Tathmini ya mwaka: Tanzania inatekeleza ipasavyo haki ya kuishi?

Jamii Africa

Kuishi ni haki ya msingi ambayo binadamu anatakiwa kuwa nayo ili apate stahili nyingine akiwa hai, lakini mifumo ya uongozi katika nchi mbalimbali imekuwa kikwazo kutekeleza haki hiyo na matokeo yake uhai wa baadhi ya watu unatoweka ili kulinda maslai ya watu wachache katika jamii. 

 Neno haki za binadamu ni muunganiko wa maneno mawili haki na binadamu. Ukiuliza nini maana ya neno haki utaambia ni stahili alizonazo mtu na anatakiwa azipate ili zimuwezeshe kuishi. Lakini utata unabaki katika neno binadamu ambapo hutafsiriwa tofauti kulingana na mazingira husika anayoishi huyo binadamu.

Wako binadamu na wasio binadamu kwa sababu binadamu ni dhana ya kiitikadi ambayo humtambulisha mtu na stahili muhimu alizonazo katika maisha ya kila siku. Ikiwa mtu hana sifa ya kuwa binadamu basi hana stahili muhimu zinazomuwezesha kuishi katika mazingira yanayomzunguka, na hapo ndipo ubinadamu hujitokeza.

Ubinadamu ni dhana ya kihistoria ambayo hutengeneza matabaka mawili ambayo huwa na uhasimu kwa kila kundi kupigania haki za msingi za kuishi katika mazingira mazuri.

Katika mfumo wa ujamaa/ujima watu  waliopo katika jamii bila kujali matabaka ya uongozi, umri na jinsia humiliki rasilimali zinazowazunguka kwa usawa na haki bila kubaguliwa na kunyanyaswa. Pia utajiri unaopatikana katika shughuli za maendeleo huwanufaisha wananchi wote ambapo hustawi wa jamii huzingatia zaidi.    

Mfumo huu wa maisha unawapa fursa watu wote waliopo katika jamii kuwa na sifa ya kuwa binadamu ambao wanapata stahili zao za kila siku. Tabaka la wenye kutumia rasilimali zaidi ya wengine halina nafasi katika mfumo huu.  Jamii nyingi zimejaribu kuishi chini ya mfumo huu lakini imekuwa vigumu kuutimiza kwa kuwa binadamu tunazaliwa tofauti katika tabia na mitazamo lakini tunaunganishwa na sheria na kanuni zilizowekwa kwenye jamii.

Mfumo mwingine wa maisha wa kikabaila (Ubepari) ambapo umiliki wa  rasilimali za jamii huwa katika mikono ya watu wachache  na kundi linalobaki ambalo hujumuisha wananchi wa kawaida humiliki sehemu ndogo ya rasilimali za jamii na kukosa haki za msingi za kuwawezesha kuitwa binadamu.

  Mfumo huu wa kisiasa ndio unaotumika kuongoza mataifa mengi duniani ikiwemo Tanzania yenye mfumo wa kijamaa lakini inatekeleza sera za mabepari ambazo zina matabaka mawili ya binadamu na wasio binadamu. Kundi la binadamu ndilo lina nguvu kubwa ya kisiasa na kiuchumi ambapo hutumia mamlaka hiyo kunyanyasa na kuwanyonya wasio binadamu.

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu  akiwa hospitali ya Nairobi nchini Kenya ambako anapatiwa matibabu baada ya kupigwa risasa mwezi Septemba mwaka huu.

Hawa wasio binadamu ndio wanaokumbwa na matatizo makubwa ya umaskini na hata wakitaka kupigania haki zao katika jamii hukumbana na vitisho na upinzani kutoka kwenye kundi la binadamu ambao hawataki kuguswa katika maslahi yao.

Katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia matukio ya watu kupotea katika mazingira ya kutatanisha na wengine kupigwa risasi na watu wasiojulikana kwasababu wanapigania usawa na haki za raia maskini. 

Tunafikia ukingoni mwa mwaka 2017 pasipo kuwaona baadhi ya watu ikiwemo mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda na mwanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ben Saanane na wananchi wengine ambao hawajulikani walipo tangu walipotea katika mazingira yasioelezeka. Pasi na shaka uhai wa raia hawa umewekwa rehani ikizingatiwa kuwa walikuwa sehemu muhimu katika kupigania haki na usawa katika jamii.

Pia tumeshuhudia kuokotwa kwa miili ya watu waliokufa wakiwa wamefungwa kwenye mifuko ya plastiki kwenye fukwe za bahari ya Hindi. Kulingana na taarifa za Jeshi la Polisi mpaka sasa ni zaidi ya maiti 8 zimeokotwa katika fukwe za Coco jijini Dar es Salaam.

Maiti ya mtu ikiwa imefungwa kwenye kiroba

 

Kirahisi hivyo uhai wa raia wasio na hatia unaondolewa na hata wale wanaowajibika kuwalinda hawatoi majibu ya kuridhisha juu ya mwenendo huu wa ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na baadhi ya watu katika jamii.

Septemba mwaka nchi iliingia kwenye taharuki, baada ya watu wasiojulikana kumshambulia kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu akiwa kwenye makazi yake mjini Dodoma. Kwa sasa anaendelea na matibabu nchini Kenya.

Kushambuliwa kwa Lisu kulitokea wiki mbili baada ya kubainisha sababu za kucheleweshwa kufika nchini kwa ndege aina ya Bombardier Q400-Dash 8 iliyonunuliwa na serikali ambapo alisema ndege hiyo imezuiliwa Canada kwa amri ya mahakama mpaka serikali ya Tanzania ilipe deni la sh. Bilioni 87 inalodaiwa na kampuni ya ujenzi ya Sterling Civil Engineering Ltd ya nchini Canada.

Siku chache baadaye, Meja Generali mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Vincent Mritaba alivamiwa na kupigwa risasi na majambazi wakati akiingia nyumbani kwake, Tegeta Dar es Salaam. Matukio ya watu kupigwa risasi yameendelea kushuhudiwa maeneo mbalimbali nchini huku baadhi yakihusishwa na masuala ya kisiasa.

 Kwa mujibu wa ripoti ya Kituo cha sheria na  haki za binadamu (LHRC) ya mwaka 2012 inaonyesha kuwa  mauaji ya raia wasio na hatia yanaongezeka kila mwaka ambapo katika kipindi kifupi cha kuanzia Januari mwaka 2012 watu waliouwawa kwa kupigwa risasi walikuwa 22.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa mwaka 2007 waliopigwa risasi bila hatia walikuwa 14 na mwaka uliofuata wa 2008 walikuwa 8. Idadi hiyo ilipungua kutokana na watetezi wa haki za binadamu kupaza sauti na kuzitaka mamlaka husika kulinda uhai wa raia wake. 

Hatua stahiki za kuwalinda raia zisipochukuliwa, uwezekano wa raia wasio na hatia kuuwawa katika mazingira ya kutatanisha ni mkubwa, wakati ambao misingi ya demokrasia inatikiswa ikiwemo kuminywa kwa uhuru wa kujieleza, vyombo vya habari na haki ya kukusanyika.

Kutokana na kuminywa kwa haki za msingi za binadamu, tunashuhudia mivutano ya viongozi wa serikali na vyama vya kisiasa ikiendelea na kutishia amani ya nchi yetu ambayo imedumu kwa muda mrefu sasa.

Tunakaribia kumaliza mwaka ni muhimu kama nchi tujitathmini juu ya utekelezaji wa haki ya kuishi ikizingatiwa kuwa tumeridhia mikataba ya kimataifa kulinda na  kuheshimu haki za raia.

Jukumu la kulinda haki za binadamu ni la watu wote katika jamii bila kujali tofauti za kidini na kikabila watu walizonazo. Taifa likishindwa kulinda haki ya kuishi, jumuiya za kimataifa hazitashindwa kutetea na kulinda haki za binadamu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *