Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa amewatoa wasiwasi wananchi wa mkoa huo kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Ebola ambao umeuikumba nchi ya jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Congo DRC).
Mkuu wa Mkoa huyo amesema hakuna tukio lolote la kuwepo kwa ugonjwa huo katika mkoa wake lililoripotiwa lakini amewataka wananchi hao kuchukua tahadhari za kiafya ili kujikinga na maambukizi yoyote yanayoweza kutokea.
Mkoa wa Songwe unapatikana Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania na unapakana na nchi ya Zambia ambayo ina muingiliano wa karibu na wananchi wa Congo DRC. Kutokana na hali hiyo, uongozi wa mkoa wa Songwe umeimarisha ukaguzi katika kituo chake cha mpakani cha Tunduma kilichopo wilaya ya Momba.
“Tunaimarisha kituo cha kupokea wageni mpakani mwa Tunduma na Zambia, watakaogulika kuwa na tatizo hilo watahifadhiwa eneo maalum kwaajili ya uangalizi na tiba,” amesema Galawa.
Kwa mujibu wa Galawa akinukuu takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) amesema ugonjwa huo uliolipuka Congo DRC umeua watu 17 na mpaka sasa kuna wagonjwa 21 katika vituo maalum vya matibabu.
Hata hivyo, Kamati ya ulinzi na usalama katika wilaya ya Momba inakutana na uongozi wa Wilaya ya Nakonde ya nchi jirani ya Zambia ili kuweka mikakati ya ukaguzi mpakani mwa nchi hizo mbili na kuhakikisha wageni wanaoingia na kutoka hawasambazi virusi vya ugonjwa huo.
Tanzania inachukua tahadhari ya ugonjwa huo ikizingatiwa kuwa imekuwa na mahusiano ya kidiplomasia na kibiashara ya muda mrefu na Congo DRC ambayo yanauungwanishwa zaidi na usafiri wa bandari ya Dar es Salaam, Reli ya TAZARA na mtandao wa barabara.
Miundombinu hiyo ya usafiri imekuwa kiungo muhimu kwa usafirishaji wa bidhaa kutoka bandari ya Dar es Salaam ambazo zimekuwa zikisafirishwa kwa malori ambayo yanapita nchi ya Zambia na kuingia Congo DRC. Pia DRC imekuwa ikisafirisha madini yake kwenda nchi za ng’ambo kupitia bandari ya Dar es Salaam.
Ebola ni ugonjwa unaotokea katika kipindi fulani na kuua watu wengi kwa muda mfupi.
Kutokana na mahusiano hayo ya karibu ni rahisi kwa virusi vya ebola kusambaa kwa haraka katika nchi za jirani ikiwemo Tanzania.
Kinachoendelea Congo DRC
Kwa taarifa zilizopo, tayari watu 17 wamefariki kutokana na ugonjwa wa virusi vya Ebola katika mji wa Bikoro uliopo Kaskazini Magharibi mwa Congo DRC. Ebola ni ugonjwa unaotokea katika kipindi fulani na kuua watu wengi kwa muda mfupi.
Ni hatua gani ambazo Congo DRC inapaswa kuchukua wakati huu?
Mamlaka za afya nchini humo tayari zimejifunza masomo ya msingi kutokana na milipuko ya ugonjwa huo iliyowahi kutokea mwaka 2014 hasa katika nchi za Afrika Magharibi ambapo zaidi ya watu 11,000 walikufa.
Kwasababu Congo RDC imekumbana na milipuko ya ugonjwa huo siku za nyuma imeimarisha uwezo wake wa kukabiliana na maambukizi mapya. Lakini kama ilivyo kwa magonjwa mengine ambayo yanatishia afya ya dunia, ni muhimu kwa nchi za jirani kushirikiana kuhakikisha mlipuko huo unadhibitiwa mapema kabla haujasambaa katika eneo kubwa.
Kwanza, mamlaka za afya zinatakiwa kubaini ukubwa wa tatizo. Pili wanatakiwa kuingilia kati na kuvunja mnyororo wa maambukizi haraka iwezekanavyo.
Taarifa za mtandao wa Quartz Afrika zinaeleza kuwa tayari wametuma wataalamu ili kufahamu lini na wapi ambako watu wameathirika zaidi, wapi walipotoka au kusafiri tangu waathirike. Uchambuzi huo utasaidia kuelewa kiasi cha maambukizi kutoka mtu mmoja kwenda kwa mwingine.
Baada ya zoezi hilo kukamilika, serikali itachukua hatua stahiki. Hatua mbalimbali za kudhibiti zitaanzishwa haraka ikiwemo kuzuia na matibabu. Katika mtazamo wa kuzuia ni vema serikali ikashirikiana na jamii ili watu waelewe mlipuko wenyewe na jinsi unavyosambaa.
Kwa mtazamo wa matibabu, mamlaka za afya zinatakiwa kujenga vituo vya matibabu na upatikanaji wa maabara za vipimo. Kulingana na kiwango cha vifo, wataalamu watafanya uchunguzi wa kina ili kubaini chimbuko la mlipuko wa Ebola. Hii ndiyo njia pekee ya kuvunja mnyororo wa maambukizi.
Wataalamu wanafanya uchunguzi wa kina ili kubaini chimbuko la mlipuko wa Ebola.
Changamoto zinazokwamisha udhibiti wa virusi vya ugonjwa huo nchini Congo DRC?
DRC imekuwa na milipuko mingi ya Ebola kuliko nchi yoyote duniani. Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita kumekuwa na milipuko 5: 2007, 2008 hadi 2009, 2012, 2014 na 2017.
Matokea yake nchi hiyo imepata uzoefu wa kutosha jinsi ya kudhibiti ugonjwa huo. Lakini bado kuna sintofahamu. Moja ya pengo kubwa ni kuelewa mabadiliko ya maambukizi ya virusi kutoka kwa wanyama walioathirika hadi kwa binadamu.
Nchi hiyo ina mfumo mzuri wa kushughulika na ugonjwa huo-maabara zake zilikuwa na uwezo wa kupima na kuthibitisha kesi za virusi ndani ya saa 24. Lakini mifumo yake ya uchunguzi na ufuatiliaji ni dhaifu. Mfumo imara ya uchunguzi ingehakikisha kesi zinaripotiwa mapema na mamlaka husika zinakuwa tayari kukabiliana nazo.