Ushuru wa bidhaa: Kero ya Muungano iliyokosa ufumbuzi wa kudumu

Jamii Africa

Serikali ya Tanzania Bara na ile ya Zanzibar kukutana kujadili kuhusu namna bora ya kupata ufumbuzi wa kudumu wa kero ya ulipaji kodi ya mizigo kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara.

Hayo yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Wingwi, Juma Kombo Hamad (CUF) aliyetaka kujua kama Serikali ipo tayari kuunda Kamati Ndogo ya Bunge kwa ajili ya kushughulikia mfumo wa ulipaji kodi ya mizigo kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara.

Katika swali la msingi, Hamad ameeleza kuwa mfumo wa ulipaji kodi wa kusafirisha bidhaa kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara umekuwa ukilalamikiwa kwa muda mrefu kwamba unawakwaza na kuvunja harakati za ukuaji wa sekta ya biashara Zanzibar na hivyo kusababisha uchumi wa nchi hiyo kushuka.

Akijibu swali hilo Dk. Kijaji, amesema kuwa Serikali hizo mbili zinaendelea kujadiliana ili suala hilo lipatiwe ufumbuzi wa kudumu na kuongeza kuwa Serikali hizo hazijashindwa kutatua changamoto hiyo na hakuna sababu ya kuunda kamati ya kushughulikia suala hilo.

Amesema chimbuko la malalamiko hayo linatokana na kuwepo kwa mifumo tofauti ya kutathmini bidhaa kati ya Zanzibar na Tanzania Bara hali inayosababishwa na viwango tofauti vya ushuru wa forodha vinavyopaswa kulipwa kwa bidhaa ya aina moja kutoka nje ya nchi na kusafirishwa kwenda sehemu ya pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dk. Kijaji amesema kuwa Mfumo wa uthaminishaji wa bidhaa zote zinazoingia Tanzania Bara unafanyika kwa kutumia mifumo ya ‘TANCIS’ na ‘Import Export Commodity Database (IECD) inayoratibiwa na kituo cha Huduma za Forodha kilichopo Dar es Salaam, lakini Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitumii mifumo hiyo na kusababisha kuwepo na tofauti ya kodi kati ya Bara na Zanzibar.

Kutokana na utofauti wa mifumo inayotumika, bidhaa zote za nje zinazoingia Tanzania Bara kupitia Zanzibar hufanyiwa uhakiki licha ya kuwa zimethaminiwa Zanzibar, iwapo uthamini wa Tanzania Bara utakuwa sawa na ule uliofanywa Zanzibar hakuna kodi itakayotozwa Tanzania Bara na ikiwa kodi iliyolipwa Zanzibar ni ndogo, Mamlaka ya Mapato hukusanya tofauti ya kodi iliyozidi”, amesema Dk. Kijaji.

Kulingana na utaratibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ushuru wa bidhaa ni kodi inayotozwa kwa bidhaa au huduma maalumu zilizozalishwa ndani ya nchi au kuingizwa nchini kwa viwango tofauti. Kodi hii inatozwa katika viwango maalumu na viwango kulingana na thamani.

Dk. Kijaji amesisitiza kuwa utaratibu wa kukusanya tofauti ya kodi kati ya Zanzibar na Bara kwa kutumia mifumo ya TANCIS na IECD haina lengo la kuua biashara Zanzibar, bali hatua hiyo inalenga kuleta usawa wa gharama za kufanya biashara na ushindani hapa nchini.

Aidha Naibu Waziri huyo amesema kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 63 (2) Bunge ni muhimili unaojitegemea na hivyo Serikali haina mamlaka ya kuunda Kamati ndogo ya Bunge kwa ajili ya jambo hilo au jambo lolote.

Ikumbukwe kuwa kodi ya Mapato na ushuru wa bidhaa katika ya nchi hizo mbili umekuwa ni kero ya muda mrefu ya Muungano ambayo haijapatiwa ufumbuzi na kwa nyakati tofauti Wazanzibar wamekuwa wakilalamika kukosa sauti kwenye mapato wakidai hakuna usawa kwenye suala hilo.

Mwanasheria kutoka Zanzibar, Awadh Ali Said, alipokuwa anazungumzia matatizo ya Muungano katika muktadha wa mapato alinukuliwa; “suala la mapato linaanguka katika suala la uchumi huku uchumi ukiwa si suala la muungano”.

Anaongeza kwamba; “kila mmoja (kati ya Tanganyika na Zanzibar) ina uchumi wake na mzigo wa kushughulikia lakini nyenzo kuu za uchumi ambazo ni sera za fedha, sera za kodi, benki kuu, yote hayo yako upande mmoja (Tanzania Bara)”.

Kutokana na hali hiyo upande wa Zanzibar umekuwa ukilalamika kukosa nguvu ya kudhibiti uchumi na sarafu. Suala la kodi limezungumzwa kwa muda mrefu lakini mpaka sasa halijapatiwa ufumbuzi baina ya nchi hizo mbili.

Januari 4, mwaka huu, Rais wa Zanzbar, Dk. Ali Mohammed Shein wakati wa ufunguzi wa jengo la Takwimu mjini Zanzibar, alinukuliwa akisema “si busara kwa mambo ya muungano kufanywa upande mmoja tu au upande mmoja kuonekana unajivutia wenyewe kila kitu, hali hiyo inaweza kuleta madhara makubwa katika utendaji wa masuala ya muungano.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *