HALMASHAURI ya Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza, imekumbwa na kashfa ufisadi wa matumizi mabaya ya fedha za miradi ya maendeleo, ambapo inadaiwa kutafuna zaidi ya sh. milioni 335.518; Imeelezwa.
Taarifa za kiuchunguzi zinaeleza kwamba, halmashauri hiyo ya wilaya ya Misungwi iliyopo chini ya Mkurugenzi wake, Xavier Tilweselekwa, tangu mwaka wa fedha 2008 hadi 2011 ilipokea jumla ya sh. 469,372,859 zilizotolewa na Serikali Kuu kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Taarifa hizo zinadai kwamba, fedha hizo zililetwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo kupitia Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM), ambapo miradi minane peke yake kati ya 10 ndiyo iliyotekelezwa.
Ripoti ya Ukaguzi wa Ndani za halmashauri hiyo imeitaja miradi iliyotekelezwa na fedha zake za MMAM kwenye mabano kuwa ni Hospitaliya Misungwi (sh. 44,144,199), Kituo cha afya cha Koromije (sh.19,613,350), Zahanati ya Mwamazengo (sh.25,762,154), ambapo jumla yake ni sh. 133,853,920.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Ukaguzi wa Ndani, miradi ambayo haikutelezwa na fedha zake kwenye mabano ni Zahanati ya Mwamboku (sh.47,979,514), Zahanati Ibongoya (sh. 20,804,000), Nyabumanda (sh.2,266,849), Hospitali ya Misungwi (sh. 86,133,260), Zahanati ya Nyamjundu (sh. 35,000,0000).
Miradi mingine ya MMAM ambayo haikutekelezwa licha ya kuwepo kwa fedha zake ni pamoja na Zahanati ya Ntulya (sh. 11,550,000), Zahanati ya Mwaniko (sh. 30,000,000), Zahanati ya Isesa (sh. 30,000,000), Zahanati ya Lubili (sh. 15,622,400), na mradi wa Zahanati ya Nyamainza sh.13,174,340, ambapo jumla yake ni sh. 335,518,939.
“Fedha hizo hazikutumika na ukamilifu wake una mashaka makubwa”, inaeleza ripoti maalumu ya ukaguzi.
Mbali na hayo, kashfa nyingine inadaiwa halmashauri hiyo ‘kuchakachua’ fedha za ukarabati wa Zahanati ya Koromije, baada ya kuelezwa kwamba Kituo hicho kilichotakiwa kununuliwa vifaa vipya kwa ajili ya ukarabati wake, kimewekewa vifaa kuukuu.
Kwa mujibu wa taarifa ya ukaguzi wa ndani, kati ya sh. 469,372,859 zilizotolewa na Serikali kuanzia mwaka wa fedha 2008/2009, 2009/2010, na 2010/2011 kwa ajili ya miradi ya MMAM wilayani Misungwi, sh.335,518,939 hazionekani na hazina maelezo ya kutosha.
Ripoti hiyo ya ukaguzi inaonesha kwamba, kiasi kilichotumika kutekeleza miradi ni sh. 133,853,920 peke yake, zikiwemo sh.19,613,350 zilizokarabati Zahanati ya Koromije.
Habari zilizopatikana kutoka Hospitali ya wilaya hiyo ya Misungwi (Mitindo), ambazo Mkurugenzi wa halmashauri, Xavier Tilweselekwa hakuzikanusha, zimesema madirisha yaliyojengewa Koromije, yaling’olewa katika Hospitali ya Mitindo.
Habari hizo zimedai kuwa, hata bati zilizoezekwa katika kituo cha Koromije ni zile zilizoezuliwa Mitindo, baada kukarabatiwa mwaka jana licha ya kiasi cha fedha zilizotolewa Koromije kujumuisha gharama za vifaa hivyo kununuliwa vipya.
Hata hivyo katika jitihada za kile kinachodaiwa kuzima tuhuma hizo nzito, halmashauri hiyo juzi inadaiwa kupeleka waandishi wa habari watano, kwa kile kilichoitwa ‘kutembelea miradi ya maendeleo’, inayodaiwa fedha zake kutafunwa.
Wakati wa ziara hiyo ya waandishi wa habari kutoka baadhi ya magazeti, na televisheni mbili timu hiyo ya wanahabari ilijionea wagonjwa katika Kituo cha Afya Koromije wakitumia shuka za kutoa majumbani mwao, huku mpya zikiwa zimefungiwa kabatini.
Waandishi walioshuhudia hali hiyo waliambiwa na wauguzi wa kituo hicho kwamba, mashuka hayo yamefungiwa yasitumike kutokana na kukosa pesa za kuyafulia licha ya wananchi kuchangia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Timu hiyo ya waandishi iliyoambatana na Mwenyekiti wa halmashsurihiyo, Bernard Polycarp, Mkurugenzi, Xavier Tilweselekwa na wataalamuwengine, walidai kushuhudia pia vitanda saba peke yake.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo ya Misungwi, Tilweselekwa, alipopigiwa simu na mwandishi wa habari hizi leo asubuhi kutaka kutoa ufafanuzi wa tuhuma hizo nzito za ufisadi, alidai yupo kwenye semina hawezi kuzungumza lolote.
Baadaye mwandishi wa habari hizi alimtumia ujumbe mfupi wa maandishi (SMS), ukisema kwamba: “Naomba kujua kuna taarifa ya fedha za MMAM Sh. 335,518,939 zinadaiwa kuliwa katika halmashauri yako. Fedha hizi zinadaiwa zilikuwa za kutekeleza miradi ya afya kuanzia mwaka wa fedha 2008 hadi 2011, je taarifa hizi zinaukweli ndani yake?.
DED akajibu kwa SMS: “Huu ni uzushi tu, Wilaya kama ya Misungwi kula mil 335,518939 maana yake hakuna chochote kitakachokuwa kimefanyika. Wakati kuna miradi mingi imetekelezwa kwa kukarabatiwa na inatumika”.
Mwandishi akamuuliza tena kwa SMS: “Ok, lakini DED taarifa za ukaguzi zinadai mamilioni hayo ya MMAM hayajulikani yalipo. Ina maana ripoti hiyo ni taarifa ya uzushi?”.
DED akajibu naye kwa SMS: “Ofisi yangu, ofisi ya mwenyekiti wa halmashauri haijawahi kupokea ‘mgt letter’ toka kwa waliotuma ‘kaguzi maalumu’ zilizofanyika ili kutoa majibu ya hoja zozote ambazo waliziona wakati wa ukaguzi.
“Kwa hiyo mie sijui lolote nitashukuru ukinipa taarifa hiyo pengine kama unayo inaweza kunipa mwanga”. Alisema Mkurugenzi huyo wa halmashauri ya wilaya ya Misungwi.
Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza
WIZI MTUPU