KIJIJI cha Mkongoro kama ilivyo katika vijiji vingine Wilayani Kigoma wakazi wake ni wakulima, ambao kilimo chao ni mazao ya chakula na biashara yakiwemo Kahawa, Nanasi na Migomba.
Kijiji hiki kina jumla ya wakazi 8,965, kati ya wakazi 18,656 wa Kata ya Mkongoro ambao 8,859 kati ya wakazi hao ni wanaume na 9,797 wakiwa wanawake.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji, Alfred Ibrahim Ntaguzwa anasema asilimia 50 ya vijana kijijini kwake, ndio wanaojishughulisha na kilimo kwa kupewa maeneo ya kulima na wazazi wao au pengine kwa kukodi ardhi kwa ajili ya kilimo cha bustani.
Asilimia nyingine 50 hawana kabisa ardhi ya kulima hivyo huamua kukimbilia mijini kutafuta shughuli nyingine ya kujikimu katika maisha yao.
Kulingana na mwenyekiti wa serikali ya kijiji, ukosefu wa ardhi kwa ajili ya kilimo ni moja ya sababu ambazo zinapelekea vijana wengi kukimbilia mijini.
Vijana wa Mkongoro hawatofautiani na mwenyekiti wao, lakini wanaongeza kuwa gharama za kilimo zimekuwa kubwa kupita kiasi.
“Kilimo cha sasa hivi hapa kwetu kimepanda juu. Maeneo ya kulima hakuna kwa sababu hapo nyuma watu walikuwa wachache sana, na maeneo yanayopatikana ni machache kulingana na eneo la kijiji,”alisema Amri Yasini.”
Alisema kuwa wazee waliotangulia kijijini hapo ndio wanaomiliki maeneo makubwa ya ardhi na kwamba ili vijana waweze kupata eneo la kulima wanahitaji kulipa fedha nyingi kuliko uwezo wao kwa ajili ya kukodi.
Kijana wa Mkongoro anatakiwa kulipa kiasi kisichopungua 100,000, ili kupata ardhi kwa ajili ya kilimo kutoka kwa watu walio na maeneo ya ardhi kijijini kwao.
Kilimo cha zao la Nanasi ni kilimo ambacho kinaweza kumkomboa kijana wa kijiji cha Mkongoro. Ni kilimo cha muda mrefu katika kijiji hicho na vijana wengi wa kijiji hicho wamekuwa wakitegemea zao hilo kujipatia kipato, lakini bado hata hivyo hakijaweza kuwakomboa vijana, ziko sababu mbali mbali.
“Kilimo cha Nanasi kimeshindwa kutukomboa. Unaweza kutumia gharama kubwa kulima nanasi, lakini kuuza unauza bei ya sawa na bure na wakati mwingine nanasi zinaozea shamba kwa kukosa soko la uhakika la kuuza nanasi kwa bei nzuri,”aliongeza Bw.Yasini.
Mwenyekiti waserikali ya kijiji cha Mkongoro, Alfred Ibrahim Ntaguzwa, anasema suala la masoko linaweza kupungua baada ya ofisa ushirika kuwapatia elimu ya kuanzisha chama cha ushirika wa wakulima wa nanasi.
Tatizo la masoko kwa wakulima katika kijiji cha Mkongoro pia linachangiwa kwa kiasi kikubwa ukosefu wa mawasiliano. Hakuna mtandao wowote wa simu katika kijiji hicho.
“Hapa hakuna mtandao wowote wa simu. Kama tungekuwa na mawasiliano simu zingesaidia kutafuta soko la mazao yetu, lakini hilo haliwezekani na Nanasi zinaozea shambani,”alisema Kimazi Hamad kijana anaelima Nanasi katika kijiji cha Mkongoro.
Tungilayo Jafari ni mmoja wa vijana ambao wamekuwa wakilima nanasi; alisema kuwa miundombinu ya kulima kwa kutumia jembe la mkono ndio inayosababisha vijana wengi kutopata ukombozi wa kilimo cha nanasi na kujikuta wengi wao wakikimbilia mijini na kwamba hata kama vijana wangepewa maeneo ya kulima tija haiwezi kupatikana kama hakuna miundombinu bora ya kulimia; mitaji pia ni tatizo.
“Ukitathimini kwenye mikoa mingine wanatumia trekta, lakini kwa sisi hapa Kigoma hususani ukanda wetu huu wa Kigoma Kaskazini, hatujawahi kuona trekta hata moja. Ndio maana unakuta sisi vijana tunashindwa kutumia kilimo cha jembe la mkono na kukimbilia mjini kuuza maji kidogo labda tunaweza tukapata wepesi wa kushika hela,”alisema Bw.Tungilayo Jafari.
Alisema hata wale vijana ambao wanabaki kijijini, wengi wao hawana shughuli ya kufanya na kwamba kinachowasaidia kidogo ni uwepo wa barabara ya kiwango cha lami inayotoka mjini Kigoma na kupita kijijini hapo kwenda Manyovu, kwa kuwa wafanyabiashara kutoka mjini hufika kijijini kwao kununua mazao na wao wanakuwa wabebaji wa hiyo mizigo kuweka kwenye gari.
“Tuko vijana wengi ambao tunaamkia kijiweni,lakini kwa kuwa wameshatutengenezea barabara ya lami, watu wa mjini hapa wako wengi wanaokuja kulangua biashara, kwa hiyo tunaponyanyua mizigo yao ndio tunapata hela kidogo, wale wanaoshindwa wanakimbilia mjini. Ndio maisha tuliyonayo vijana hapa kijijini.”
Mzee Ramadhani Abeid ni mmoja wa wazee wakazi wa kijiji cha Mkongoro. Anasema wanao vijana wanaopenda kilimo isipokuwa ajira ya kilimo ni ngumu. Na wengine wanajikita kwenye mambo ya sanaa na kwamba wanaokimbilia mijini ni wale wanaopenda mambo ya muziki.
“Kama kweli serikali ingetujali hapa kwetu kijijini mambo yasingekuwa mabaya, nafikiri ni kijiji cha kwanza kwa kuzalisha nanasi,”aliema Mzee Ramadhani.
Thobiasi Misuzi ambaye ni afisa ughani anaeshughulikia masuala ya kilimo na zao la Kahawa katika Kata ya Kalinzi Wilayani Kigoma ambako Kahawa na Migomba inastawi kwa wingi. Anasema tatizo la vijana kukosa ardhi kwa ajili ya kilimo linatokana na serikali za vijiji kutojua umuhimu wa vijana kwa kutowamilikisha vijana ardhi na ndio chanzo cha vijana kukimbilia mijini.
“Serikali za vijiji hawatengenezi mipango ya kuwamilikisha vijana ardhi, kwa sababu ardhi ndio rasilimali ya kwanza katika shughuli yoyote ya maendeleo, kwa hiyo mtu yeyote anapokuwa hana ardhi hiyo ni chanzo cha umasikini na ndio maana vijana huamua kuondoka vijijini,”alisema Bw.Misuzi.
Anaongeza kuwa kitu kingine katika kilimo kinachoongeza uzalishaji ni pamoja na masoko. “Ukiangalia watu wanaolima maeneo kama Dodoma, Morogoro; kule kuna soko la moja kwa moja kwa sababu wanunuzi kutoka Dar es Salaam hununua mazao sehemu hizo.Hali hiyo ni tofauti katika vijiji vingi mkoani Kigoma.”
Nae Michael William Mbago, mwenyekiti wa mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA), wilaya ya Kigoma anasema kilimo hakina tija na hakijawekewa mazingira ambayo yatamshawishi kijana afurahie kilimo.
“Vijana wengi wanakimbilia mjini kwa kuwa wamekuwa wakiona kuwa kilimo ni adhabu kwa sababu kilimo hakina tija,”alisema Bw.Mbago.
Aliongeza kuwa tatizo lingine ni kwamba serikali ya kijiji haijatoa dira nzuri jinsi ya kuwaboresha vijana kwa kuwatengea maeneo ya kulima.
Nae Kimazi Ahmad anasema ameanza kilimo cha nanasi mwaka 1999, lakini mpaka sasa ameshindwa kununua hata piki piki, lakini vijana waliotoka vijijini kwenda mijini wanazo piki piki na ndio maana vijana wanakimbilia mijini na kilimo kinakosa mwenyewe.
Hivi karibuni serikali imetoa hati za kimila kwa baadhi ya wakazi wa kijiji cha Mkongoro suala ambalo lingewasaidia wakulima kupata mikopo kwa ajili ya kuboresha kilimo chao, lakini Sheikh wa kijiji cha Mkongoro Sheikh Kidana Haruna anasema hati miliki za kimila ni kama usanii kwani benki hazitambui hati miliki za kimila na hivyo kutowakopesha wakulima.
“Hati miliki ziboreshwe kwa mfumo wa kibenki na kwa riba nafuu hapo ndipo wakulima watajitahidi na hakuna kijana atakaekimbilia mjini kwa kijana anakwenda mjini kwa kukosa jinsi ya kufanya,”alisema.
Nini kifanyike?
Thobiasi Misuzi, ambaye ni afisa ugani anaeshughulikia masuala ya kilimo na zao la kahawa katika Kata ya Kalinzi Wilayani Kigoma, anasema kuwa mipango ya serikali kuhusu vijana ianzie chini kabisa. Kuwe na mipango iliyoandaliwa kwa vijana kabla na baada ya kumaliza shule kuwawezesha kujiajiri katika kilimo.
Serikali imeanzisha benki ya kilimo kusaidia sekta ya kilimo na kuwawezesha wakulima kupata benki ambako wataweza kupata mikopo kwa uhakika na urahisi zaidi, lakini Sheikh Haruna anashauri kuwa benki hiyo iendane na hati za kimila ili wenye hati hizo waweze kunufaika.
Mwaka jana ofisi ya taifa ya takwimu ilitoa matokeo ya utafiti wa mapato na matumizi ya kaya binafsi Tanzania bara kwa mwaka 2011/2012.
Utafiti huo unaonesha hali ya umasikini kwa wananchi vijijini bado ni mbaya sana na hiyo inatokana na wengi wao kuwa wakulima na hivyo ni wazi kwamba kilimo hakijawasaidia kuboresha maisha yao.
Maeneo ya vijijini umasikini bado upo kwa kiwango kikubwa ambapo asilimia 84.1 ya watanzania vijijini ni masikini ukilinganisha na asilimia 14.4 ya wale waishio mijini huku kama Dar es salaam ni asilimia 1.5.
Hiyo inaonyesha uhalisia kwamba kilimo hususan kwa wakulima wadogo bado kina changamoto kubwa hivyo ujio wa benki hiyo unapaswa kuwa hamasa ya kuinua wakulima kupitia vikundi vya kuweka na kukopa vya wakulima.
Bila shaka matarajio ya wananchi wakulima ni kuona benki hiyo inatoa huduma kwa walengwa kwani hatua ya serikali kuiwezesha benki hiyo mtaji wa shilingi bilioni 100 ndio ilifanya shirika la kilimo na chakula ulimwenguni (FAO), kuahidi kuisaidia nchi kuanzisha benki hiyo.
Aidha sera ya maendeleo ya vijana ya mwaka 2007 itekelezwe kwa vitendo hasa sura ya nne ya sera hiyo ambapo malengo 13 yameainishwa ikiwemo kuwa na mipango mizuri ya ajira ambayo itawasaidia vijana kutatua matatizo yao ya ukosefu wa ajira na kuwawezesha kujitegemea kiuchumi.
Kubainisha mahali vijana walipo, idadi yao shughuli, zao na mahitaji ili kuweza kutumia takwimu hizo katika upangaji wa shughuli za maendeleo yao.
Kulingana naTakwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, idadi ya watu wanaoishi Mijini imeongezeka zaidi ya mara tano kutoka asilimia 6.4 mwaka 1967 hadi kufikia asilimia 29.6 kwa mwaka 2012.
Jiji la Dar es Salaam pekee lina asilimia 10% ya watu wote hapa Tanzania Bara wakati Mjini Magharibi ina asilimia 46 ya watu wote wa Zanzibar.
Aidha takwimu hizo zinaonesha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam una asilimia kubwa ya Vijana wenye umri wa miaka 15-35.
Nazo takwimu za Shirika la Maendeleo ya Makazi ya Watu la Umoja wa Mataifa, (UN Habitat), iliyotolewa mjini Bamako, Mali hivi karibuni, inabainisha kwamba, katika kipindi cha miaka arobaini kuanzia sasa, idadi ya watu wanaoishi mijini itaongezeka maradufu Barani Afrika, hali ambayo itasababisha kutokuwepo na uwiano mzuri katika ekolojia.
Watu waliojazana katika maeneo ya mijini wengi wao wakiwa ni vijana, wanatoka katika maeneo ya vijijini ambako kama inavyofahamika ajira kubwa huko ni kilimo, lakini hata hivyo ushriki wao katika kilimo unaendelea kupungua.
Kimsingi vijana wanaamini kwamba kila kitu kipo mjini, akienda mjini atatoka, lakini tunaweza kujifunza jambo moja, miundombinu lazima iwepo vijana kubaki vijijini kuzalisha kwa tija, kujiinua kiuchumi hali ambayo itawafanya wajione kwamba wameyapatia maisha.