USAID, Internews wazindua mradi wa ‘Boresha Habari’ kuimarisha uhuru wa kujieleza na kuhabarishwa

Jamii Africa

Shirika la Misaada la Marekani (USAID) kwa kushirikiana na Asasi za Kirai Tanzania wamezindua mradi wa Boresha Habari unaolenga kuwahusisha na kuwawezesha wanawake na vijana kupaza sauti zao kupitia vyombo vya habari ili kuongeza uwajibikaji na uwazi katika jamii.

Mradi  wa ‘Boresha Habari’ umezinduliwa leo jijini Dar es Salaam ambapo unatarajiwa kuanza kutekelezwa Machi mwaka huu na kukamilika kwake kutaongeza uhuru wa kujieleza, haki ya kupata habari na kuboresha utendaji wa vyombo vya habari na Asasi za Kiraia nchini.

Mradi  huo unaratibiwa na taasisi ya Internews kwa kushirikiana  na USAID pamoja na FHi360 ambapo taasisi za JamiiForums, Tanzania Bora Iniative,  Baraza la Habari Tanzania (MCT), Geopoll (Kenya) na International Center for Not-for-Profit Law (ICNL)  zitahusika kwenye utekelezaji .

 Internews ambayo ni taasisi ya Kimataifa yenye lengo kuu la kuvipa vyombo vya habari vya ndani duniani kote uwezo wa kuwapa watu taarifa na habari wanazohitaji, uwezo wa kuungana na namna ya kufanya sauti zao kusikika.

 Malengo ya Boresha Habari ni kuboresha mazingira yatakayowezesha vyombo vya habari kufanya kazi kwa uhuru ili kuifikishia jamii taarifa za kweli na uhakika ambazo zitawawezesha wanawake na vijana kusikika katika jamii. Waandishi wa habari pia watawezeshwa kutimiza majukumu ya kuhabarisha kwa kuzingatia taaluma na weledi.

Pia kuziwezesha Asasi za Kiraia kutumia vyombo vya habari kuwasiliana na kuiwakilisha jamii kwenye mambo ya msingi ya maendeleo ambapo radio za kijamii zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini zitahusishwa kutoa habari za kweli na uhakika.

 

Uhuru wa Vyombo Vya Habari nchini

Mwaka 2017, serikali iliyafungia magazeti kadhaa yakiwemo Raia Mwema, Tanzania Daima, MwanaHalisi kwa makosa mbalimbali ya uchochezi lakini kasi hiyo inawatisha wadau wa masuala ya habari duniani ikizingatiwa kuwa uhuru wa kujieleza ni haki ya msingi ambayo inapaswa kulindwa kwa gharama yoyote ili kujenga jamii iliyostaarabika.

Kulingana na Utafiti wa Twaweza (2016) unaeleza kuwa  “Uhuru wa kujieleza umekuwa ukikabiliwa na vitisho vikali ambapo polisi wamekamata watu 358 kwa mwaka 2015 na watu 911 mwaka 2016 kwa kosa la kutumia lugha mbaya”.

Hata hivyo, ili kusimamia maudhui na ukuaji wa tasnia ya habari nchini, sheria mbalimbali zimepitishwa ikiwemo; Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Huduma za Habari (2016) na Sheria ya Takwimu (2015). Lakini changamoto inajitokeza ni jinsi sheria hizo zinavyotekelezwa ambapo zinatajwa kuminya uhuru wa kujieleza.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *