Ukosefu wa taarifa sahihi za viwango na aina ya samaki wakwamisha ujenzi wa viwanda nchini

Jamii Africa

Tanzania itaanza kufaidika na rasilimali za bahari baada ya kuanza kutekeleza Programu ya Udhibiti na Matumizi Endelevu wa Rasilimali Samaki (EAF-Nansen) kudhibiti mabadiliko ya tabia na uchafuzi wa mazingira yanavyoathiri uzalishaji wa mazingira ya bahari na afya.

Programu ya EAF-Nansen inayofadhiliwa na Norway na kutekelezwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Mambo ya Bahari ya Norway (IMR) itasaidia kutunza mazingira na mifumo ya ikolojia kwa upande mmoja na kutatua mahitaji ya binadamu ya chakula na faida za kiuchumi.

Programu hiyo imekuja siku chache baada ya meli ya kisasa ya utafiti wa samaki na mazingira baharini yenye jina la Dkt. Fridtjof Nansen kukamilisha uchunguzi wake wa rasilimali na mazingira bahari katika maji ya Bahari ya Hindi nchini Tanzania.

Meli hiyo imebaini kuwa Tanzania ina uhaba wa taarifa sahihi za viwango na aina ya samaki, hali inayokwamisha ujenzi wa viwanda vya kusindika samaki nchini.

Chini ya Mpango wa Programu ya EAF-Nansen, meli hiyo inaendesha utafiti wake wa rasilimali bahari na mazingira baharini katika ukanda wa Kusini Mashariki mwa Afrika na Bahari ya Hindi. Nchi thelathini za Kiafrika ikiwemo Tanzania zitapata msaada wa kitaalamu na kisayansi wa namna ya kudhibiti rasilimali zao za samaki na viumbe bahari wengine kwa kutumia na kutekeleza mpango endelevu wa utunzaji wa mazingira.

Akizungumza katika hafla fupi ya kilele cha utafiti huo iliyofanyika ndani ya meli iliyotia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam, Katibu mkuu kiongozi, Balozi John Kijazi amesema mpango huo umekuja kwa wakati muafaka kwani utachochea kasi ya uanzishwaji wa viwanda hapa nchini hususani katika sekta ya uvuvi.

Hii ni hatua kubwa sana kwa Tanzania ambayo itafaidika na huduma za utafiti wa kisasa wa meli hii kupitia ushirikiano wa wadau hapa nikizungumzia FAO na Serikali ya Norway, kuweza kujua kwa uhakika aina na kiwango cha samaki na rasilimali bahari nyingine tulizonazo katika maji yetu,” amesema Balozi Kijazi.

Amesema taarifa kuhusu rasilimali bahari yetu ni muhimu sana katika kufanya maamuzi na kupata fursa za ndani na kimataifa za uwekezaji katika sekta ya uvuvi na kutilia maanani mambo muhimu ya utunzaji wa mazingira.

Kwa kutumia taarifa sahihi tunaweza kuwavutia wawekezaji kuja na kujenga viwanda vya kusindika samaki na vingine vinavyohusiana na sekta hii ya uvuvi na hivyo kuongeza kasi kwenye mpango wetu wa kujenga Tanzania ya viwanda,” amesema Balozi Kijazi.

Kwa upande wake,Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina amesema, mpango huo utaongeza ajira na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika sekta ya uvuvi. “Hii itatuwezesha kupata wawekezaji katika eneo hili ambao watajenga viwanda vya kuchakata na kusindika mazao ya samaki ambapo mbali ya kutoa fursa za ajira kwa watu wetu hususani vijana katika mnyororo wa thamani, lakini pia utakuza mapato ya Serikali.”

Wadau wa mazingira wanasema ikiwa mpango huo utatekelezwa kikamilifu unaweza kusaidia kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yameathiri uhai wa bahari na rasilimali zilizopo.

Mbali ya taarifa ambazo zitawezesha udhibiti bora wa rasilimali kwa matumizi endelevu, utafiti huu utapekelea uelewa mzuri wa athari za mabadiliko ya tabia nchi na athari nyingine za nje, kama vile uchafuzi wa mazingira na mifumo ya uhai baharini.,” amesema Mwakilishi wa FAO nchini Tanzania, Fred Kafeero.

Programu ya Udhibiti na Matumizi Endelevu wa Rasilimali Samaki (EAF) imekuwa ni moja ya marejeo makuu za FAO katika kusaidia nchi katika juhudi zao za kudhibiti na kutekeleza kanuni za maendeleo endelevu.

Kwa mujibu wa FAO, programu ya EAF ni njia ya kutekeleza kanuni sahihi za uvuvi kwa kutoa mwongozo wa namna ya kufikia malengo ya sera ya kiuchumi, kijamii na ikolojia kupitia malengo, viashiria na njia za tathimini. EAF inanuia kuweka uwiano kati ya mambo mawili muhimu; Utunzaji wa mazingira na mifumo ya ikolojia kwa upande mmoja na kuweza kutatua mahitaji ya binadamu ya chakula na faida za kiuchumi upande mwingine.

Uvuvi haramu bado ni changamoto

Utafiti uliotolewa hivi karibuni na Taasisi ya Overseas Development ya nchini Uingereza unaeleza tatizo la uvuvi haramu kwenye bahari kuu ikiwemo bahari ya Hindi kwamba unachochewa zaidi na ukosefu wa miundombinu ya mawasiliano, ushirikiano na teknolojia ya kutunza takwimu za meli za uvuvi kwenye bahari kuu ikiwemo bahari ya Hindi ambayo inaunganisha mataifa mbalimbali duniani.

Tatizo ni kubwa kwa nchi za Afrika ambazo hazina teknolojia ya kisasa na taasisi imara za kusimamia uvuvi ambapo kila mwaka nchi za Afrika Magharibi zinapoteza Dola bilioni 2 za kimarekani huku nchi zinazotumia bahari ya Afrika Mashariki (Kenya, Tanzania, Mauritius, the Comoros, Mozambique, and the Seychelles ) zinapoteza zaidi dola milioni 200 kila mwaka.

Licha ya kila nchi kuwa na taratibu zake katika kupambana na uvuvi haramu, hazijafanikiwa kumaliza tatizo hilo na changamoto inayojitokeza kwenye ukusanyaji wa takwimu na matumizi ya vifaa vya kusimamia mwenendo wa meli katika eneo la bahari kuu.

Utafiti huo unaeleza kuwa ili kufuatilia eneo na safari, meli zinapaswa kuwa na kifaa cha mawasiliano kijulikanacho, ‘Vessel Management Systems (VMS)’. Hata hivyo meli nyingi hazina kifaa hiki hasa katika nchi zinazoendelea ambako teknolojia hiyo haipatikani au wasimamizi wa meli huzima ili kuepuka kufuatiliwa na mamlaka husika.

Licha ya kifaa cha VMS kuwa na uwezo wa kutambua eneo, umbali na mwelekeo wa meli lakini hakiwezi kutambua meli zinazoharibu mazalia ya samaki na viumbe wengine wa baharini

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *