Wagiriki wana tafsiri yao demokrasia kama ‘uongozi wa watu’. Na tafsiri ya kisasa inaelezeaza demokrasia zinasema ni mfumo wa serikali unaoongozwa na watu moja kwa moja ama kwa kutumia wawakilishi wanaotokana na wao wenyewe.
Tunashuhudia ubinafsishaji wa demokrasia katika bara la Afrika na hasa ukanda wa Afrika Mashariki. Wananchi wamekuwa mihuri ya watawala katika kupitisha maamuzi yao ili kutoa uhalali wa ubinafsishaji huu.
Tumeshuhudia Burundi, nchi mwanachama wa Afrika Mashariki ikitumia wananchi kuhalalisha ukomo wa uongozi kwa kupiga kura kubadilisha katiba kutoka miaka 5 hadi miaka 7 kwa muhula mmoja.
Hili limetokea baada ya Uganda nao kubadilisha katiba yao mwaka 2017 kuondoa ukomo wa umri kwa Rais wa kugombea wa miaka 75. Lakini kabla ya hapo mwaka 2005, mabadiliko ya katiba yalifanyika na kuondoa ukomo wa mihula ya uongozi yakimruhusu rais Yoweri Museveni kuendelea kugombea.
Mabadiliko mengine ya katiba yalifanyika Rwanda ambapo wananchi walipiga kura mwaka 2017 kumruhusu rais Paul Kagame kuhudumu mihula mingine miwili kila muhula ukiwa na miaka 7.
Sudan ya Kusini nako mambo sio shwari, kwani walipaswa kuwa na uchaguzi mwaka 2015 ambapo ungekuwa uchaguzi wao wa kwanza tangu kupata uhuru ila haukufanyika kutokana na mgogoro unaondelea. Bunge la nchi yao likafanya mabadiliko kwenye katiba yao ya mpito ya mwaka 2011 ili kuongeza muda wa uchaguzi mpaka mwaka 2018 mwezi wa saba.
Nchi wanachama pekee ambao ni Tanzania na Kenya bado zimekuwa imara zikiheshimu katiba zao na kuzingatia mihula ya uongozi. Ni jambo zuri kuona nchi hizi mbili bado ziko imara, lakini ni jambo la kuwa waangalifu kwani nchi hizi zinaweza kutumbukia katika mkumbo wa nchi zingine wanachama na kubadili katiba zao.
Hivi karibuni minong’ono ilianza nchini Tanzania kutoka kwa baadhi ya watu na wabunge waliotaka mabadiliko ya katiba yatakayoruhusu Rais kuhudumu kwa muda mrefu zaidi. Ila Rais John Magufuli alizima mjadala huo na kusema wazi hana nia ya kufanya hivyo kwani anaheshimu katiba ya nchi na hawezi kuivunja.
Niwakumbushe kuwa Tanzania sio mara ya kwanza kuwa na minong’ono ya kuongeza muda wa Rais kusalia madarakani. Katika kitabu cha Mwalimu Nyerere kijulikanacho kama “Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania” Mwalimu alieleza wazi ya kuwa kulikuwa na minong’ono kutoka kwa watu na wabunge ambao walitaka Rais Ali Hassan Mwinyi asalie madarakani kwa muhula mmoja zaidi. Mwalimu alikiri wazi kuwa alihuzunishwa na jambo hilo kisha alimwendea Rais Mwinyi ili aweze kufunga mjadala huo ili kuweza kuheshimu matakwa ya katiba.
Kwa nchi ambazo zimefanikiwa kuongeza ukomo wa uongozi wamefanya hivyo kwa kisingizio cha maslahi ya kisiasa ya baadhi ya watu ambao wana uchu wa madaraka. Ukweli unabaki kuwa, wananchi wanatumika kupitisha ajenda za viongozi ambao wameamua kubinafsisha demokrasia kwa matakwa yao binafsi.
Ubinafsishaji huu wa demokrasia unadhihirisha maovu yake kwa kuongezeka kwa migogoro, ukosefu wa amani na uvunjifu wa haki za binadamu katika nchi zilizowageuka wananchi wao na kuishia kujinufaisha wao wenyewe.
Kwa kuzingatia ubinafsishaji huu wa demokrasia Afrika, baraza la Umoja wa Afrika liliazimia mwaka 2007, kuwa na Mkataba wa Afrika juu ya Demokrasia, Uchaguzi na Utawala kama unavyojulikana kwa kiingereza “The African Charter on Democracy, Elections and Governance”.
Mkataba huu unajumuisha jumla ya wananchama 54 wa Umoja wa Afrika ambao ulianza rasmi Februari 15, 2012. Kati ya wanachama hao 54, waliotia sahihi na Kuridhia mkataba huo ni wanachama 10 tu ikiwamo Rwanda kwa Afrika Mashariki.
Wanachama waliotia sahihi bila kuridhia ni 28 ikiwamo Kenya, Uganda na Burundi kwa Afrika Mashariki. Wanachama ambao hawajatia sahihi wala kuurudhia ni 16 ikiwamo Tanzania.
Mkataba huo umekuja kama suluhisho la miaka mingi la utawala mbovu hususani chaguzi zisizo huru na haki, uvunjifu wa haki za binadamu, ushiriki hafifu wa wananchi katika serikali zao, na mabadiliko ya serikali bila kufuata katiba.
Mkataba huo unalenga kuimarisha ahadi na utayari wa nchi wananchama wa Umoja wa Afrika unaotaka kuwe na thamani ya demokrasia, heshima kwa haki za binadamu, uongozi wa sheria, ukuu wa katiba na mfumo thabiti wa katiba katika mipangilio ya dola.
Haya yote yamelenga kuwapa nguvu nchi wanachama kuweza kuwa walezi kwa wengine endapo makubaliano haya yatavunjwa. Ila mpaka sasa ubinafsishaji wa demokrasia unaendelea licha ya mkataba huo kupitishwa mwaka 2012.
Nitoe rai kwa Waafrika wenzangu tupaze sauti kwa nchi zetu kutia sahihi na kuridhia mkataba huu ili tuweze kuimarisha demokrasia Afrika. Tukumbuke kuwa mkataba huu umetokana na sisi waafrika wenyenye sio ile aina ya mikataba ambayo inatokana na misukumo ya nchi za Magharibi ambayo mara nyingi inakuwa na ajenda binafsi.
Kwa kuhitimisha, Afrika ni yetu sote na sisi wananchi tuna jukumu la kuhakikisha tunaimarisha demokrasia yetu wenyewe kwa kuzingatia matakwa yetu kwa kuwakumbusha viongozi wetu kwamba tumewapa madaraka ya kusimamia hoja zetu na sio matakwa yao binafsi.
Tatizo la Afrika viongozi wetu wanalewa na madaraka sana na wanakuwa wepesi kutumia mabavu kwa kutegemea jeshi linalinda uozo wao na pia wanapenda kutumiwa na nchi za magharibi kwa kujichumia pesa, yote hii ni tamaa…kwa asilimia kubwa waafrika wameamka yatizo pakusemea hakuna kwasababu ya udikteta wa viongozi ambao hawataki kushaurika.