Utafiti uliotolewa hivi karibuni umebaini kuwa watu wanaochelewa kulala wana uwezekano mkubwa wa kufa mapema kuliko wale wanaoamka mapema wakati wa usubuhi.
Msingi wa utafiti huo ni kwamba watu wanaolala muda mzuri na kuamka mapema wanaweza kuishi muda mrefu ukilinganisha na wale ambao wanachelewa kulala ambao wakati mwingine wanaamka mapema wakiwa na uchovu mwingi.
Matokeo ya utafiti huo ambayo yamechapishwa kwenye Jalida la Chronobiology International, yamechambua sampuli ya watu laki 5 wenye umri wa miaka 30 hadi 73 ambao walifuatiliwa tabia za ulalaji wao kwa zaidi ya miaka 6 na nusu.
Watafiti walibaini kuwa watu ambao walikuwa wanachelewa kulala walikuwa na hatari kwa asilimia 10 kufa mapema katika kipindi cha utafiti kuliko wale ambao wanalala mapema na kuamka mapema.
Watafiti wengine kutoka Chuo Kikuu cha Surrey nchini Uingereza na wale wa Chuo Kikuu cha Northwestern kilichopo Chicago, Marekani walibaini kuwa watu wanaochelewa kulala au wanaokesha kama bundi (night owls) wana uwezekano mkubwa wa kupata matatizo ya kisukari, akili na mfumo wa upumuaji.
Hii siyo mara ya kwanza kwa utafiti ambao unahusianisha kati ya kuchelewa kulala na matatizo ya kiafya. Tafiti zingine zimehusianisha ukeshaji na hatari kubwa ya kupata msongo wa mawazo, matumizi ya madawa ya kulevya, mtindo wa tabia hasi kama kutokula mlo kamili, unene uliopitiza.
Sababu nyingine ambayo ni muhimu ni kwamba dunia imeundwa kwa watu wa asubuhi (wanaoamka mapema). “Afya dhoofu ya watu wanaochelewa kulala inni matokeo ya kushindwa kupanga muda wa kulala na muda wa shughuli za kijamii,” inaeleza sehemu ya utafiti huo.
Hata hivyo, Utafiti umeonyesha uhusiano pekee kati ya kuchelewa kulala na kufa mapema, lakini matokeo hayo bado hayajakamilika. Haiwezekani kusema watu walioshiriki kwenye utafiti walikuwa wanachelewa kulala au walikuwa wanaamka mapema wakati wote.
Ikiwa shughuli zinazomfanya mtu achelewe kulala zinaweza kusababisha kufa mapema, kuna nafasi ya kuingilia kati na kuchunguza zaidi. Japokuwa watafiti wanasema mfumo wa vinasaba vinaweza kuchangia mtu kuchelewa kulala au kuamka mapema, lakini hilo linaweza kudhibitiwa na baadhi ya watu.
Katika taarifa ya utafiti huo, Mwandishi kiongozi, Profesa Mshiriki katika Shule Kuu ya Feinberg ya Chuo Kikuu cha Northwestern , Kristen Knutson amesema ikiwa watu wanataka kuwa na tabia ya kuamka mapema wanatakiwa kuzingatia muda wa kulala ili kujiepusha na hatari inayoweza kuwapata. Kukamilisha shughuli mapema ili kupata muda mzuri wa kupumzika, kuamka mapema na kupata jua la asubuhi lenye vitamin D.