Imeelezwa kuwa uhaba wa walimu na mlundikano wa wanafunzi katika madarasa ya awali ni kikwazo kwa Tanzania kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu ya 2030 yanayohimiza utolewaji wa elimu bora na yenye usawa.
Uchambuzi wa takwimu uliofanywa na FikraPevu kuhusu elimu ya awali umebaini kuwa miaka miwili mfufulizo tangu mwaka 2016, uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi katika madarasa ya awali umekuwa sio wa kuridhisha.
Hali hiyo imesababishwa na upungufu wa walimu katika madarasa ya awali ambapo mzigo wa walimu kufundisha watoto wengi umeongezeka, jambo linalotishia mstakabali wa elimu ya watoto wanaoandaliwa kuingia katika shule za msingi.
Kwa mujibu taarifa ya mapendekezo ya bajeti ya elimu ya Shirika la HakiElimu (2018) yaliyotolewa hivi karibuni yanaonesha kuwa uwiano wa mwalimu kwa mwanafunzi kwa mwaka 2017 ulikuwa mwalimu 1 kwa wanafunzi 159 (1:159) ukilinganisha na uwiano wa mwaka 2016 ambapo ulikuwa 1:135.
Hiyo ni sawa na kusema wanafunzi katika madarasa ya awali waliongezeka zaidi kwa mwaka 2017 lakini idadi ya walimu haikuongezeka au ilipungua kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa sera elimu bila malipo.
Kimsingi mzigo wa walimu kufundisha umeongezeka ukilinganisha na mwaka 2016. Kwa mfano kama darasa la moja la awali lilikuwa na wanafunzi 135 ina maana mwaka uliofuata (2017) waliongezeka wanafunzi wengine 29.
Mtaala wa Elimu ya Awali Tanzania toleo la 2013 na vigezo vya Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), unapendekeza uwiano sahihi katika madarasa ya awali ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 25 (1:25).
Ukilinganisha na uwiano uliopo katika madarasa mbalimbali ya awali nchini, bado haukidhi matakwa ya TAMISEMI na uwezekano wa wanafunzi kukosa maarifa ya msingi kuwaandaa kuingia elimu ya msingi ni mkubwa.
Pia takwimu za TAMISEMI na kuchapishwa kwenye kitabu cha Takwimu za Mwaka 2016 (Tanzania in Figures 2016) ambazo zimetolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) zinaeleza kuwa mwaka 2016 pekee madarasa ya awali nchi nzima yalikuwa na walimu 14,958 lakini waliokuwa na sifa za kufundisha ni 11,920 sawa na asilimia 79.7.
Zinaeleza zaidi kuwa uwiano wa mwalimu (kwa walimu wenye sifa) kwa wanafunzi kwa mwaka huo ulikuwa 1:131 ambapo ni mara 5 zaidi ya uwiano unaotakiwa wa 1:25.
Maoni ya Wadau
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la HakiElimu, Dk. John Kallage wakati akitoa mapendekezo ya shirika kuhusu bajeti ya elimu ya mwaka wa fedha wa 2018/2019 alisema serikali inapaswa kuweka kipaombele katika utatuzi wa matatizo sugu katika sekta ya elimu ikiwemo suala la ajira za walimu katika madarasa ya awali.
“Kutenga na kuongeza bajeti kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika sekta ya elimu na hasa fedha zinazokwenda TAMISEMI kwa ajili ya elimu msingi. Kutenga bajeti yenye uhalisia wa kutatua changamoto sugu na muda mrefu za miundombinu mashuleni na kuweka kipaumbele katika suala la ajira za walimu,” alisema Dk. Kallage.
Serikali imeshauriwa kuanzisha mpango wa kutoa ruzuku kwa wanafunzi wa madarasa ya awali kama ilivyo kwa shule za msingi na sekondari ili kuboresha ustawi wa elimu ya watoto nchini.
Kwa upande wake, Mwandishi wa Vitabu na Mwanaharakati wa masuala ya Watoto, Richard Mabala amesema licha ya kuongeza idadi ya walimu katika madarasa ya awali, wanafunzi wapewe ulinzi na elimu bora itakayowakomboa fikra na maisha yao.
“Mimi naamini suala kubwa elimu bure, pili ulinzi kwasababu mimi kama mzazi nikijua shuleni wasichana wanatongozwa, wanatishiwa kubakwa na njiani hakuna ulinzi. Kwahiyo kuwe na ulinzi wa kutosha kuhakikisha watoto wako salama,” amesema.
Msimamo wa Serikali
Serikali kupitia Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako imesema inaendelea na jitihada za kuboresha elimu ya awali kwa kujenga madarasa, kuajiri walimu na kuhakikisha vifaa vya kujifunzia na kufundishia vinakuwepo mashuleni.
Akisoma bajeti ya elimu jana, Prof. Ndalichako alisema, “Katika kusimamia Elimu ya Msingi na Sekondari, katika mwaka 2018/19 Wizara itatekeleza yafuatayo: itaandaa Mwongozo wa Kitaifa wa uendeshaji wa Elimu ya Awali unaozingatia viwango. Lengo la Mwongozo huo ni kufafanua viwango vya Elimu ya Awali kwani kwa sasa kuna mifumo mingi ambayo inahitaji uratibu wa karibu kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi hao kusoma katika mazingira tulivu na salama yenye kusaidia kuinua ubora wa elimu na mafunzo.”