Nianze kwa kutoa pongezi kwa wanawake wenzangu wote ulimwenguni kwa kuadhimisha hii siku yetu muhimu katika harakati zetu za kujikomboa na mfumo dume.
Leo naomba nitumie siku hii kutoa changamoto kwa wanasiasa na wanaharakati wanawake nchini mwetu Tanzania kujipanga na kuhakikisha wanawania na kushikilia nafasi muhimu za juu katika uongozi wa nchi hii. Walau tupate japo mwanamke mmoja katika nafasi yoyote kati ya hizi za Rais wa nchi, Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Spika wa Bunge.
Sio rahisi kukamilika kwa nia yetu hiyo, ila tukijiamini na kuthubutu tutaweza bila shaka yoyote. Wapo wanawake katika nafasi nyingine za uongozi wa kiserikali ambao wana upeo mkubwa wa kushika hizo nafasi endapo watajiamini na kuthubutu kuziwania. Wanawake kama Dr. Asha Rose Migiro, Dr. Gertrude Mogella, Dr. Anna Tibaijuka, Dr. Mary Nagu na wengineo ni wanawake wenzetu wasomi, wana uzoefu, wapo kwenye siasa muda mrefu na upeo wao juu ya masuala ya kijamii ni mkubwa sana kwa sasa! Wana vigezo vyote vya kuwania hizi nafasi na wakashinda na kufanikiwa kuzitumia vyema!
Kinachotakiwa ni sisi wanawake wengi wetu tulio nguvu ya umma kuwaunga mkono vya kutosha kuhakikisha lengo letu la mwanamke mwenzetu kutufungulia njia kushika nafasi nyeti ya kiserikali linafanikiwa haraka iwezekenavyo. Misemo ya kizamani na isiyo na mantiki wala tija kama “Adui wa mwanamke ni mwanamke mwenzie” isipewe tena nafasi baina yetu kwani ni propaganda za mfumo dume!
Wanawake wenzetu duniani wameshafungua njia na wamefanikisha hili. Mfano ni jirani zetu Uganda tu hapo Naibu Waziri Mkuu (Eriya Kategaya) ni mwanamama mwenzetu, huko Ujerumani Bi Angela Mercel aliwania na kushinda nafasi ya juu kabisa ya kuwa Kansela sawa na wadhifa wa Rais nchini mwetu. Brazili pia Bi Dilma Rousseff ameshinda kiti cha urais. Hata Liberia pia wana Raisi mwana mama Bi Ellen Johnson Sirleaf.
Wito wangu kwenu wanawake wenzangu, 2015 tuweke ujinsia mbele kuliko ushabiki wa kivyama. Ukiona mwanamke mwenzio kathubutu na kagombea wadhifa wowote ule, mtie moyo na muunge mkono ili kuwezesha nia yetu ya kina mama wengi zaidi kupata nafasi za kuwania wenyewe kwenye serikali itakayoingia madarakani 2015 na si kutegemea viti vya upendeleo. Bila jitihada zetu binafsi, mfumo dume utaendelea kutawala serikali wakati sisi tukiwatizama.
Pia natoa wito kwa vyama vya siasa kuwatia moyo kina mama watakaojitokeza kuwania nafasi mbali mbali kwa tiketi ya vyama vyao vya siasa. Wawape nafasi wanawake thabiti, wenye uwezo wa kuongoza na watakaoleta tija na mafanikio katika uongozi wao si mradi ni mwanamke.
Kina mama wenzangu, wakati wetu ndo huu! Tumeungojea karne na karne toka enzi za kabla ya kuja kwa Kristu wakati wanawake hatuhesabiwi, tukajikongoja mpaka tukaruhusiwa kusoma, hatukata tamaa, mpaka tukapewa nafasi kwenye uongozi wa dini na kijamii. Sasa tulikofika si kubaya ila sio mwisho wa Safari! Tumekula ng’ombe mzima amebakia mkia! Tuungane kuumalizia mkia huo!