Hujavuka miaka 30? Unashauriwa kusafiri sana na kuhifadhi fedha kadiri uwezavyo!

Jamii Africa

Kufikisha miaka 30 maishani yaweza kuwa kipindi cha mabadiliko makubwa kwenye maisha ya mtu na taaluma yake. Ni kipindi ambacho malengo ya wengi kitaaluma huanza kuwa wazi na shauku ya kufika sehemu fulani kimaendeleo huongezeka.

Yalifanyika mazungumzo na baadhi ya Maafisa Watendaji Wakuu wa makampuni mbalimbali kuhusu kipi wangependa wafanyakazi wao wawe wamefanya kabla ya kufikisha miaka 30. Haya ni baadhi ya maoni yao kuanzia kwenye suala la kutembelea sehemu mbalimbali, kuweka akiba ya fedha na hata kuanzisha biashara zao wenyewe:

Aaron Smith (Afisa Mtenda mkuu na mwanzilishi wa kampuni ya KX)

Kitu cha kwanza ninachopenda kuwashauri ni kutembelea sehemu mbalimbali duniani. Hakuna kitu kizuri kinachofungua macho kama kusafiri kwenda sehemu mbalimbali ili kupanua uelewa wako na kuboresha mbinu zako za mawasiliano kutoka kwa watu wengine wa tamaduni tofauti.

Uzoefu wa kidunia hauna gharama. Inakusaidia kufahamu mambo chanya kwenye ulimwengu halisi wa watu. Hadi kufikia umri wa miaka 25 nilikuwa nimeshatembelea nchi zaidi ya 40 na kuishi mbali na nyumbani kwa miaka 5. Kilikuwa kipindi kizuri sana.

Kuwa mbinafsi, jitoe kwa kila kitu na uishi maisha kadiri uwezavyo. Kabla ya kufikisha miaka 30 unakuwa huna majukumu makubwa na pengine huna hata familia ya kuitunza. Jitoe na tumia ulivyonavyo vyote ili upate maendeleo makubwa.

Wewe bado ni kijana mwenye nguvu nyingi, mwenye ushawishi na una muda mwingi wa kufanikiwa zaidi hata pale unaposhindwa unaweza kuanza tena na kufanikiwa maana huna cha kupoteza.

Aaron Smith katika moja ya semina zake

Kadiri umri unavyoongezeka ndivyo sababu za kutokufanya jambo fulani huongezeka na mwisho wa siku utakuja kujuta kwa kutokujaribu mapema. Nilipoteza akiba yangu yote ya fedha kwenye biashara nilipokuwa na umri wa miaka 18 na nikafanikiwa kwenye biashara ya pili nikiwa na umri wa miaka 26. Tambua kwamba utakosea huko mbele.

 

Taichi Hoshino (Afisa mtendaji wa Monetise).

Jenga tabia au maadili mazuri. Kuanzia kwenye matumizi mazuri ya muda, maadili ya kazi, kujiwekea mipaka ya kazi au maisha, mazoezi, kula vizuri au kuwa na nidhamu na fedha zako binafsi, maadili ndiyo msingi wako mkuu.

Pale unapokutana na mazingira yasiyotabirika kwenye maisha, maadili mazuri uliyojijengea kwa muda mrefu ndiyo yatakayokusaidia. Anza nayo mapema nayo yatakuwa nawe maisha yako yote.

Taichi Hoshino

 

Jo Burston (Mwanzilishi na Afisa mtendaji mkuu wa Inspiring Rare Birds).

Jifunze kukabiliana na kupanda na kushuka kimaisha. Watu wengi ninaokutana nao walio kwenye miaka ya 20 na kuendelea wako bize kuhangaika kuwasimamia wenzao wenye ujuzi mdogo, wakati ujuzi halisi ni kusimamia kutoka juu hadi kwa watu wenye ujuzi na uzoefu mkubwa. Ujuzi wa mazungumzo na kuzungumza mbele za watu utakupeleka kokote maishani.

Tambua kile unachokipenda na lenga kuwa bora duniani katika kile unachokifanya kupitia kuwa na kiu ya kujifunza zaidi kwa nadharia na kwa vitendo pia.

Tafuta mwalimu au mtu ambaye amewahi kupita kwenye njia unayotamani kuipita. Kuwa mbunifu, mwaminifu na heshimu muda unaoutumia pamoja naye. Anajifunza kutoka kwako pia.

Weka akiba ya kila pesa unayoipata. Jifunze kuweka akiba na utoke nyumbani kwenda kujitegemea mwenyewe. Hakuna mtu anayekudai hivyo achana na hisia kwamba kuna watu unawajibika kwao. Hilo sio jukumu lako.

Jitahidi uanzishe biashara hata kama ni ndogo. Utakapoweza kujifunza mbinu hizi mapema utajifunza namna ya kupata hasara kwa gharama ndogo. Msingi mzuri wa ujuzi wa biashara na fedha utakusaidia kufanikiwa baadaye.

Tembelea sehemu mbalimbali za ulimwengu itakusaidia kujikubali, kuwa na uvumilivu na kuwa jasiri na pia utaona jinsi dunia yetu ilivyo nzuri.

 

Dean Ramler (Mtendaji Mkuu na mwanzilishi mwenza wa Milan Direct)

Jifunze ubunifu wa kwenda mbali zaidi kwa kufanya zaidi ya kile unachotakiwa kufanya au zaidi ya kile unacholipwa kukifanya. Mfanyakazi wa kawaida hufanya kazi mpaka saa 11 jioni kwasababu huu ndiyo muda ambao muda wa kazi huisha. Kila mtu ana haki ya kufanya hivi.

Lakini kuna watu wachache wanaobaki nyuma kama mimi wenye malengo makubwa ambao wanafahamu thamani ya kwenda zaidi na kufanya zaidi ya kile wanacholipwa kukifanya na hawa mara nyingi huangalia namna ya kuzalisha zaidi kwa ajili ya kampuni.

Kama kiongozi mara nyingi utajikuta unawategemea wafanyakazi wachache wale ambao hufanya zaidi ya kile wanachotakiwa kukifanya, na huwa ni mazoea kuwaita hawa wachache kukusaidia kazi muhimu pale ambapo wengi wanakuwa wameshaondoka.

Na sio jambo la kushangaza kwamba hawa wachache mara nyingi ndiyo huja kuwa viongozi wa wenzao ndani ya kampuni, na ndiyo ambao hupandishwa vyeo na kuongezewa mishahara.

Dean Ramler

 

Philip Weinman ( Afisa Mtendaji Mkuu wa Locomote).

Anzisha biashara yako mwenyewe ukiwa bado unaishi nyumbani kwenu. Ni muda mzuri wa kujaribu mawazo mbalimbali ya kibiashara huku ukiwa huna gharama kubwa kimaisha. Tafuta mwalimu au mtu unayemuamini tofauti na ndugu yako ambaye atakushauri na asiwe na malengo ya kufaidika kifedha kutoka kwako.

Katika kipindi hiki utajifunza zaidi kupitia makosa unayoyafanya na pale itakapotokea ukafanya maamuzi ya kutoka nyumbani tayari utakuwa unajua kipi kinaleta faida na kipi hakileti faida. Pamoja na kupata uzoefu kwenye biashara, pia utajifunza kufanya maamuzi na kuyasimamia.

Philip Weinman

 

Christian Mischler (Afisa Mwendeshaji na mwanzilishi mwenza wa Hoteli ya Quickly).

Tembelea sehemu mbalimbali ulimwenguni! Tembelea maeneo mbalimbali na tamaduni tofauti, husaidia kukujengea hali ya kujitegemea na itakupa uzoefu wenye madhara chanya ambao ni wa muda mrefu maishani mwako mwote.

 

John Winning (Afisa Mtendaji Mkuu na mwanzilishi wa Winning Group).

Ongeza uzoefu kwa kadiri utakavyoweza – ni jambo la muhimu sana kuwa na uzoefu wa aina nyingi kwenye maisha na kwenye kazi pia. Jitahidi kufanya kazi sehemu mbalimbali ikiwemo viwandani au kwenye shule hata kama ni kazi za muda mfupi au za masaa machache. Mimi niliendesha magari ya mizigo, nilifanya kazi ya kusambaza bidhaa majumbani na pia kwenye maduka ya kuuza bidhaa.

Kuwa na uhakika wa kupata elimu zaidi itakayokuvutia. Sio lazima iwe kutoka chuoni lakini hata kwenye kusoma vitabu maana ni vizuri kuwa na shauku ya kujifunza zaidi, na shauku ni motisha nzuri. Sikwenda kusoma chuoni baada ya kumaliza shule lakini miaka iliyofuata ilitengeneza namna au jinsi ninavyofanya kazi na jinsi biashara yangu inavyokwenda.

Kutoka kwenye biashara ya rejareja, mpaka mafanikio binafsi hadi kupata tuzo ya dunia, kumeimarisha sana fikra zangu na uwezo wa kukabiliana na vikwazo na kukamata fursa nyingi kwenye biashara.

John Winning

 

Zach Johnson (Afisa Mtendaji Mkuu wa atmail.com).

Ishi maisha kwa kiwango kikubwa kwa kadiri unavyoweza na pokea kila uzoefu unaoupata pale unapokuja – Yote na kamili.

 Zach Johnson 

 

Charlie Wood (Meneja Mkuu wa Dropbox)

Nashauri watu wapate uzoefu wa miaka kadhaa kutoka kwenye makampuni makubwa hasa wakiwa kwenye kipindi cha miaka 20. Uzoefu ambao wataupata kutoka kwenye makampuni haya utawajenga katika kufanikiwa hapo baadaye.

Wale ambao ni wafanyabiashara kwa asili ni vizuri watimize ndoto zao na kuyaweka mawazo yao kwenye vitendo kwa kuanzisha biashara zao wenyewe au kwa kushirikiana na watu wachache.

Moja ya jambo muhimu ambalo mtu anatakiwa kulifanya kabla ya kufika miaka 30 ni kusafiri kwenye sehemu mbalimbali ulimwenguni, kukutana na watu tofauti na kutengeneza maisha mapya. Uzoefu huu utapanua uelewa wa mtu na kumsaidia kujipanga kwa ajili ya kipindi cha miaka 30.

 

Bevan Nel (Mkurugenzi Mtendaji wa Helping).

Kuwa na nidhamu katika matumizi yako ya fedha, weka bajeti na uifuate!

Pili, kama unataka kufanya biashara, jitahidi uifanye kabla hujaoa/kuolewa na kuwa na watoto na familia. Utakuwa muoga sana na hutakuwa na uthubutu wa kutosha pale tu utakapoanza kuwa na familia na maendeleo ni ya muhimu sana kuanzia mwanzo wa taaluma yako.

Mwisho kabisa, ni vizuri kuendeleza mawasiliano na wafanyabiashara au wateja wako wa zamani. Tunza mawasiliano yao, fanya vyovyote inavyowezekana ili kutunza mawasiliano yako siku zote. Mawasiliano ni muhimu maana hujui ni wakati gani utahitaji msaada kutoka kwa mtu fulani.

Kwa mtazamo usio wa kibiashara….safiri…safiri…safiri! Hiki ndicho ninachowaambia vijana. Kusafiri ni jambo zuri katika kukujengea ujasiri, kukutana na watu wa kufanya nao biashara na pia ni njia nzur ya kujiburudisha na kuamsha mwili na akili.

Bevan Nel

 

Kevin Lynch (Afisa Kiongozi wa Masoko wa Open Colleges).

1. Jifunze kutoka kwa wenzako: Kadiri tunavyozidi kukua katika taaluma zetu kwenye miaka 20 na kuendelea tunahitaji kujifunza sio tu kwa wale waliotuzidi, bali hata kutoka kwa wale tulionao kwenye ngazi moja. Hii itakuhakikishia ujenzi wa msingi imara kwa ajili ya miaka ya 30.

Najifunza sana kutoka kwa wenzangu, watu ambao wananizunguka. Hawa ndio watu wanaofanya mambo yanaenda, ni waerevu zaidi yangu. Watu wanaotuzunguka ndio wanaofanya tuwe tulivyo.

Tunajitahidi kuhakikisha kwamba tunaendeleza utamaduni uliopo na kuhakikisha panakuwa mahali salama kwa wafanyakazi wetu kutimiza majukumu yao, mahali ambapo watu wanaamini maono ya kampuni katika kubadilisha maisha ya watu kupitia elimu.

           Kevin Lynch

 

Nicholas Smedley (Mkurugenzi Mtendaji wa Steller).

Kwa kuwa tupo kwenye biashara ya kuuza na kupangisha nyumba, vyumba na viwanja nafikiri ni muhimu kwa wafanyakazi wetu kulielewa soko. Hakuna njia nzuri zaidi ya ile ya kuingia kwenye soko sahihi.

Ushauri ni anza kuweka akiba mapema kadiri unavyoweza – haijalishi kama ni kupitia hisa au kufanya uwekezaji wa aina nyingi. Hakuna kitu bora zaidi kuliko riba mchanganyiko. Hii itakuingiza kwenye uwanja wa ufahamu wa kuweka akiba na kukuwezesha kununua rasilimali yako ya kwanza kabla ya kufikisha miaka 30 ambao utakuwa ni mwanzo mzuri.

                 Nicholas Smedley

 

Levi Aron ( Meneja wa Yumtable).

Chukua muda tulivu kuweka malengo mapema kabla ya kuanza, yafuatilie na pambana kuyatimiza. Siku zote kumbuka kujipongeza kila unapofanikiwa kufikia hatua fulani. Ni vizuri kujipongeza wewe binafsi. Fanya kazi kwa bidii kukabiliana na vikwazo lakini usisahau kujipongeza na kupumzika kila inapowezekana.

Kumbuka, pasipo na malengo = hakuna jitihada = maisha ya kawaida/chini, Ni nani anataka maisha ya hivyo?

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *