Utata, nadharia iliyojificha kwenye Hati, kero za Muungano wa Tanzania

Jamii Africa

Leo watanzania kutoka nchi mbili za Zanzibar na Tanzania Bara wanaungano kusherehekea miaka 54 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulioasisiwa April 26, 1964 na viongozi wawili wa kitaifa; Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Aman Abeid Karume.

Maadhimisho hayo yanafanyika pale mjini Dodoma, makao makuu ya nchi  na mgeni rasmi ni rais John Magufuli ambapo ataambatana na viongozi mbalimbali waandamizi katika kutathmini mafanikio na changamoto za muungano.

Lakini Muungano bado una kero ambazo hazitafutiwa ufumbuzi licha ya kuwepo mijadala mbalimbali inayonuia kuimarisha Muungano.

Akiwasilisha Mada yake kuhusu Muungano kule Wete- Pemba mwaka 2012, Profesa Abdul Sherrif wa Baraza la Katiba la Zanzibar katika Mjadala wa Katiba Mpya, alizungumza mambo mengi ambayo ndiyo kiini cha kero zisizokwisha za muungano wa nchi hizi mbili.

Jambo mojawapo ni hati ya Muungano ambayo inasimama kama katiba ya muungano ambayo bado inaleta changamoto katika uimarishaji wa Jamhuri.

Prof. Sherrif katika mada yake alieleza kuwa, “katika Hati ya Muungano, kitu kilichofanyika ni kwamba, jina la Serikali ya Tanganyika likabadilishwa na kupewa jina la Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Baadae ikabidilishwa kuwa Tanzania, na kutaka kuufuta kabisa utaifa wa Zanzibar. Wako wanaosema kuwa hiyo haikuwa sawa. Hata Katiba ya Tanganyika ikatumika, baada ya kurekebisha mambo machache tu, kama kubadilisha jina na bendera.

SMZ (Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) ikabakia, lakini madaraka 11 ya serikali hiyo yalihamishwa na kupelekwa kwenye Serikali ya Muungano. Sasa, tukiweka serikali 2 hizi katika mizani, zitakuwa hazina usawa tena, kwa sababu Serikali ya Muungano sasa imekusanya madaraka yote ya Tanganyika na mambo 11 ya Zanzibar.

Mambo haya 11 ya Muungano si yote yana sura ya kimataifa, bali yanahusu mambo mengi ya uchumi wa ndani. Biashara ya Nje ni katika mambo hayo ya Muungano, lakini uchumi wetu wakati ule ulikuwa unategemea sana uuzaji wa karafuu nchi za nje. Hali kadhalika, Kodi ya Mapato na Ushuru wa Bidhaa yote haya yamehodhiwa na Serikali ya Muungano, na SMZ inapewa ruzuku ya aslimia nne nukta tano (4.5%) tu.

Vilevile, SMZ inakosa madaraka juu ya biashara na kodi, hivyo inakosa uwezo wa kupanga uchumi wa nchi moja kwa moja. SMZ imeachiwa kazi ya kuendesha serikali bila kupewa nyenzo ya fedha. Kwa hivyo, hata mgawanyo wa madaraka haukuwa wa usawa.

Hati ya Muungano ni mkataba wa kimataifa kama unavyojulikana katika sheria ya kimataifa, na haiwezi kubadilishwa kila mara. Iligawana madaraka kati ya SMZ iliobakia na mambo yote yasiokuwa ya Muungano, na Serikali ya Muungano iliokuwa na madaraka yote ya Tanganyika yasiyo ya Muungano, na Mambo 11 ya Muungano ya Tanganyika na ya Zanzibar.

Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Karume wakiweka saini kwenye hati ya Muungano mwaka 1964. 

Lakini mambo hayakuishia hapo. Kila mwaka au miaka 2, madaraka mengine ya Zanzibar yalikuwa yananyakuliwa na kufanywa Mambo ya Muungano, haya ni pamoja na sarafu (1965), mafuta na gesi (1968)-hili limerudishwa mikononi mwa SMZ, na hata Baraza la Mitihani (1973).

Mpaka sasa, mambo mengine 11 yamehamishwa kutoka katika madaraka ya SMZ na kupelekwa Dodoma – wengine wanasema mambo haya ni 22. Maana yake ni kwamba ile mizani iliyoinama sana baada ya kuundwa Muungano, basi sasa imelala chini kabisa.

Hapa tunapaswa tujiulize swali, je hii ilikuwa ni halali? Hapa hatuna budi kumnukuu Prof. Shivji, mwanasheria aliyebobea katika sheria ya katiba. Huyu sio Mzanzibari lakini ni Mtanganyika; yeye si adui wa Mwalimu Nyerere bali ni mpenzi wa mawazo ya Mw Nyerere.

Mwaka wa 1990 alitoa hotuba yake muhimu sana kama tunataka kufahamu chanzo na sababu za ‘Kero za Muungano’:

Alieleza kwamba sehemu ya Hati ya Muungano inayotaja mambo 11 ya Muungano, ndiyo iliyogawana madaraka kati ya serikali mbili, na kwa hivyo haiwezi kubadilishwa bila kuvuruga muundo mzima wa Muungano.

Na anaendelea kusema kwamba, si Bunge wala Baraza la Wawakilishi, kwa kila mmoja peke yake, hawana madaraka ya kubadilisha sehemu hii ya Hati ya Muungano. Kwa hivyo, Bunge kubadilisha sehemu hii, kama ilivyofanya mara 11, ni kuzidisha madaraka yake, na kuipokonya Zanzibar. Huu ni ‘unyang’anyaji na ubomoaji wa mfumo halisi wa Muungano.’ Mwisho wake SMZ itabakia na kete tupu.

Prof Shivji anamalizia kwa kusema kwamba, mabadiliko yote yaliyofanyiwa sehemu hii ya Hati ya Muungano ni ‘haramu na batili.’

Kwa bahati mbaya, Serikali ya Tanzania hawakujali onyo la Profesa Shivji, baada ya miaka miwili tu, waliporejesha mfumo wa vyama vingi, wakaendelea na mtindo wao wa kawaida. Wakachukuwa fursa ya kumnyima Rais wa Zanzibar, anaechaguliwa na watu wa Zanzibar, nafasi yake kama Makamo wa Rais wa Tanzania, iliyotajwa katika Hati ya Muungano.

Yeye alikuwa kiungo muhimu kati ya SMZ na Serikali ya Muungano. Sheria hii ilipitishwa na Bunge bila kuhitaji kura ya Theluthi Mbili (2/3) kwa pande zote mbili. Wabunge wengi wa Zanzibar waliogopa kupinga msimamo wa chama tawala.

Mwalimu Nyerere akichanganya udongo wa Tanzania Bara na Tanganyika kuashiria muungano nchi mbili

Baadaye tu wakazinduka na wakaamua kumuingiza Rais wa Zanzibar kama Waziri bila Kazi Maalum katika Baraza la Mawaziri la Tanzania, ambayo ni kumvunjiya heshima yake. Badala yake, wakaleta mfumo wa Makamo Mwenza anaechaguliwa na Watanzania wote, na anatakiwa awashughulikie Watanzania wote, lakini hana nafasi katika SMZ.

Kwa ufupi, ongezeko la Mambo ya Muungano baada ya 1964, na kumuondosha Rais wa Zanzibar kutoka nafasi yake ya Makamo wa Rais wa Tanzania, yamevuruga kabisa muundo wa Muungano. Vilevile, yamevunja Hati ya Muungano, ambayo ilikuwa mkataba wa kimataifa kati ya Tanganyika na Zanzibar.

Hati ya Muungano ndio Katiba Mama ya Tanzania. Kwa kiasi kikubwa, mambo yaliofanyika baada 1964 kwa makusudi hayakutaka kuheshimu makubaliano kati ya Marehemu Mzee Karume na Mw. Nyerere, na kuheshimu utaifa wa Zanzibar. Sasa, hata Jaji Mkuu (wa wakati huo) na Waziri Mkuu wanathubutu kusema Zanzibar si nchi.”

Huo ndio ulikuwa mtazamo wa Prof. Sherrif kuhusu hati na kero za Muungano na jinsi unavyoleta changamoto kwa nchi zote mbili.

 

Nini Kifanyike

Wadau mbalimbali wameitaka serikali ya Jamhuri kuzileta nchi zote mbili pamoja na kujadili kwa kina mambo yenye changamoto ili kuhakikisha kunakuwa na usawa katika utekelezaji wa matakwa ya hati ya Muungano na Katiba ya nchi.

Mbunge wa Temeke, Maulid Mtolea, akiwa bungeni hivi karibu alisema, “Nawapongeza wazanzibar kwa umoja wao wa kuipigania Zanzibar yao bila kuzingatia wanatokea upande upi wa kisiasa, ndio maana wenzetu wanafanikiwa. Watu wanahisi Tanzania bara hakuna kero za Muungano lakini ukweli ni kwamba kero za upande huo hazina pa kwenda, hazina wa kuzisemea.’

Alisema ili muungano udumu na kuwa imara kuna umuhimu wa kupunguza manung’uniko kwa kujadiliana na kutafuta ufumbuzi wa kero zilizopo.

“Kuwafurahisha watanzania bara siyo kuwabana wazanzibar, ni kuwaacha watanzania bara nao waseme,” alisema Mtolea.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dkt. Hellen Kijo Bisimba amesema watanzania wakubali kuwa kero zipo na watafute njia mbadala za kuzitatua ili matunda ya muungano yaonekane dhahiri kwa pande zote mbili.

“Huu muungano ni muhimu na inasemekana ni wa tofauti sana na wa aina yake na unahitaji kulindwa lakini hautalindika kama tusipokubali kukaa chini na kuuzungumzia na kuona zile tunaziita kero zinachukuliwa na kufanyiwa ufumbuzi,” ameshauri Dkt. Hellen.

Akizungumza kwa niaba ya serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Raisi (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema kero zilizopo hazitaweza kuyumbisha muungano na wataendelea kutafuta mbinu mbalimbali kuhakikisha unadumu daima.

“Hakuna changamoto yoyote inayoweza kutufarakanisha, kutenganisha wala kuturudisha nyuma…kwa watu wote na pande zote za Muungano. Mjadala sio uhalali wa Muungano bali mbinu za uimarishaji,” alibainisha Makamba.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *