Serikali ya Tanzania imeanza kunufaika na sheria mpya ya madini kwa kufanikiwa kukusanya mrabaha wa Tsh Milioni 615 kutoka kwa wachimbaji wadogo wa Tanzanite katika robo ya kwanza ya mwaka 2018.
Sheria hiyo mpya ya mwaka 2017 inakusudia kuongeza kodi za madini, kuzilazimisha kampuni kujadili mikataba kabla haijaanza kutumika, inaruhusu Serikali kumiliki asilimia 50 ya hisa za makampuni ya madini, kuhakikisha kampuni hizo zinawekeza katika mshine za kuchakata mchanga wa madini nchini na kutengeneza ajira kwa wazawa
Kwa mujibu wa Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amesema makusanyo hayo ni mara mbili ya kiasi kilichokusanywa kwa miaka mitatu iliyopita, sawa na ongezeko la asilimia 59 la mapato ya madini ya Tanzanite yanayopatikana nchini.
Mwaka uliopita, Kamati ya Bunge ilifanya uchunguzi kwenye migodi ya Tanzanite na kubaini kuwa kulikuwa na upotevu mkubwa wa mapato ya Serikali yanayotokana na kukwepa kodi. Kamati hiyo ilibaini kuwa nchi ilikuwa inapata asilimia 5.2 tu ya mapato yote ya Tanzanite inayouzwa duniani kwa miaka kumi iliyopita.
Kutokana na upotevu huo, Septemba 2017 Rais John Magufuli aliagiza Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kujenga ukuta wenye urefu wa kilomita 24 kuzunguka eneo lote la Mirerani lenye madini ya Tanzanite. Ujenzi huo ulifuatiwa na kufunga mfumo wa kisasa wa kamera za CCTV na vituo vya ukaguzi kuhakikisha eneo hilo linakuwa salama wakati wote dhidi ya biashara haramu ya madini.
“Kwa hatua hiyo, Serikali ilikusanya mrabaha wa Tsh Milioni 714.67 kwa miezi mitatu na Tsh Milioni 614.67 kutoka kwa wachimbaji wadogo wa Tanzanite,” alinukuliwa Kairuki wakati akisoma hotuba ya bajeti Bungeni.
Katika Mwaka 2017, Sekta ya Madini ilikua kwa asilimia 17.5 ikilinganishwa na asilimia 11.5 ya Mwaka 2016.
“Kuongezeka kwa kiwango cha ukuaji wa Sekta ya Madini kulitokana na kuimarishwa kwa udhibiti wa biashara haramu na utoroshwaji wa madini; kuimarishwa kwa ukaguzi na usimamizi katika sehemu za uzalishaji, biashara ya madini na usafirishaji wa madini nje ya nchi; kuongezeka kwa viwango vya mrabaha na kuanzishwa kwa ada ya ukaguzi wa madini kufuatia marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 yaliyofanyika Mwaka 2017 na Kanuni zake,” amesema Waziri Kairuki.
Wachimbaji wadogo wa madini
Wizara ya Madini inatarajiwa kutumia sh 58.90 bilioni kama bajeti yake ya mwaka 201/2019 ukilinganisha na waka uliopita wa 2017/2018 ambapo alipanga bajeti ya sh52.445 bilioni. Kiasi hicho ni sawa na asilimia 36 ya bajeti yote ya Serikali na 3.2% ya bajeti ya maendeleo.
Hali halisi
Imeelezwa kuwa ili Tanzania iwe kitovu cha uzalishaji wa vito vya madini ya Tanzanite, Serikali na wadau wa madini nchini washirikiane na kutumia sheria kutatua migogoro baina yao na wachimbaji wadogo.
Changamoto inayojitokeza ni migongano na wawekezaji kugombania maeneo ya kuchimba madini hayo. Hali hiyo inachochewa na maeneo waliyokabidhiwa wawekezaji ikiwemo kampuni ya Richland Resources kutokuyaendeleza ambapo wachimbaji wazawa huingia na kuchimba Tanzanite katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wawekezaji kutoka nje.
Kulingana na Sera ya Madini (2009) ambayo ilijenga msingi wa kuanzishwa kwa Sheria ya Madini ya mwaka 2010, inaitaka Serikali kuhamasisha, kusaidia na kuwawezesha watanzania kushiriki katika uchimbaji wa vito vya madini ili Tanzania iwe kitovu cha uzalishaji wa vito vya thamani Afrika.
Pia kuhakikisha uchimbaji wa kati na mdogo wa vito vya madini unamilikiwa na kuendeshwa na watanzania na kuwashirikisha wawekezaji wa ndani katika uchimbaji huo.
Ripoti ya Taasisi ya Umiliki wa Rasilimali Asili (2009) inaeleza kuwa mamlaka za Serikali zimeshindwa kutumia sheria na sera kikamilifu kumaliza migogoro katika eneo la Mirerani na badala yake wachimbaji wadogo wanaondolewa katika maeneo hayo ili kupisha uwekezaji mkubwa ambao utaihakikishia Serikali mapato.
Ili kutuliza migogoro ya madini, Serikali imejenga ukuta kutoka kitalu A hadi D kuzunguka eneo lote la mgodi wa Tanzanite One ili kudhibiti uchimbaji na soko la madini hayo ambayo yanapatikana Tanzania pekee. Lakini wachambuzi wa masuala ya madini wanasema njia hiyo inaweza isiwe suluhisho kumaliza migogoro na wachimbaji wadogo waliopo katika eneo hilo.`
Imeelezwa kuwa njia sahihi ni kuweka mfumo wezeshi ambao utawakutanisha wachimbaji wadogo na wawekezaji wa kigeni kufanya kazi pamoja kwa kuzingatia matakwa sheria.