VITUKO katika sherehe za miaka 50 ya Uhuru mkoani Mwanza

Jamii Africa

MAADHIMISHO ya miaka 50 ya Uhuru Tanganyika (Tanzania Bara?) ngazi ya mkoa wa Mwanza yaliingia dosari baada ya idadi kubwa ya wananchi wa kawaida, watendaji wa Halmashauri na Wilaya pamoja na  viongozi wa vyama vya upinzani ngazi za wilaya na mkoa kupuuza kujitokeza kwa wingi uwanjani; hatua ambayo ilisababisha Mweka Hazina (DT) wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Paul Ntinika aamue kuokoa jahazi kwa kujitokeza kuimba shairi.

Mweka Hazina huyo, alianza kuimba shairi lake majira ya saa 5:10 asubuhi; hali iliyosababisha mgeni rasmi pamoja na viongozi wachache waliokuwa wameketi meza kuu waanze kujitokeza kwa kumpatia zawadi za fedha.

Pamoja na maudhui mengine, shairi la Mweka Hazina huyo lilizungumzia maana ya uhuru na maadhimisho, mafanikio pamoja na wajibu wa Watanzania hasa wakati Taifa likitimiza miaka 50 ya Uhuru.

Mwandishi wa habari hizi alihudhuria kwenye sherehe hizo ambazo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Said Amanzi.

Hata hivyo, Amanzi alikuwa amemwakilisha Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Mhandisi Evarist Ndikilo.

Viongozi wengine waliojitokeza kuhudhuria kwenye maadhimisho hayo ni Kamanda  wa Polisi wa  mkoa, Liberatus Barlow ambaye alikuwa amefuatana na askari Polisi wenye vyeo tofauti tofauti wasiopungua 20; huwenda kwa ajili ya kuimalisha ulinzi na usalama uwanjani hapo.

Mkurugenzi Mtendaji wa  Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Dr Leonard Masale pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Colnel Ngudungi pekee ndio walihudhuria kwenye maadhimisho hayo. Baadhi ya Wakurugenzi ama waliwakilishwa au hawakuhudhuria kabisa.

Katika hatua  nyingine, sherehe hizo zilizofanyika katika uwanja wa Nyamagana, zilidumu kwa takribani saa moja.

Madhimisho hayo yalianza rasmi majira ya saa tano asubuhi, baada ya kuwasili aliyekuwa  mgeni rasmi na kufikia tamati muda wa saa 5:50 asubuhi baada ya mgeni rasmi kuondoka eneo la tukio.

Habari hii imeandikwa na Juma Ng’oko – Mwanza

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *