Shinikizo la Damu la Juu, Homa ya Dunia!

Dr. Joachim Mabula
Doctor taking blood pressure of a patient

Si rahisi kwa binadamu yeyote kukubali ushauri wa daktari pale anapogundulika amepatwa na ugonjwa wa shinikizo la damu.

Na, mazoea yanaonyesha kuwa inakuwa ngumu zaidi pale daktari anapo mshauri mgonjwa husika kutumia dawa maisha yake yote, ili kudhibiti madhara yatakanayo na kupanda kwa shinikizo la damu.

Madaktari hutaja baadhi ya madhara yatokanayo na kutotibiwa au kutodhibitiwa kwa ugonjwa wa shinikizo la damu.

Madhara hayo ni kama vile kiharusi, moyo kushindwa kufanya kazi, matatizo katika mshipa mkubwa wa damu ambapo ukuta wa ndani huchanika na damu kukusanyika katika ukuta wa mshipa huo, magonjwa ya mishipa ya damu, kushindwa kuona na pia huathiri ubongo.

Lakini hii ndiyo hali halisi hapa Tanzania na kwingineko duniani ambako kupanda kwa shinikizo la damu hudhuru mamilioni ya watu. Huku takwimu kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) zikionyesha kwamba mmoja kati ya watatu duniani ameathiriwa na ugonjwa huu.

Shinikizo la damu ni msukumo wa damu kwenye kuta za mishipa. Shinikizo la damu ni muhimu kwa ajili ya kusukuma damu katika sehemu zote za mwili, lakini shinikizo la damu la juu huweza kuleta matatizo na madhara makubwa kiafya.

Shinikizo la damu la juu (Hypertension) au presha ya damu ya juu (High Blood Pressure), pia huitwa shinikizo la mishipa (Arterial Hypertension) ni hali ya ugonjwa sugu ambapo nguvu ya msukumo wa damu katika mishipa inaongezeka.

Ongezeko hilo husababisha moyo kufanya kazi kupita kiasi ili uzungushe damu katika mishipa ya damu.

Shinikizo la damu linaweza kupimwa na kifaa maalumu kinachojulikana kitaalamu Sphygmomanometer/Sphygmometer/Blood Pressure Meter.

Kifaa hiki huonyesha muhtasari wa vipimo viwili. Kwa mfano kinaweza kurekodi kipimo cha 110/70. Nambari ya kwanza huonyesha kipimo cha shinikizo la damu wakati moyo unapopiga (Systole). Nambari ya pili huonyesha kipimo cha shinikizo la damu katikati ya mapigo ya moyo (Diastole).

Shinikizo la damu hupimwa kulingana na milimeta za zebaki (Millimeter Mercury/mmHg).

Kipimo cha kawaida cha shinikizo la damu ni 100-140 milimeta za zebaki (mmHg) kipimo cha juu (Systolic) na 60-90 milimeta za zebaki (mmHg) kipimo cha chini (Diastolic). Shinikizo la damu la juu hutokea kama kipimo kikiwa zaidi ya 140/90 milimeta za zebaki (mmHg) kwa muda mrefu.

Ugonjwa huu kwa kawaida huitwa muuaji wa kimya kimya (Silent Killer) kwa maana kuwa, mtu anaweza akawa na ugonjwa huo kwa miaka kadhaa lakini bila kujua, huku ugonjwa huo ukimletea madhara makubwa.

Shinikizo la damu kwa kawaida huongezeka katika kipindi cha miaka kadhaa na huweza kumpata karibu kila mtu, lakini huwapata zaidi wenye umri wa zaidi ya miaka 35.

Takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) zinasema tayari watu bilioni moja duniani kote, wanaathiriwa na shinikizo la damu la juu likisababisha mshtuko wa moyo (Heart Attacks)  na kupooza/kiharusi (Strokes).

Watafiti wamekadilia watu kama milioni nane hufa kila mwaka kwa kupanda kwa shinikizo la damu.

AINA ZA SHINIKIZO LA DAMU LA JUU

Kuna aina mbili za shinikizo la damu la juu. Aina ya kwanza ni shinikizo la damu la juu la asili (Primary/Essential Hypertension) na aina ya pili ni shinikizo la damu la juu linalosababishwa na magonjwa mengine (Secondary Hypertension).

Inakadiriwa asilimia 90-95 ya watu wenye shinikizo la damu la juu wanaathiriwa na shinikizo la damu la juu la asili, yaani wana ugonjwa huu bila kuwa na chanzo cha kisayansi kinachofahamika.

Shinikizo la damu la juu linalosababishwa na magonjwa mengine kama ya figo, mishipa, moyo, mfumo wa homoni huathiri asilimia 5-10 iliyobaki ya watu wenye shinikizo la damu la juu.

Sababu nyingi huathiri ugonjwa wa shinikizo la damu kama wingi wa maji mwilini, wingi wa chumvi mwilini, homoni, kiwango cha mishughuliko, hali ya joto au hali ya baridi, hali ya hisia, hali ya figo, mfumo wa neva, na mishipa ya damu.

MGAWANYIKO WA SHINIKIZO LA DAMU KULINGANA NA RIKA/HALI

=> Watoto waliozaliwa karibuni (Neonates) & watoto wachanga (Infants).

Sio kawaida kwa watoto waliozaliwa karibuni kuwa na shinikizo la damu la juu na ni asilimia 0.2-3 tu ya watoto wachanga ambao wanapata. Shinikizo la damu halipimwi mara kwa mara kama watoto ni wadogo na wana afya mzuri.

Kuna masuala tofauti ya kuangalia, kama vile kipindi cha ujauzito, umri baada ya utungaji momba, na uzito wakati wa kuzaliwa kabla ya kuamua kama kipimo cha shinikizo la damu ni cha kawaida kwa mtoto mchanga.

=> Watoto (Children)

Ni kawaida kwa watoto na vijana kupata shinikizo la damu la juu (Asilimia 2-9 hutegemea na umri, jinsia na asili) na huambatana na afya mgogoro/dhaifu.

Hivi sasa kuna pendekezo la kuwapima shinikizo la damu watoto wenye zaidi ya miaka mitatu na kuangalia kama wana shinikizo la damu la juu kila wanapoenda kupima afya zao.

Shinikizo la damu la juu kwa watoto huthibitishwa ikiwa wastani wa kipimo cha juu (Systolic Pressure) au kipimo cha chini (Diastolic Pressure) vilivyopimwa nyakati tatu tofauti ni asilimia 95 au zaidi kulingana na jinsia, umri na kimo cha mtoto.

=> Vijana (Adolescents)

Kwa vijana, inapendekezwa kwamba shinikizo la damu la juu la na dalili za shinikizo la damu la juu zichunguzwe na kuainisha kwa kutumia vigezo vya watu wazima.

=> Watu wazima (Adults)

Kwa watu wenye umri wa miaka 18 au zaidi, shinikizo la damu la juu linaweza kuwa kama kipimo hicho ni zaidi kuliko kipimo cha kawaida kinachokubalika ambacho ni 139/89 milimeta za zebaki (mmHg).

=> Kipindi cha ujauzito (Pregnancy)

Shinikizo la damu la juu hutokea takribani asilimia 8-10 ya ujauzito. Tunasema mwanamke ana shinikizo la damu la juu ikiwa shinikizo la damu yake ni zaidi ya 140/90 milimeta za zebaki (mmHg) lililopimwa kwa nyakati tofauti zinazotofautiana masaa 6.

Wanawake karibu wote wenye shinikizo la damu la juu wakiwa na mimba walishakwisha umwa na shinikizo la damu la juu la kawaida.

Hali hiyo ikitokea katika ujaizito ni dalili ya kwanza ya kifafa cha mimba kabla hakijashikika kabisa.

Maradhi hayo hutokea katika kipindi cha miezi mitatu ya pili ya ujauzito (Second Trimester) na majuma machache baada ya kujifungua.

Uaguzi wa maradhi hayo ni pamoja na shinikizo la damu kuongezeka na dalili za protini ndani ya mkojo.

Maradhi hayo hutokea takribani asilimia 5 ya ujauzito yakisababisha takribani asilimia 16 ya vifo vya wenye ujauzito.

SABABU ZA KUPANDA SHINIKIZO LA DAMU

Shinikizo la damu hupanda wakati damu nyingi inapopita mshipani au wakati mshipa unapokuwa mwembamba.

Mtu anaweza kupata ugonjwa huu kwa mambo yasiweza kuepukika na mambo yanayoweza kuepukika.

Mambo yasiyoweza kuepukika mfano kurithi tatizo la kupanda kwa shinikizo la damu kupitia kuzaliwa pamoja kwenye familia yenye watu wenye shinikizo la damu la juu.

Pia inasemekana kwamba uwezekano wa kupata tatizo hilo huongezeka mtu anapozidi kuzeeka na kwamba wanaume wenye asili ya afrika wanakabili uwezekano mkubwa zaidi wa kupata ugonjwa huo.

Mambo unayoweza kuepuka ni pamoja na matumizi ya chumvi (Sodium). Hii inahusu hasa wagonjwa wa kisukari, watu ambao shinikizo la damu hupanda sana, wazee na watu fulani weusi.

Mafuta mengi katika damu yanaweza kufanyiza utando wa kolesteroli (Cholesterol) kwenye kuta za ndani za mishipa. Hivyo, mishipa huwa myembamba na shinikizo la damu huongezeka.

Watu ambao ni wazito kupita kiasi kwa asilimia 30 wanaweza kupata tatizo la kupanda kwa shinikizo la damu.

Uvutaji wa sigara unaweza kusababisha utando mgumu wa mafuta kwenye kuta za mishipa, ugonjwa wa kisukari, mshtuko wa moyo na kiharusi.

Ijapokuwa uthibitisho unapingana, kafeini inayopatikana katika kahawa, chai na vinywaji vya kola yaweza kusababisha tatizo la kupanda kwa shinikizo la damu.

Kunywa kileo mara nyingi na kupita kiasi na kutofanya mazoezi kwaweza kuongeza shinikizo la damu.

DALILI NA ISHARA (SYMPTOMS & SIGNS) ZA KUPANDA SHINIKIZO LA DAMU

Mara nyingi watu wenye shinikizo la damu la juu hawana dalili za moja kwa moja na huwa inagundulika baada ya kufanya uchunguzi kwa kawaida au wakati maangalizi ya afya yanafanywa kwa sababu nyingine.

Watu wengine wenye shinikizo la damu la juu huwa wanapata maumivu ya kichwa (Haswa nyuma ya kichwa mara nyingi nyakati za asubuhi), pamoja na kuchanganyikiwa, kizunguzungu, kelele sikioni (Mvumo au Mazomeo masikioni), kutoweza kuona vizuri au matukio ya kuzirai.

KUJUA KAMA SHINIKIZO LA DAMU LIMEPANDA

Pale mtu anapokuwa na dalili za kupanda kwa shinikizo la damu, hupaswa kufika kwa wataalamu wa afya kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi ili kubaini kama shinikizo la damu limepanda.

Vipimo vya shinikizo la damu vinapatikana katika vituo vya afya na wajuzi mbalimbali wa afya wanaweza kuvitumia.

Kipimo kimoja cha shinikizo la damu hakimaanishi kupatikana au kuugua ugonjwa huo, inanidi kupimwa zaidi ya mara mbili kwa nyakati tofauti.

Kama shinikizo lako la damu liko juu, ni muhimu kufanyiwa uchunguzi zaidi wa matatizo mengine ya kiafya.

Vipimo vingine ni pamoja na kuchunguza damu ili kufahamu wingi wa kolesteroli (Cholesterol) mwilini, kupimwa BUN na electrolytes, kuchunguza mkojo (Urinalysis), ECG, Echocardiography na pia ultrasound ya figo.

JINSI YA KUISHI NA SHINIKIZO LA DAMU LA JUU

Mabadiriko ya maisha hupendekezwa ili kushusha shinikizo la damu lililopanda kabla ya kuanza matumizi ya dawa za tiba (Antihypertensives).

=> Kudumisha uzito wa mwili wa kawaida. Kwa mfano Mwili Molekuli Index (BMI) ya 20-25 kg/m°2

=> Kupunguza kiasi cha chumvi (Sodium) unachotumia.
Kupunguza ulaji wa sodium kwa < 100 mmol/siku (<6g ya kloridi sodium au < 2.4 g ya sodium kwa siku).

=> Kufanya mazoezi kwa ukawaida.
Kushiriki katika shughuri za mara kwa mara za kimwili kama vile kutembea upesi kwa dakika 30 au zaidi.

=> Usinywe sana kileo.
Watafiti fulani wanasema kwamba wanaume walio na ugonjwa wa kupanda kwa shinikizo la damu hawapaswi kunywa zaidi ya mililita 30 za kileo kila siku, wanawake na vilevile watu ambao si wazito sana hawapaswi kunywa zaidi ya mililita 15 za kileo.

Kileo cha mililita 30 kinalinganishwa na mililita 60 za vinywaji aina ya Spirits kama wiski & vodka, kadhalika mililita 240 za divai (Wine) au mililita 720 za pombe (Beer).

=> Kutumia lishe yenye matunda na mboga.
Kwa mfano angalau visehemu vitano kwa siku.

=> Kula vyakula vingi vyenye potasiamu, magnesi na kalisi.
Uchunguzi mbalimbali unaonyesha kwamba kula vyakula vingi vyenye potasiamu na kalisi kwaweza kupunguza shinikizo la damu.

=> Dhibiti mfadhaiko.

=> Acha kuvuta sigara.

=> Dhibiti kiwango cha kolesteroli (Choresterol).

=> Dhibiti ugonjwa wa kisukari.

=> Usitumie dawa zinazoweza kuongeza shinikizo la damu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *