Ufisadi wakwamisha ununuzi kahawa Mbeya

Jamii Africa

UAMUZI wa Serikali wa kuizuia kampuni ya Lima Ltd kununua kahawa mkoani Mbeya umetajwa kuwa ni mbinu chafu zinazofanywa na watendaji wa serikali za wilaya na mkoa wakishirikiana na baadhi ya wafanyabiashara, hali inayokwamisha maendeleo ya wakulima wa zao hilo mkoani humo.

Wakulima wa kahawa mkoani humo wamesema watendaji wa wilaya na mkoa wanaizuia kampuni hiyo kununua kahawa ili kuwaruhusu walanguzi ambao wanawapunja kwa maslahi ya viongozi hao.

“Sisi wakulima tunakombolewa kwa kuuza kahawa yetu kwa bei nzuri kupitia Lima na siyo kutoka kwa walanguzi ambao wamekuwa wakitunyonya kwa kununua kahawa kwa bei ndogo,” anasema Bi. Tuntufye Mwakipesile.

Wakulima hao wameonekana kukerwa na msimamo wa serikali ulioonyeshwa Januari 16, mwaka huu wakati wa kikao cha Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, viongozi wa mkoa, wilaya pamoja na wafanyabiashara kilichofanyika mjini Vwawa, Mbozi.

Katika kikao hicho, ambacho baadhi ya watendaji wa serikali na Chama cha Mapinduzi walimshambulia Waziri wa Kilimo Prof. Jumanne Maghembe na kuhoji uwezo wake, waziri huyo alikubaliana na uamuzi wa viongozi hao wa wilaya pamoja na mkoa wa kuendelea kuizuia kampuni ya Lima kununua kahawa mbivu (cherry).

“Naunga mkono uamuzi wa uliotolewa na uongozi wa mkoa na wilaya wa kutoruhusu kampuni ya Lima kununua kahawa mbivu (Cherry). Katika msimamo wangu, viongozi wa mkoa na wilaya wanapaswa kusimamia bei nzuri kwa mkulima badala ya kuishia kupiga marufuku uuzaji na ununuzi wa kahawa hiyo,” alikaririwa akisema.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Bi. Tuntufye, kampuni ya Lima ndiyo inayonunua kahawa kwa bei nzuri zaidi kuliko walanguzi ambao wanapigiwa debe na watendaji wa wilaya na mkoa, ambao wanatajwa kwamba wana maslahi binafsi ya kutetea walanguzi.

Awali, Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa, Adolph Kumburu alisema kanuni za Wizara ya Kilimo zinaruhusu kununua kahawa mbivu kwa ajili ya kutafuta ubora wa zao hilo katika soko la kimataifa.

Alisema kwamba mkulima anaruhusiwa kuuza kahawa mbivu kwa mujibu wa kanuni hizo na Sheria namba 23 ya mwaka 2003 ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2011 inaruhusu ununuzi wa kahawa hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Kandoro naye anasema uamuzi wa mkoa huo  katika vikao vyake vilivyoketi mwaka jana, wa kutoruhusu kampuni hiyo kununua kahawa, hautatenguliwa.

Kwa upande wao, Mabwana Shamba wastaafu 49 waliokutana Januari 20, mwaka huu mjini Mbeya, wamesema watendaji wa serikali za wilaya mkoani humo wanafanya hila kuinyang’anya haki kampuni ya Lima isinunue kahawa, kwa lengo la kuwapatia fursa walanguzi wanaowapunja wakulima.

“Wafanyabiashara wengi wanaokingiwa kifua na watendaji wa serikali, kwa maana ya baadhi ya wakuu wa wilaya na wakurugenzi, wanatupunja kahawa yetu kuliko tunavyouza katika kampuni ya Lima Ltd, ambayo mbali ya kutupatia bei nzuri, lakini pia inatupatia pembejeo,” alisema Ambindwile Mwakangale (71) kutoka wilayani Rungwe.

Kikao cha maofisa hao wastaafu kilifanyika takribani siku nne tangu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushiriki, Profesa Jumanne Maghembe akutane na wafanyabiashara na watendaji wa wilaya za Mbozi, Ileje, Rungwe na Mbeya Vijijini mjini Vwawa wiki iliyopita.

Maofisa hao wa ugani wastaafu wamewalaumu wakuu wa wilaya na wakurugenzi kwa kumkashfu Waziri wa Kilimo kwamba ameshindwa kusimamia zoezi la ununuzi wa kahawa.

“Tunafahamu kwamba miongoni mwa wakurugenzi hawa na wakuu wa wilaya wanafanya biashara ya kununua kahawa kwa kuwatumia jamaa zao. Hatuko tayari kuuza kahawa yetu kwao, tumechoka kupunjwa,” alisema Gwakisa Kibona, kutoka wilayani Ileje.

Hata hivyo, maofisa hao wamemwandikia barua Rais Jakaya Kikwete kumweleza kuhusu njama zinazofanywa na watendaji wa serikali katika wilaya hizo ili kuikwamisha kampuni ya Lima Ltd isinunue kahawa kutoka kwa wakulima.

Barua hiyo iliyoandikwa Januari 20, 2012, inaeleza kwamba, mbinu hizo chafu za watendaji siyo tu zinakwamisha maendeleo binafsi ya wakulima, lakini pia zinakwamisha uchumi kwani mpaka sasa kahawa ya wakulima haijanunuliwa huku wakiwa hawana uwezo wa kupata pembejeo za kilimo.

Wiki iliyopita, wakulima wa kahawa walimzuia kwa dakika 10 Waziri Maghembe asiingie ukumbini mjini Vwawa kuzungumza na wafanyabiashara wakimtaka kwanza azungumze na wao, hali iliyofanya Mkuu wa Mkoa Abbas Kandoro kuingilia kati na kuteua wawakilishi 10 wa wakulima kuhudhuria kikao hicho.

Meneja wa Kampuni ya Lima Ltd tawi la Rungwe, Ephraim Kasanga, amesema kwamba kampuni yake iliomba kibali tangu Oktoba 2011 cha kusafisha kahawa waliyoinunua, lakini mpaka sasa ofisi ya mkuu wa Wilaya ya Rungwe haijawajibu.

“Tumewakumbusha tena wiki iliyopita kwa barua, tukiwaeleza kwamba kadiri kahawa ile inavyochelewa kukobolewa ndivyo inavyozidi kupoteza ubora wake, lakini hatujapata jibu lolote,” alisema Kasanga.

Barua hiyo kwenda kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mazao Wilaya ya Rungwe ya Januari 19, 2012
, inaeleza kwamba kampuni hiyo ilinunua kilogramu 8,048 za kahawa wilayani humo mwaka jana, lakini tangu walivyoomba kibali Oktoba 27, 2011 mpaka sasa hawajajibiwa.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa maelezo kwamba tayari liko mikononi mwa waziri mwenye dhamana ya kilimo.

Habari hii imeandikwa na Daniel Mbega

1 Comment
  • Kahawa ni zao kuu la uchumi linaloliingizia Taifa fedha nyingi sana za kigeni.Kama lilivyo zao la pamba Kahawa imekuwa ikilimwa na wakulima wa mikoa ya Kilimanjaro , Arusha na ziwa magharibi nk chini ya usimamaizi wa vyama vya ushirika

    Vyama vya ushirika vinavyosimamia mazao haya ya biashara ni manufaa makubwa kwa wakulima kwasababu mbali na kununua mazao yao pia huwapatia mbegu na pembeeo kama madawa, mabomba ya kupulizia, magunia ya kuhifadhia kahawa au pamba nk

    Mbali na faida hizo za pembejeo pia hulipa malipo mara mbili au tatu kulingana na soko la dunia kwa maana hiyo mkulima akiuza hupewa fedha hapo kwa hapo na baadaye kahawa au pamba inapouzwa kwenye soko la dunia hupewa ile tofauiti baada ya kuondoa gharama za pembejeo

    Kutokana na faida hizo nawashauri wakulima wa Mbeya .Ruvuma na Iringa ambao zao la kahawa linastawi vizuri kuunda vyama vya ushirika ili waweze kunufaika na pato linalotokana na kahawa yao

    Kumbuka unapouza kahawa kwa mtu binafsi au kampuni binafsi matokeo yake unalipwa fedha mara moja

    Pia nawashauri wakulima kutokuuza kahawa ya maganda ni vizuri kuipikichua kahawa yako na kuianika vizuri na gharama yake inakuwa ni kubwa

    Hivyo sioni kama huu ni ufisadi bali elimu ya kuuza kahawa kutumia vyama vya ushirika ni budi kutolewa na ofisi za serikali za mitaa na wizara ya kilimo na ushirika
    Mungu ibariki Tanzania

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *