Upungufu wa dawa katika vituo vya afya waongezeka kwa asilimia 70

Jamii Africa

Tanzania ni miongoni mwa nchi za Kusini mwa jangwa la Sahara iliyopiga hatua kubwa katika uboreshaji wa sekta ya afya na kupunguza vifo vya wajawazito, watoto na vifo vinavyotokana na ugonjwa wa malaria na virusi vya UKIMWI.

Licha ya mafanikio hayo bado inakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya na hospitali.

Kulingana na Sera ya Afya (2007) katika kifungu cha 5.4.3 inatamka kuhakikisha kwamba dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi vinapatikana wakati wote, kwa kiasi cha kutosha na ubora unaotakiwa katika vituo vya afya.
Lakini hali halisi iliyopo katika vituo vya afya ni tofauti na sera inavyotamka.

Wananchi walioenda kutibiwa katika vituo mbalimbali nchini wamekiri kukumbana na upungufu wa dawa na wakati mwingine dawa muhimu hazipatikani katika maduka ya vituo hivyo.

Ripoti ya shirika la Twaweza (Agosti, 2017) iliyoangazia maoni ya wananchi kuhusu huduma za afya na ustawi wa jamii miezi mitatu iliyopita inathibitisha kuwa asilimia 70 ambayo ni sawa na wananchi 7 kati ya 10 walioenda kutibiwa katika vituo vya afya walikutana na upungufu wa dawa na vifaa tiba.

Upungufu huo wa dawa umeongezeka kwa asilimia 11 ikilinganishwa na mwaka 2016 ambapo ilikuwa ni 59%. Pia kulikuwa na ongezeko la asilimia 6 mwaka 2016 ikilinganishwa na asilimia 53 mwaka 2015.

Hali ya upatikanaji wa dawa 2017 inalingana kwa karibu na ile ya 2014 (62%) ambapo ni tofauti ya 8%. Hali hiyo ikashuka katika miaka miwili iliyofuata kabla ya kuongezeka kwa kasi na kufikia 70% mwaka huu.

Baadhi ya vituo vya afya havina dawa kabisa na wananchi huandikiwa wakanunue mahali pengine yakiwemo maduka binafsi. Na hata kwa vituo ambavyo dawa zipo lakini bado hazitoshelezi mahitaji ya wagonjwa wote kutokana na mfumo usioridhisha wa usambazaji wa dawa hizo.

Ripoti ya Sauti za Wananchi ya Twaweza ya mwaka 2013 inaeleza kuwa “karibu wagonjwa wote (97%) wanaofika katika vituo vya afya huandikiwa dawa au maelezo ya dawa ama kupewa vyote kwa pamoja. Hata hivyo wagonjwa wawili kati ya watano (41%) wanaripoti kutokufanikiwa kupata dawa walizoandikiwa”.

Licha ya wananchi kukutana na upungufu wa dawa lakini hutumia muda mrefu katika foleni kuzipata dawa hizo na huduma nyingine za matibabu.

Ripoti hiyo ya Twaweza inaeleza kuwa tatizo kubwa la pili lililojitokeza sana ni muda wa kusubiri, ambapo wananchi sita kati ya kumi (63%) walioenda kupata matibabu wanasema muda wa kusubiri ni mrefu sana.

Serikali inakiri kuwa kuna upungufu wa dawa katika vituo vya serikali kupitia Sera ya Afya ya mwaka 2007 katika kifungu cha 5.4.3, “Pamoja na jitihada za Serikali za kuhakikisha kwamba dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi vinapatikana, bado kuna upungufu na matatizo ya upatikanaji wake katika vituo vya kutolea huduma za afya na hivyo kuathiri utoaji wa huduma bora”.

Utafiti wa viashiria vya Utoaji wa Huduma wa mwaka 2010 unaonyesha kuwa robo (24%) ya dawa muhimu, kwa wastani, hazikuwepo kwenye vituo vya afya nchini kote.

Kwa upande wake serikali kwa nyakati tofauti imeelezea mipango yake ya kuboresha huduma za afya ikiwemo upatikanaji wa dawa kwa wakati.

Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa nchini (MSD), Laurean Bwanakunu anasema hali ya upatikanaji wa dawa imeimarika kwa asilimia 83 na serikali imetenga bilioni 250 kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 kwa ajili ya manunuzi ya dawa.

Kwa upande wake Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akisoma hutuba ya bajeti ya wizara bungeni amekiri kuwepo kwa changamoto za upatikanaji wa dawa ikiwemo baadhi ya Halmashauri/hospitali kutowasilisha mahitaji yao ya dawa kwa wakati na hivyo kusababisha tatizo la upatikanaji wa dawa katika vituo vyao.

“Kuna usimamizi hafifu wa matumizi ya dawa, makusanyo na matumizi ya fedha zinazotokana na uchangiaji wa huduma za afya na matumizi ya mifumo na utunzaji wa taarifa za dawa na vifaa tiba”

Anasema wanachukua hatua mbalimbali kukabiliana na upungufu wa dawa ikiwa ni pamoja na fedha za dawa kupitia Mfuko wa Pamoja wa Afya (Health Basket Fund) zitapelekwa moja kwa moja katika vituo vya kutolea huduma. Kwa mwaka huu wa fedha wametenga jumla ya shilingi bilioni 263 kwa ajili ya kukabiliana na tatizo hili la dawa na vifaa.

“Mikakati mizuri yenye motisha kwa watumishi (wahudumu wote wa afya kuanzia madaktari mpaka maafisa ununuzi) na mfumo wa uwazi na uwajibikaji wa manunuzi ya dawa na vifaa, vinahitajika kuhakikisha Tanzania yenye huduma bora za afya”. Inaeleza ripoti ya Twaweza.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *