MAMLAKA ya Maji Safi na Maji taka ya Manispaa ya Bukoba(Buwasa)haitoi huduma zake kwa kwa siku nne mfululizo baada ya Shirika la umeme (Tanesco) kuikatia umeme na mitambo ya kusukuma maji kushindwa kufanya kazi.
Hali hiyo pia inahatarisha maisha ya wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya Mkoa wa Kagera ambapo gari la kikosi cha zimamoto na uokoaji limelazimika kutumika kusomba maji kutoka ziwa Victoria kwa ajili ya matumizi wa hospitali hiyo.
Baada ya hali kuwa mbaya hospitalini hapo kutokana na kukosekana kwa maji Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Nassoro Mnambila aliingilia kati na kuonekana mara kwa mara hospitalini hapo akifuatilia zoezi la usombaji wa maji.
Kufuatia kuwepo kwa tatizo hilo wakazi wengi wa mji wa Bukoba wanafuata huduma ya maji ziwa Victoria,huku wengine wakitumia maji ya mito inayopita maeneo ya mji huu hali inayoweza kuchangia magonjwa ya mlipuko.
Mkurugenzi wa Buwasa Chaggaka Kalimbia alikiri mamlaka hiyo kudaiwa kiasi cha shilingi milioni 30 na kuwa hawawezi kutoa huduma ya maji baada ya kukatiwa umeme na Tanesco na kuwa hawana fedha za kulipa kwa sasa.
“Tanesco wamenikatia umeme,ela sina na uwezo sina tunadaiwa milioni thelathini na sina mahali pa kuzipata…hivi sasa niko safari lakini kuna majadiliano yanayoendelea kati yetu,.ofisi ya Mkuu wa mkoa na Tanesco”aliiambia Mwananchi kwa njia ya simu
Naye Meneja wa Tanesco Mkoa wa Kagera Athanasius Nangali alisema walipata taarifa kuwa Mamlaka hiyo ilishapewa fedha kutoka serikalini na kuwa wanatakiwa kuwalipa deni lao alilosema ni kubwa sana.
Pia alisema kuwa zoezi la kuwakatia umeme wadaiwa wao sugu linaendelea takribani mikoa yote na kuwa zoezi hilo ni maagizo ya wizara na mwisho wa adha hiyo kwa wakazi wa Bukoba haijulikani.
Na. Phineas Bashaya
Mwisho