Ukosefu wa huduma za dharura za uzazi washamirisha vifo vya wajawazito Ilemela

Jamii Africa

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amezitaka halmashauri zote nchini kuboresha huduma za dharura za uzazi katika vituo vya afya ili kupunguza vifo vya wajawazito na watoto.

Akizungumza katika ziara ya kukagua utoaji wa huduma za afya katika kituo cha afya cha Karume kilichopo kata ya Igombe wilaya Ilemela, amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zenye vifo vingi vya wajawazito na watoto wachanga ambapo sababu kubwa ni ukosefu wa  huduma za dharura za uzazi katika vituo vya afya.

“Leo hii toka saa sita usiku tuanze siku hadi saa sita usiku wanawake 30 wa kitanzania wanafariki kwasababu tu ya kutimiza wajibu wao wa kuleta kiumbe duniani”, amesema waziri Ummy.

Takwimu za serikali ya Tanzania za mwaka 2016 zinaonyesha kuwa vifo vya mama wajawazito ni 556 kila mwaka kati ya vizazi hai 100,000. Miongoni mwa watoto wachanga ni vifo 25 kati ya watoto 1000.

Amebainisha kuwa halmashauri zote nchini zinatakiwa kuweka kipaumbele katika ujenzi wa miundombinu ya huduma za dharura za uzazi ikiwemo vyumba vya upasuaji, maabara, wodi za wazazi na nyumba za watumishi ili kuhakikisha afya ya mama na mtoto inakuwa ya uhakika wakati wote.

Ameongeza kuwa wakurugenzi wa halmashauri hizo wahakikishe fedha zinazoelekezwa kwenye huduma za dharura zitumike kama zilivyopangwa, “kama fedha zitabaki unaweza kufikiri kujenga vitu vingine, kuliko kwenda kutumika kwa masuala mengine kama baadhi ya sehemu nyingine wanavyofanya”.

Kituo cha afya cha Karume  kwa muda mrefu kilikuwa hakina huduma ya dharura ya uzazi ambapo serikali ilitoa milioni 500 ili kuboresha miundombinu ya afya ikiwemo ujenzi wa chumba cha upasuaji, maabara ya damu na wodi ya akina mama.

Kwa wakazi wa maeneo yanayozunguka kituo hicho hasa wajawazito ni mkombozi ikizingatiwa kuwa kabla ya maboresho hayo walikuwa wanatembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika hospitali ya Wilaya ya Ilemela.

Kutokana na matumizi mazuri ya fedha katika wilaya ya Ilemela, serikali imeahidi kuboresha huduma ya dharura katika kituo kingine cha afya cha Buzurugwa katika wilaya hiyo ili kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga.

Jengo la Maabara lililojengwa kwenye kituo cha afya cha Karume katika mpango wa Serikali wa kuboresha huduma za dharura za uzazi kwenye vituo vya afya nchini

 

Vifo vitokanavyo na uzazi Afrika Mashariki

Miaka 28 iliyopita Tanzania ilikuwa inashika nafasi ya 18 barani Afrika katika orodha ya nchi 20 zilizokuwa zikiongoza kwa idadi kubwa ya vifo vitokanavyo na uzazi.

 Tanzania imejitahidi kupunguza idadi hiyo kwa takriban theluthi mbili kutoka vifo 997 mwaka 1990 hadi 398 mwaka 2015 kati ya vizazi hai 100,000, japokuwa inaendelea kushika nafasi ya tatu kwa Afrika Mashariki.

Hata hivyo, idadi ya vifo hivyo iliongezeka hadi kufikia 556 kati ya vizazi hai 100,00 mwaka 2016 kwasababu ya kupungua kwa uwekezaji wa huduma za mama na mtoto.

Inaelezwa kuwa Kenya, ambayo ilikuwa ikiongoza kwa kuwa na idadi ndogo ya vifo (vifo 687 kati ya vizazi hai 100,000), hivi sasa inashika nafasi ya nne kwenye kanda hiyo ambapo sasa inarekodi vifo 510 kati ya vizazi hai 100,000.

Ingawa mafanikio hayo hayawezi kulinganishwa na Rwanda, inayoongoza kwa idadi ndogo ya vifo 290 kutoka vifo 1,300 mwaka 1990, lakini walau yanatia moyo kwamba kuna jitihada kubwa zilizofanyika kuhakikisha usalama wa afya ya wajawazito na watoto wanaozaliwa.

Licha ya takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) kuonyesha matumaini hayo, lakini bado kuna changamoto ya kutokomeza vifo hivyo walau kufikia kwenye tarakimu mbili kama siyo tarakimu moja kama ilivyo kwa Libya.

Libya ndiyo nchi pekee barani Afrika ambayo kwa kiasi kikubwa imeweza kufikia kwenye tarakimu moja ya vifo kwa kurekodi vifo 9 tu kati ya vizazi hai 100,000 mwaka 2015 kutoka vifo 39 mwaka 1990.

Kufikia tarakimu mbili kama ilivyo kwa Misri, Cape Verde, Mauritius na Tunisia ni changamoto, lakini inawezekana ikiwa Serikali itatenga bajeti ya kutosha katika sekta ya afya na kuboresha huduma kuanzia ngazi ya msingi hadi rufaa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *