MAOFISA wa Uhamiaji wa Tanzania, wamewakamata vigogo wawili wa usafirishaji binadamu akiwamo Raia wa Afghanistan Jamaluddin AbdulKahar , ambaye amekuwa akitafutwa kwa muda mrefu.
Taarifa zilizothibitishwa na maofisa uchunguzi na ukaguzi wa Idara ya Uhamiaji Tanzania, zinaeleza kwamba wafanyabiashara hao wa binadamu, walikamatwa na maofisa wa idara hiyo mkoani Dar es Salaam wakiwa na watu wanaowasafirisha.
Biashara ya binadamu imepigwa marufuku duniani kote na kuwekewa sheria kali na mikataba ya kimataifa, lakini imekua ikishamiri katika siku za karibuni kutokana na hali mbaya ya uchumi katika nchi nyingi duniani.
Watuhumiwa wote ambai ni raia wa nchi mbalimbali za Asia, walikamatwa katika operesheni maalum inayoendeshwa na Idara ya Uhamiaji mkoa wa Dar es Salaam na watafikishwa mahakamani kwa kuendesha biashara haramu ya binadamu.
Mbali ya Jamaluddin ambaye ni raia wa Pakistan,uhamiaji wamemkamata Ashok Kumar Khadraka, ambaye naye ni kigogo wa biashara haramu ya binadamu.
Miongoni mwa waliokamatwa pia wamo raia wa nchi mbalimbali waliokutwa wakiishi nchini kinyume sheria wakiwamo raia wa Kenya, China, Pakistan, India,Nepal na Bangladesh.
Mkenya Abdul Aden yeye alikamatwa na maofisa wa uhamiaji mkoa wa Dar es salaam kwa kosa la kutaka kujipatia pasipoti ya Tanzania ilihali yeye si raia wa Tanzania, akisaidiwa na Omar Mussa Omar raia wa Tanzania mkaazi wa temeke.
Uhamiaji Tanzania yakamata vigogo wa biashara haramu ya binadamu
1 Comment
bado biashara hii haieleweki vizuri. Kwa wengi wanaaomini katika bahati na kufanikiwa kwao kusafirishwa kwa kile tunachokiita biashara haramu wanatushangaa! natoka kijijini nije mjini kutafuta maisha! natoka mjini niende ulaya kuafanikiwa kimaisha! na mafanikio hayaangalii nimeyapataje! NI VYEMA HABARI ZINAZOHUSU WAATHIRIKA WA BIASHARA HII ZINGEONGEZWA ZAIDI KWENYE MACHAPISHO ILI KUIFANYA JAMII IELEWE TUNAPAMBANA NA NINI HASA.