Tunaishi katika ulimwengu unaokabiliwa na athari kubwa za mabadiliko ya hali ya hewa. Moja ya athari hizo ni kuongezeka kwa joto na kupungua kwa mvua katika maeneo mbalimbali. Athari hizi zinagusa moja kwa moja afya ya binadamu.
Ripoti ya mabadiliko ya hali ya hewa ya mwaka 2017 imeonesha kuwa kuongezeka kwa joto kunaathiri afya ya binadamu kwa kiasi kikubwa. Ripoti hiyo inatoka kundi la vyuo mbalimbali na mashirika tofauti ya Umoja wa Mataifa inasema watu wengi wanaathirika na joto pamoja na mlo hafifu sambamba na kusambaa kwa magonjwa.
Moja ya kisababishi cha mabadiliko ya hali ya hewa ni uchafuzi wa anga. Uchafuzi wa anga ni kuchanganyika kwa hewa asili katika anga na vitu kama vile moshi, majivu, gesi za kemikali katika hali na kiwango ambacho huathiri sifa ya hewa na kusababisha madhara kwa binadamu na viumbe vingine.
Baadhi ya vitu na vitendo huathiri vibaya anga letu. Baadhi ya vitu hivyo ni kama gesi na moshi unaotoka kwenye viwanda, moshi kutoka kwenye magari, marashi, dawa ya kuuwa wadudu shambani na kadhalika.
Lakini umewahi kujiuliza kuwa aina ya chakula unachokula kinaweza kukusaidia kukabiliana na athari za kiafya zinazotokana na uchafuzi wa hewa?
Wanasayansi katika utafiti wao uliotolewa hivi karibuni, wanaeleza ulaji wa chakula cha Mediterania ( Mediterranean diet) chenye matunda mengi, mbogamboga, nafaka isiyokobolewa, samaki, maharage jamii ya soya, mafuta ya mizeituni na mayai yanaweza kuwalinda watu dhidi ya athari za afya zinazotokana na uchafuzi wa hewa.
Wanasayansi hao kutoka Shule kuu ya Udaktari ya NYU ya Marekani, walichambua data za watu takribani 550,000 wenye wastani wa umri wa miaka 62 kwa miaka zaidi ya 17 ambapo waliwapanga watu hao kwenye makundi kulingana na ulaji wao unaoendana na chakula cha Mediterania na kulinganisha na muda waliokaa kwenye hewa iliyochafuliwa.
Walibaini kuwa watu ambao walizingatia kula vyakula vilivyotajwa hapo juu walikuwa na uwezekano mkubwa wa kuepuka magonjwa na vifo vinavyotokana na uchafuzi wa hali ya hewa. Magonjwa hayo ni yale ya mfumo wa upumuaji, moyo na kansa.
Vyakula jamii ya Mediterania
Vyakula hivyo jamii ya Mediterania vina uwezo mkubwa wa kukabiliana na vimelea vya maambukizi ya magonjwa kwa mtu ambaye atazingatia kwa usahihi kutumia katika maisha yake.
“Uchafuzi wa hewa unasababisha athari mbaya za kiafya kupitia hewa ukaa na mlo wa Mediterania una virutubisho muhimu kupambana na vimelea vya magonjwa,” anasema Mwandishi Mtafiti wa utafiti huo, Chris Lim wa Chuo cha NYU.
Lim anasema vyakula vya aina nyingine vinaweza kusaidia kukabiliana na athari hiyo. “Nilipoangalia kila mchanganyiko wa chakula cha Mediterania, kina matunda, mbogamboga na mafuta yanayoweza kupambana na athari za hewa chafu,” anasema.
Utafiti kuhusu ulaji kama unaweza kuzuia athari za kiafya za uchafuzi wa hewa bado haujahakikiwa na kukubalika kisayansi. Lakini utafiti huo sio wa kwanza kutafuta uhusiano wa mlo na athari za kiafya za uchafuzi wa hali ya hewa.
Wakala wa Uhifadhi wa Mazingira wa Marekani (U.S. Environmental Protection Agency (EPA)) unatafiti kama mlo unaweza kumlinda mtu dhidi ya athari za uchafuzi wa mazingira. Pia wanatafiti ili kujiridhisha kama virutubisho hivyo vinaweza kutumika badala ya dawa za kitabibu na kwa kiasi gani mtu anatakiwa apate virutubisho hivyo kumhakikishia usalama dhidi ya uchafuzi huo.
Hata hivyo, bado watu wanashauriwa kutumia zaidi matunda na mbogamboga kwenye milo yao ya kila siku ili kupata faida mbalimbali za kiafya.