Tofauti ya utegemezi kati ya bajeti kuu ya serikali na bajeti ya elimu yaibua mjadala

Jamii Africa

Wakati utegemezi katika bajeti kuu ya Serikali ukishuka mwaka hadi mwaka, utegemezi katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia umekuwa ukiongezeka jambo ambalo wadau wanaeleza kuwa huenda likaathiri utoaji wa elimu bora pale wahisani wanaposhindwa kutoa mikopo au misaada waliyoahidi kwa wakati.

Utegemezi wa fedha za nje katika bajeti ya elimu, kwa mujibu wa wadau unaweza kuathiri uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia na kufundishia ikiwa Serikali haitaimarisha mfumo wa ukusanyaji mapato ya ndani.

Uchambuzi wa bajeti  za wizara ya elimu kwa miaka minne uliofanywa na Fikra Pevu umebaini kuwa katika kipindi cha miaka minne mfululizo tangu mwaka wa fedha 2015/2016 hadi mwaka wa fedha ujao wa 2018/2019 utegemezi wa fedha za nje katika miradi ya maendeleo katika bajeti ya wizara ya elimu umekuwa ukiongezeka kila mwaka.

Hali hiyo ni tofauti na bajeti kuu ambayo katika kipindi hicho  utegemezi umekuwa ukipungua mwaka hadi mwaka kiasi cha kuibua mjadala juu ya mgawanyo na  mwenendo wa mapato na matumizi ya serikali.

Fedha za nje ambazo hutafsiriwa kama utegemezi hujumuisha misaada, mikopo yenye masharti nafuu na ufadhili wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambazo hutolewa na mashirika ya kimataifa ya fedha na nchi marafiki.

Katika mwaka wa fedha ujao wa 2018/2019, wizara ya elimu imepanga kutumia Sh1.4 trilioni ambapo kati ya fedha hizo Sh311 bilioni ni fedha za nje sawa na asilimia 22.11 ya bajeti yote.

Katika mwaka ujao wa fedha, bajeti kuu inatarajiwa kuwa Sh32.4 trilioni na mapato ya nje yatakuwa Sh2.67 trilioni sawa na asilimia nane ya mapato yote ya Serikali kwa mwaka huo.

Hata hivyo utegemezi ya wizara ya elimu umepungua kiduchu kwa 0.57% ukilinganisha na mwaka 2017/2018 ambapo mapato ya nje yalikuwa Sh310.07 (22.68%).

Iwapo utalinganisha na mwenendo wa utegemezi wa bajeti kuu ya Serikali ambao upo ndani ya tarakimu moja,  bado utegemezi wa bajeti ya elimu umekuwa ni mkubwa kwa miaka mitatu mfufululizo (2016/2017-2018/2019) kwa kuwa umevuka asilimia 20 ya bajeti yote.

Katika kipindi hicho, bajeti ya elimu imekuwa ikitegemea zaidi ya moja ya tano ya bajeti yake yote kutoka kwa wahisani, jambo ambalo haliashirii mwelekeo mzuri wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika wizara hiyo.

Ni mwaka 2015/2016 pekee wizara hiyo ilijadhatiti kutumia fedha zake za ndani kuendesha wizara.

Pia katika kipindi hicho cha 2015/2016 Serikali ilipanga kupata fedha za nje Sh4.46 trilioni kwa ajili ya bajeti kuu sawa na asilimia 19.8 ya bajeti yake yote kabla ya kufanya mageuzi makubwa mwaka uliofuata ambapo ilipunguza utegemezi wa nje hadi kufikia trilioni 3.12 kati ya trilioni 29.54 ya bajeti kuu.

Katika mwakao huo, wizara ilitumia asilimia 3.24 ya fedha za nje kugharamia shughuli za maendeleo na kiasi hicho kikaongezeka mara sita zaidi na kufikia asilimia 19.82 mwaka uliofuata wa 2016/2017.

  • Ukitaka kujua matokeo ya shule za sekondari tembelea hapa- Elimu Yangu

Ongezeko kubwa la utegemezi katika mwaka 2016/2017 huenda lilichochewa na kuanza kutekelezwa  kwa sera ya elimu bure ambayo ilihitaji fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu nchini.

Hata hivyo, bajeti ya elimu imekuwa ikiongezeka kila mwaka huku fedha zinazotengwa kutekeleza miradi ya elimu ikiwemo uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia na kufundishia nazo zimekuwa zikiongezeka kila mwaka.

Mathalani mwaka 2015/2016 bajeti ya maendeleo ilikuwa 48.3% katika mwaka uliofuata wa 2016/2017 bajeti hiyo iliongezeka hadi 64.2% na 2017/2018  (68.5%) iliongezeka kabla ya kushuka mwaka 2018/2019 hadi kufikia 926.96 (66.1%).

                                    Fedha za maendeleo ni muhimu kwa uboreshaji wa mazingira ya kusomea

Kutokana na ukweli kwamba utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya elimu hutegemea kwa sehemu fedha za nje, wadau wanaeleza kuwa kuna uwezekano likaathiri utoaji wa elimu bora pale wahisani wanaposhindwa kutoa mikopo na misaada waliyoahidi kwa wakati.

Katika mapendekezo  ya Serikali ya mpango wa maendeleo ya Taifa na kiwango cha ukomo wa bajeti wa 2018/2019, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango alisema “kuchelewa kupatikana kwa misaada na mikopo kunatokana na majadiliano na washirika wa maendeleo kuchukua muda mrefu; na pia kupanda kwa riba ya mikopo ya kibiashara katika soko la fedha la kimataifa.”

 

Nini kifanyike

Wadau wa masuala ya elimu wameishauri serikali kuimarisha mfumo wa makusanyo ya ndani na kupunguza utegemezi wa fedha za wahisani ili kuhakikisha bajeti ya maendeleo inapatikana kwa wakati.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la HakiElimu, Dk. John Kallaghe wakati akitoa mapendekezo ya shirika lake kwa bajeti ya wizara ya elimu ya 2018/2019 alisema serikali inapaswa kubuni vyanzo vya ndani vitakavyoihakikishia wizara uhai wakati wote.

“Serikali inatakiwa kutenga na kuongeza bajeti kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika sekta ya elimu na hasa fedha zinazokwenda Ofisi ya Rais-Tamisemi kwa ajili ya elimu msingi.

“Lakini bajeti ya maendeleo itegemee vyanzo vya mapato vya ndani na kutenga bajeti yenye uhalisia wa kutatua changamoto sugu na muda mrefu za miundombinu mashuleni,” anasema Dk Kallaghe.

             Utegemezi wa bajeti unaathiri uboreshaji wa miundombinu ya shule

 

Serikali yajipanga kupunguza utegemezi

Serikali  imeeleza kuwa itaimarisha sera za mapato kwa mwaka 2018/19 ili kuongeza mapato ya ndani kwa kurahisisha ulipaji wa kodi kwa kutumia mifumo ya kielektroniki na kuendelea na zoezi la kurasimisha sekta isiyo rasmi.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango amesema fedha za ndani zitakazopatikana zitaelekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na uboreshaji wa huduma za kijamii ikiwemo elimu.

“Eneo hili linalenga kuendeleza mafanikio ya upatikanaji wa huduma msingi kwa ustawi wa maisha ya Watanzania. Miradi katika eneo hili ni pamoja na: ujenzi na ukarabati wa maktaba za mikoa; ujenzi na uboreshaji wa maabara katika shule na taasisi; kuendeleza ujenzi na kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji, kupanua huduma za elimu ya afya na usafi wa mazingira shuleni, mijini na vijijini,” ameeleza Dk Mipango.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *