Tanzania yaondolewa 10 bora vivutia vya uwekezaji Afrika

Jamii Africa

Inaelezwa kuwa serikali ya Tanzania inaweza isifikie lengo lake la kujenga uchumi wa viwanda kutokana na mabadiliko ya sera za usimamizi wa fedha na rasilimali ambazo sio rafiki kwa wawekezaji.

Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti ya taasisi ya Qutinum Global Research Lab (Machi, 2018) juu ya Uwekezaji barani Afrika imebaini kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 13 kwa uwezo wa kuvutia wawekezaji ikilinganishwa na April, 2017 ambapo ilishika nafasi ya 8 na kuwa miongoni mwa nchi 10 za Afrika zenye mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji.

Utafiti huo ulihusisha nchi 54 za Afrika umeiweka nchi ya Morocco katika nafasi ya kwanza kuvutia wawekezaji ikifuatiwa na Misri, Algeria, Botswana, Ivory Coast, Afrika Kusini, Ethiopia, Zambia, Kenya na Senegal. Nchi 10 za mwisho ambazo zilishindwa kukidhi vigezo vya kuvutia wawekezaji ni Jamhuri ya Afrika ya Kati, Liberia, Somalia, Eritrea, Equatorial Guinea, Gambia, Sierra Leone, Guinea, Sao Tome na Zimbabwe.

Vigezo vilivyotumika katika upangaji wa madaraja ya vivutio vya uwekezaji katika nchi za Afrika ni kiwango cha ukuaji wa uchumi, mzunguko wa fedha, nguvu ya sarafu (current account ratio), urahisi wa kufanya biashara. Vigezo vingine ni ukuaji wa idadi ya watu na matumizi ya mtaji wa mitandao ya kijamii ikiwemo facebook.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa kushuka kwa Tanzania kwenye nchi zilizo na mvuto kwa wawekezaji hadi nafasi ya 13 kunatokana na mabadiliko ya sera za fedha na mazingira magumu ya kuanzisha na kufanya biashara ambayo yanaathiriwa zaidi na ongezeko la kodi na upatikanaji wa leseni za biashara.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia (WB), urahisi wa kuanzisha biashara nchini Tanzania uko chini ya wastani unaotakiwa na nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, sababu inayokwamisha ukuaji wa sekta binafsi na uchumi wa wananchi.

Benki ya Dunia inaeleza kuwa Tanzania imeangushwa na ongezeko la ada ya usajili inayotozwa kwenye ardhi na makazi ambako biashara mpya zinafunguliwa. Pia ukiritimba wa upatikanaji wa leseni na   mrundikano wa kodi kwa wafanyabiashara na kodi mpya inayokatwa kwenye mishahara ya wafanyakazi. Yote haya yamekuwa kikwazo kwa wawekezaji kuja nchini.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa mabadiliko ya sera za fedha hasa uamuzi wa serikali kupunguza mahusiano na benki binafsi umeathiri mzunguko wa fedha na viwango vya kubadilisha fedha za kigeni.

Inaelezwa kuwa ukopeshaji katika benki za biashara umepungua kwasababu serikali imeamua kutunza fedha zake zinazokusanywa katika maeneo mbalimbali kwenye Benki Kuu ya Tanzania (BOT).

Hali hiyo imezikosesha benki nyingi fedha ambayo ilikuwa inapelekwa kwenye mzunguko wa biashara na sekta binafsi ili zitumike kama dhamana ya kuendesha bishara zao. Tafiti zinaeleza kuwa mzunguko wa fedha umepungua kutoka asilimia 22 mwaka 2011 hadi kufikia 1.8% mwaka huu ambapo ukuaji wa usafirishaji wa bidhaa hasa mazao ya kilimo umeshuka.

Athari za ongezeko la kodi limejidhihirisha pia katika sekta ya usafirishaji na ughavi ambapo mizigo iliyokuwa inapitia bandari ya Dar es salaam imepungua na usafiri wa malori kutoka na kuingia nchini umepungua kutokana na mabadiliko ya kibiashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Sababu hizo zimetajwa kama tishio kwa wawekezaji kuwekeza mitaji yao nchini.

 

Tumaini lililobaki…

Hata hivyo, Tanzania ina nafasi ya kufanya vizuri siku zijazo kwasababu ina ukuaji mzuri wa uchumi, idadi ya watu ambao wakiandaliwa vizuri kifikra na kiteknolojia wataweza kuongeza nguvu kazi katika uzalishaji na soko la bidhaa za wawekezaji.

Kulingana na Benki ya Dunia, Tanzania ni miongoni mwa nchi tano za Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi, ambapo hadi kufikia 2015 uchumi wake ilikuwa umekua kwa zaidi ya asilimia 5.4. Kulingana  na takwimu za serikali uchumi umeimarika na kukua kwa asilimia 6.8 kwa mwaka 2017

Pia matumizi ya mitandao ya kijamii ikiwemo facebook yameongezeka nchini ambapo wigo wa mawasiliano umetanuka na kuifanya nchi kufikika kirahisi. Lakini pia imechochea matumizi ya teknolojia ya kisasa miongoni mwa raia.

Licha ya juhudi mbalimbali za nchi za Afrika kuvutia wawekezaji, uwekezaji kutoka nchi zilizoendelea ulipungua kwa mwaka 2016 ambapo ulifikia Dola za Marekani 59 bilioni. Lakini wachambuzi wa masuala ya uchumi wanasema uwekezaji utaimarika kwasababu nchi nyingi zimeboresha miundombinu ya barabara, reli na viwanja vya ndege.

Katika sekta ya usafiri wa anga, Tanzania imeendelea na upanuzi wa uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Dar es salaam na viwanja vingine nchini ili kuziwezesha ndege kubwa kutua nchini. Pia imenunua dege mbili aina ya Bombardier na mwakani ndege mbili kubwa zitawasili nchini.

Pia Serikali inatarajia kujenga reli ya kisasa (Standard Gauge) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ambayo itagharimu zaidi ya bilioni 400. Ikikamilika pia itaunganishwa mpaka mkoa wa Mwanza.

Mradi mkubwa wa upanuzi wa bandari unaojulikana kama ‘Dar es Salaam Marine Gateway Project (DMDP)’ ambao unalenga kuifanya bandari hiyo kuwa na hadhi ya kimataifa na kuwezesha kupokea meli kubwa na kuhifadhi mizigo mingi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *