Ni matamanio ya kila mtu kuwa na afya bora itakayomuwezesha kuishi maisha marefu ili kutimiza kusudi la kuja duniani. Lakini mtindo wa maisha usiozingatia kanuni za afya umefupisha maisha ya watu wengi.
Usihofu sana juu ya maisha yako, kwani wanasayansi wamegundua tiba mpya ya kukuwezesha kuishi maisha marefu! Twende pamoja kuifahamu tiba hiyo.
Kwa mujibu wa utafiti mpya uliofanyika nchini Marekani umebaini tabia 5 ambazo mtu akizifuata kwa usahihi anaweza kuongeza umri wa kuishi kwa miaka 10 zaidi alionao.
Tabia hizo zinajulikana- kula mlo kamili, kufanya mazoezi, kuepuka vileo, uvutaji wa sigara na unene uliopitiliza. Lakini utafiti unaweka mkazo kwa kiasi gani tabia hizo zinaweza kuathiri afya na maisha ya mtu.
Matokeo ya utafiti huo yalichapishwa kwenye jalida la Circulation ambapo watafiti wameibaini kuwa tabia hizo tano zikitekelezwa kwa usahihi zinaweza kuongeza umri wa kuishi wa mwanamke kwa miaka 14 zaidi na mwanaume ataongezewa miaka 12.
Watafiti hao walichambua data kutoka tafiti kubwa mbili za nchini Marekani zilizofanyika kati ya mwaka 1980 hadi 2014, ambapo waliwashirikisha wanawake 79,000 na zaidi ya wanaume 44,300.
Watu hao walijaza hojaji kuhusu afya zao na mtindo wa maisha yao mara mbili kwa miaka 4, huku watafiti wakifuatilia kwa karibu jinsi wanavyofuata tabia 5 ambazo zimeainishwa kwenye utafiti.
Watu walihesabika kuwa wanakula mlo kamili ikiwa walipata zaidi ya asilimia 40 ya maswali waliyojibu. Kwa upande wa unywaji pombe, wanawake walihesabika kwamba wanakunywa kiasi ikiwa walikunywa pombe kidogo kwa siku na wanaume kama walikunywa mara mbili kwa siku.
Uzito sahihi uliokubalika ni kati ya bmi 18.5 hadi 24.9 (body mass index). mazoezi; kama mtu alifanya mazoezi kwa dakika 30 kwa siku na kigezo cha mwisho ilikuwa ni kutokuvuta kabisa sigara.
Watafiti walifuatilia maisha ya watu hao kwa miaka 34. Lakini katika kipindi hicho, zaidi ya watu 42,000 walikufa. Takribani vifo 14,000 vilitokana na kansa, na vifo 10,700 vilikuwa vya magonjwa ya moyo.
Wale waliozingatia tabia zote 5 waliweza kuishi kwa asilimia 74 katika kipindi chote cha uangalizi kuliko wale ambao hawakufuata tabia hata moja.
Mbali na vigezo vya jumla vya kupunguza hatari ya kufa, asilimia 82 ya kundi hilo walikuwa na uwezekano mdogo wa kufa kwa magonjwa ya moyo huku 65% waliepuka vifo vinavyotokana na kansa.
Matokeo ya utafiti huu yanatukumbusha umuhimu wa kutathmini mtindo wa maisha tunayoishi. Je unataka kuishi maisha yenye afya kwa muda mrefu? Basi fuata tabia 5 na ziwe sehemu ya maisha yako.
Dunia bado inakuhitaji kutimiza kusudi lako ili kuyafanya mazingira unayoishi kuwa bora zaidi kwa vizazi vijavyo. Ni tabia tano- mazoezi, mlo kamili, epuka pombe, sigara na unene uliopitiliza!