sheria, kanuni na taratibu katika sekta hiyo.

 

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu, amesema mfumo thabiti wa taasisi za fedha utasaidia nchi kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

“Kuwepo kwa viwanda vingi italeta ongezeko la ajira kwa wananchi walio wengi pamoja na kuiongezea Serikali mapato” amesema Dkt. Kazungu

Ili kufikia azma hiyo, watoa huduma kwenye taasisi za fedha wameshauriwa kuongeza ubunifu kwenye utoaji wa huduma zinazokidhi mahitaji ya wapokeaji  kulingana na shughuli wanazofanya na kwa gharama nafuu.

Dkt. Kazungu amezitaka taasisi za fedha kuwekeza katika kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia taasisi hizo kwa kujiwekea akiba na kupata mitaji itakayowezesha kukuza biashara na shughuli zao za kiuchumi.

Hata hivyo, wadau wa masuala ya uchumi wamesema mikopo ya biashara kwenda kwenye sekta binafsi hairidhishi kutokana na wadau wa uchumi kudai kuwa mabadiliko ya sera na sheria yamechangia kuyumba kwa sekta fedha nchini.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Prof. Faustin Kamuzora amesema benki ziimarishe utoaji wa huduma za miamala ya fedha kwa njia ya simu ili kukabiliana na mabadiliko ya sekta ya fedha yanayotokea duniani.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Prof. Elisante Ole Gabriel ameitaka Sekta binafsi inayonufaika na mikopo inayotolewa na taasisi za fedha kuwekeza kwenye miradi yenye tija na kulipa mikopo yao kwa wakati pamoja na kuongeza thamani ya bidhaa wanazozalisha na kiwango cha mauzo ya bidhaa hizo nje ya nchi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *