Ripoti mpya iliyotolewa na taasisi huru ya Freedom House imesema misingi ya demokrasia ikiwemo uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kukusanyika imeendelea kudhoofika nchini Tanzania na hali hiyo isiporekebishwa itaingia kwenye kundi la nchi zisizo na uhuru kabisa duniani.
Kulingana na Freedom House ambao walichambua data katika nchi 195 za ulimwenguni katika mwaka 2017 wamebaini kuwa nchi 88 zina uhuru, 58 zimejumuishwa kwenye kundi la nchi zenye uhuru kiasi huku 48 zikiwekwa kwenye kundi la nchi zisizo na uhuru kabisa.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa misingi ya demokrasia ikiwemo uchaguzi usio huru na haki, uhuru wa kujieleza umeendelea kushuka kwa mwaka wa 12 mfufululizo duniani kote. Miongoni mwa matokeo yaliyostaajabisha ni kudhoofika kwa Marekani ambayo ni mama wa demokrasia kutokana na uchunguzi unaofanywa na Mwendesha Mashtaka Maalumu kuhusu Urusi kuingilia uchaguzi mkuu wa mwaka 2016 ambao ulimpa ushindi Rais Donald Trump.
Tanzania imewekwa kwenye nchi 88 ambazo zina uhuru kiasi lakini inatahadharishwa kuwa inaweza kuingia kwenye nchi zisizo na uhuru kabisa. Tahadhari hiyo inatokana na mwenendo wa viongozi wa serikali kufungia vyombo vya habari, kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, kushtakiwa kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii kwa tuhuma za uchochezi na kukamatwa kwa wapinzani wa kisiasa ambao wanakosoa na kutoa mawazo yanayotofautiana na serikali.
Pia utekelezaji wa Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015, Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016 na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 umekuwa ukilalamikiwa na wadau wa maendeleo kuwa ni mkakati wa kudhoofisha uhuru wa kutoa maoni, uwazi na uwajibikaji.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) nchini hivi karibuni kilitoa tamko la tathmini ya uchaguzi mdogo wa marudio wa kuchagua madiwani uliofanyika katika kata 43 kwenye mikoa 19 ya Tanzania Novemba 24 mwaka jana ambapo kilibaini mambo mbalimbali ya ukiukwaji wa haki za binadamu.
Tathmini hiyo iliibua mambo mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya nguvu ya vyombo vya dola, matukio ya watu kutekwa na watu wasiojulikana, watu kupigwa, kujeruhiwa kwa lengo la kuharibu na kuvuruga uchaguzi na vilevile kuwatia hofu wapiga kura.
Afrika Mashariki hali bado tete
Tanzania inaungana nchi nyingine za Afrika Mashariki ikiwemo Kenya na Uganda ambazo nazo zimewekwa kwenye kundi la nchi zenye uhuru kiasi huku za Rwanda, Burundi na Sudan ya Kusini zimejumuishwa kwenye nchi zisizo na uhuru kabisa.
Awali Uganda ilikuwa kwenye nchi zisizo na uhuru kabisa lakini imepanda hadi kwenye uhuru kiasi kwasababu ya kuimarika kwa tasnia ya habari na utashi wa wanahabari, blogu na uhuru wa wananchi kutoa maoni yao licha ya mazingira ya kisiasa kuminywa na utawala wa muda mrefu wa Rais Yoweri Museveni.
Rais Museveni mwenye umri wa miaka 73 amekuwepo madarakani tangu 1986 amefanikiwa kubadilisha sheria ya ukomo wa umri wa miaka 75 wa kugombea urais ambapo atapata fursa ya kugombea tena mwaka 2021. Chaguzi nchini Uganda zimekuwa zikitawaliwa na vurugu za polisi na wananchi, kuzimwa kwa intaneti na kuwekwa kizuizini kwa viongozi wa upinzani ikiwemo Kizza Besigye wa chama cha Forum for Democratic Change.
Kwa upande wa Kenya ambayo imekuwa ikisifika kwa kuimarisha misingi ya demokrasia katika ukanda wa Afrika Mashariki ambapo kwa mara ya kwanza mahakama ilifanikiwa kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa Urais yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta uliofanyika Agosti 2018. Uchaguzi ulirudiwa na Rais Kenyatta alichaguliwa tena.
Marudio ya uchaguzi yalilamikiwa na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa kuwa hayakuzingatia haki za binadamu ambapo watu ambao walipinga uchaguzi huo walikumbana na mkono wa dola. Matendo hayo ndiyo yaliiweka Kenya kwenye kundi la nchi zilizo na uhuru kiasi.
Burundi na Sudan Kusini zimewekwa kwenye kundi la nchi zisizo na uhuru kabisa kutokana na mapigano ya kikabila ambayo yamedhoofisha mfumo wa kisiasa wa kuongoza nchi. Vyombo vya habari na wananchi wanaotoa maoni tofauti na serikali wamekuwa wakiteswa, kufungwa na kuuwawa.
Chanzo: Freedom House – Nchi zisizo na uhuru – Nchi zenye uhuru – nchi zenye uhuru kiasi
Hali ilivyo Afrika
Afrika kama zilivyo nchi za Afrika Mashariki hali ya demokrasia siyo ya kuridhisha ikizingatiwa kuwa asilimia 11 ya wakazi wapatao bilioni 1.02 wa bara hilo ndio wana uhuru wa kweli, huku 52% wana uhuru kiasi na 37% hawa uhuru kabisa.
Ripoti ya Freedom House inaeleza kuwa waliangazia nchi 49 za Afrika na kugundua kuwa nchi 8 (18%) ndio zina uhuru wa kweli, nchi 22 (43%) zina uhuru kiasi na 19 (39%) hazina uhuru kabisa. Nchi zinazotajwa kuwa na uhuru ni Afrika Kusini, Namibia, Botswana, Ghana, Togo, Senegal na Kisiwa cha Sao Tome.
Sababu ya nchi nyingi za Afrika kuwepo kwenye kundi la zisizo na uhuru ni matokeo ya viongozi kukaa madarakani muda mrefu, vurugu za kisiasa na kikabila ambazo zimekuwa zikihatarisha haki za binadamu.
Demokrasia ya Dunia
Demokrasia ya dunia inakabiliwa na mzozo mkubwa wa kisiasa kuliko wakati mwingine ambapo mwaka 2017 ulishuhudia ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwemo kuminywa kwa uchaguzi huru na kweli, haki za watu wachache, uhuru wa kujieleza, utawala wa sheria.
Nchi 71 kati ya 195 zimeshuhudiwa zikiteteleka katika kulinda haki za kisiasa na jamii ambapo ni nchi 35 tu ndizo zimeweza kulinda haki hizo. Kudhoofika kwa demokrasia kunaendelea kushuka kwa miaka 12 mfululizo na hatua muhimu zisipochukuliwa amani ya dunia itawekwa rehani.
Marekani ambayo ni bingwa wa demokrasia duniani nayo imeripotiwa na taasisi ya Freedom House kudhoofika katika kulinda haki za kisiasa na kijamii na kuzua mgongano wa mawazo miongoni mwa nchi zinazoibukia katika kujenga demokrasia ya dunia.
Tangu kuisha kwa vita baridi, nchi nyingi ziliachana na utawala wa kiimla na kugeukia demokrasia ya vyama vingi lakini hali hiyo imeanza kujitokeza tena ambapo idadi ya viongozi wanaoongoza kwa udikteta inaongezeka.
Uhuru wa nchi moja unategemea uhuru wa nchi zote
Demokrasia itabaki kuwa tunu muhimu kwa jamii zilizostaarabika, ikifungua milango ya uwazi, mawazo na fursa mpya na zaidi ya yote kulinda uhuru wa mtu mmoja mmoja. Ikiwa watu duniani kote wanadai mazingira mazuri ya kisiasa ni dhahiri wanakumbatia misingi ya demokrasia: uchaguzi huru, uhuru wa kujieleza, uwazi na uwajibikaji wa serikali, utawala wa sheria ambao hauingiliwi na polisi, jeshi au taasisi nyingine za nchi.
Hata hivyo, Karne ya 21 imeshuhudia ugumu wa kuifanya demokrasia kuwa endelevu ambapo baadhi ya nchi zinatekeleza lakini zingine zinapuuza. Utawala wa kidekteta wa Urusi na China unatambua wazi ili uendelee kuwepo unahitaji kuimarisha demokrasia katika nchi nyingine ili ziendelee kufaidika na mahusiano ya kidiplomasia. Ukuaji wa demokrasia ni kulinda haki za watu wote duniani kupitia utandawazi
So what next? If the situation will continue to exist?