Hivi karibuni Rwanda imebadili Sheria yake ya mwaka 2009 iliyokuwa inakataza umiliki na uuzwaji wa silaha za moto. Sheria mpya ya silaha za moto nchini humo inaruhusu wananchi kumiliki silaha na pia watu binafsi kufungua maduka ya uuzwaji wa silaha za moto.
Sheria inaenda mbali zaidi na kuruhusu uwekezaji wa viwanda vya silaha za moto nchini Rwanda.
Serikali ya Rwanda imetetea uamuzi huo kwa kusema ni wakati sahihi kwa raia wake kumiliki silaha na kudai kuwa itasimaia vizuri sekta hiyo ili isilete madhara.
Hatua hii ya kubadili Sheria na kuruhusu watu binafsi kuwa na maduka ya kuuza silaha za moto na pia kuruhusu uwekezaji katika viwanda vya silaha za moto imeamsha hisia tofauti za wananchi na wachambuzi mbalimbali masuala ya usalama Afrika.
Nchi zetu za Afrika bado zinakabiliwa na changamoto lukuki ikiwamo usalama, vita vya wenyewe kwa wenyewe, ujambazi uliokithiri, ugaidi, fujo katika chaguzi na mambo mengine mengi.
Haya na mengine mengi yanaleta hofu endapo ubinafsishaji holela unafanyika katika silaha za moto. Hapa najaribu kufikiria matokeo ya mbele zaidi, kwani madhara yake yanaweza yasiwe sasa ila katika muda mrefu ujao tunaweza kuyaona kwa wingi.
Nieleze wasiwasi wangu katika uamuzi huo wa kubinafsisha sekta ya silaha za moto. Kwanza kabisa sio wananchi kumiliki silaha, hili halina tatizo sana kwani hata Tanzania tunafanya hivi lakini kupitia kwa taasisi za Serikali.
Wasiwasi mkubwa nilionao ni kubinafsisha silaha za moto kuuzwa katika masoko huria na wawekezaji kuwekeza katika sekta hiyo.
Najaribu kutafakari, Je, hitaji la wananchi lilikuwa silaha za moto kana kwamba kulikuwa na upungufu kiasi cha kuruhusu watu kuwekeza katika sekta hiyo?
Je, ajenda hii haina msukumo wowote kutoka kwa mabepari ambao biashara yao kubwa ni uuzaji wa silaha za moto na wanatafuta masoko mapya Afrika?
Duka la silaha za aina mbalimbali
Twakimu za Taasisi ya Utafiti ya Stockholm International Peace (SIPRI) za mwaka 2015 zinaonesha kuwa makampuni makubwa kumi bora ya utengenezaji wa silaha za moto duniani, nane yanatoka Marekani, moja Italia na lingine Umoja wa Ulaya.
Takwimu hizi pia zinaonesha nchi zinazouza silaha za moto kwa wingi duniani ni pamoja na Marekani, Urusi, China, Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, Uhispania, Italia, Ukraine na Israeli.
Taarifa ya SIPRI ya mwaka 2012 zinaeleza kuwa nchi kumi bora zinazoagiza silaha kwa wingi duniani ni India, Saudi Arabia, Umoja wa Kiarabu, China, Australia, Aljeria, Uturuki, Iraq, Pakistani, Vietnam. Katika orodha hii, utaona nchi za Afika ni chache sana kwani nyingi huagiza silaha kwa kiwango kidogo na nyingine hufanya biashara kwa magendo.
Kwa takwimu hizo hapo juu, ni dhahiri sasa mabepari hawa wanatafuta mahala pa kuwekeza viwanda vyao vya silaha za moto na Afrika ni chaguo lao kwa wakati huu.
Hata hivyo, Hii inaweza kuwa fursa nzuri kwa Rwanda kwani watapata wawekezaji wengi katika sekta hii ila waathirika wa silaha hizi za moto ni majirani ambao inatupasa tukae chonjo sasa.
Marekani kama mfano duniani imekuwa muhanga mkubwa wa Sera na Sheria zake za ubinafsishaji wa silaha za moto ambapo upatikanaji wa silaha umekuwa rahisi kiasi kwamba maduka binafsi yanauza silaha hizo.
Tangu mwaka 2011, kumezuka matukio mengi ya watu kupigwa risasi katika shule na maeneo yenye mikusanyiko ya watu. Matukio haya nchini Marekani yanazidi kila mwaka na sasa wananchi wameanza kuipigia kelele sheria ya silaha za moto ibadilishwe.
Ugumu wa kubadili Sheria hizi nchini Marekani unatokana na ukweli kwamba ni biashara inayoingiza kipato kikubwa kwa makampuni ya nchi hiyo. Takwimu za SIPRI za mwaka 2012 zinakadiria kuwa mapato ya jumla ya makampuni 100 makubwa ya uuzaji wa silaha za moto yanafika Dola za Marekani 395 bilioni.
Kwa hakika hii ni biashara kubwa inayoweza kuipatia nchi mapato. Na sasa tunaweza kushuhudia Rwanda ikiwa moja ya nchi inayoweza kufaidika na mpango huu wa ubinafsishaji sekta ya silaha za moto.
Lakini fursa hiyo ya Rwanda kutengeneza silaha inapaswa kuangaliwa kwa jicho la tatu ili isiwe chanzo cha kuchochea machafuko katika nchi za Afrika, ikizingatiwa kuwa bado bara hilo halijatulia; ziko nchi kama Sudan ya Kusini, Somalia, Congo DRC, Jamhuri ya Kati, Burundi ambazo zinakumbwa na mizozo ya kisiasa.
Nchi hizo zinaweza kutumia silaha zinazouzwa Rwanda kuendeleza mapigano katika nchi zao. Katika hili serikali ya Rwanda inapaswa kuweka mfumo madhubuti wa kusimamia utengenezaji na uuzaji wa silaha hizo ili zisivurue amani ya Afrika.