Wachezaji wetu na upeo mdogo wa soka

Jamii Africa

“Yanga wakija na dau zuri, nitajiunga nao tu. Mimi nacheza kwa kutafuta maslahi, sijali nachezea wapi”  ni kauli iliyoanza kuzoeleka sana miongoni mwa wachezaji kadhaa wa soka Tanzania ikiwa ni  kudhihirisha na kuwakilisha upeo mdogo walionao wachezaji wetu.

Kabla sijaingia ndani kusema kwa nini naiona kauli hiyo kuwa imetolewa na watu wasio na upeo wa kutosha, naomba kwa ufupi sana nieleze kuhusu matendo kadhaa yaliyowahi kuthibitisha upeo mdogo wa wacheza soka wa nchi hii.

Wachezaji wetu, wanaotafuta kufikia viwango vya kukubalika kimataifa, walishawahi mara kadhaa kucheza ovyo ili viongozi wao waliowakera waonekane hawafai na waondolewe madarakani wakati kwa kufanya hivyo walioonekana hawafai ni wao kwani wengi hawakuijua njama hiyo bali waliona tu kwamba wachezaji hao wamekwisha kisoka!

Walishavurunda makusudi kupinga mshahara mkubwa aliolipwa kocha mwenye wasifu mkubwa kimataifa kama Trott Moloto wa Afrika Kusini dhidi ya mishahara yao midogo bila kujali kuwa yule ni mtaalaam wa kuwatengenezea maisha yao ya hali ya juu ya baadaye!

Wenzao Ulaya, wachezaji wenye mishahara midogo sana ikilinganishwa na ya nyota wao fulani kwenye timu, huushinikiza uongozi wa timu umlipe nyota huyo mshahara mkubwa zaidi kama anavyodai ili wabaki naye kutokana na kuyajali mafanikio ya timu na yao binafsi kwa sababu kuwa na nyota huyo, kunasaidia nao kung’ara kwa mipira mizuri anayowatengenezea uwanjani.

Kwetu, mshahara wa kocha umevuruga kiwango cha timu! Ni wachezaji wetu hawa waliowahi kugomea kambi ya mazoezi kwa madai kwa uongozi wa klabu yao wakati mazoezi hayo ni kwa faida yao, familia zao, ndugu zao na kwa ujumla wote kwa maisha yao.

Yote yaliyozungumzwa hapa, hayakufanywa na Nonda Shaaban “Papii” alipokuwa Yanga ingawa kwenye kipindi hicho migomo migomo ya aina hiyo ilijitokeza tokeza klabuni hapo na ndiyo maana hivi sasa, mchezaji huyo yuko mbali kimaisha.

Upeo mdogo mwingine wa wachezaji wetu ulidhihirika pale mchezaji mkubwa Victor Costa alipoelezewa kwenye vyombo vya habari kukataa ushauri wa nadaktari wa yeye kufanyiwa upasuaji wa mguu, tiba ambayo ina umuhimu mkubwa katika maisha yake ya soka, ikizingatiwa kuwa bado ana safari ndefu katika mchezo huo.

Miongoni mwa watu walioshangazwa na kusikitishwa sana na uamuzi huo wa Costa ni mtu mwenye uchungu wa dhati wa soka la nchi hii,Erick David Nampesya wa BBC.

Mdau huyo, alisikitishwa na uamuzi huo akiuweka kwenye upande wa pili wa uamuzi wa mchezaji Daniel Agger wa Liverpool  ya Uingereza aliyefurahia ushauri kama huo aliopewa na madaktari siku hizo hizo ambazo Victor Costa alishauriwa na kukataa ambapo naye alishauriwa hivyo baada ya kuanza kucheza akitoka kwenye kuuguza mguu.

Ukiitafakari mifano yote hiyo ya upeo mdogo wa wachezaji wetu, utaona kuwa huwa hawaangalii mbali kuhusu maisha yao kisoka na hivyo, maisha yao kwa ujumla.

Nikija kwenye sababu iliyofanya niamini waliotoa kauli niliyoanzia makala haya ni wachezaji wa Simba wenye upeo mdogo, swali la kujiuliza, kwa nini Yanga na si Mtibwa, Moro United, Toto African au Prisons?

Kwa nini waelekeze kauli zao moja kwa moja kwa Yanga wakati timu nyingine zinaweza kuwapa mkataba mnono zaidi ya Yanga? Hili lina majibu mawili: Kwanza, wanaona Yanga na Simba ndiyo kilele chao.

Wachambuzi wa soka kwenye vyombo vya habari kama kina Edo Kumwembe watamaliza maneno yote kuwapa ushauri wa nini cha kufanya kuwafikisha alikofika Nonda Shaaban lakini wanajisumbua tu kwani wenzao tayari wako kileleni Simba na wakitoka hapo basi waende kwenye kilele cha pili Yanga, mchezo unaisha.

Kwa maana hiyo, kwenda Prisons na kupata ajira ya kudumu ndani ya Jeshi la Magereza  au kwenda Polisi Dodoma na kupata ajira ya kudumu ndani ya Jeshi la Polisi.

Jibu la pili ni kwa wachezaji hao kutumia kauli hiyo kama njia ya kuongezewa dau na uongozi wa Simba ili wabaki klabuni hapo. Wakisema wako tayari kwenda timu yoyote itakayowaahidi donge nono bila kutaja Yanga, viongozi wa Simba hawatarushwa roho sana.

Kwa hiyo wanaitaja Yanga ili kupandisha dau hapo Simba walipo. Kama wangekuwa na upeo mzuri, ambacho wangefanya ni kuzungumza na uongozi wa Simba kwa kuwaambia: “Wazee, nadhani mmeiona kazi yangu nzuri kwenye msimu huu, kwa hiyo bila kiasi fulani cha pesa, naweza kufanya mazungumzo na wengine watakaonihitaji kwa kiasi hicho”.

Matokeo ya mazungumzo yatakayofuata yatakuwa ama mchezaji huyo abaki kwa malipo yatakayokubaliwa au akajaribu kwingine baada ya kushindwa kukubaliana lakini haipendezi kwa soka la kisasa kukimbilia kwenye vyombo vya habari moja kwa moja na kusema “Yanga njooni”.

Hii inaathari kithamani ya mchezaji hata huko Yanga anakojinadi kwa sababu Simba wanaweza kuachana naye na akakosa uchaguzi na hivyo Yanga kumchukua kwa bei ndogo kwani chema chajiuza, kibaya chajitembeza.

Kwa wadogo zangu wa Prisons mlio na ajira za kudumu ndani ya Jeshi la Magereza, tafakarini sana kabla ya kushawishika kwenda Yanga au Simba kwa dau kubwa la mara moja la usajili.

Kumbukeni yaliyowakuta Herry Morris na Primus Kasonso. Waliokuwa wakiwawekea pingamizi wasihame, hadi kuwachukulia hatua za kijeshi waliyajali sana maisha yao. Hebu tafakarini sana kabla ya kuamua.

Katika dunia ya sasa, wachezaji wetu jaribuni kuishi maisha kama wanayoishi wenzenu wa Ulaya kimaamuzi. Kuzidiwa kwa mbali viwango vya soka, kusiwe sababu ya kutofautiana kwa mbali kiupeo. Tafadhali jirekebisheni kabla hamjawakatisha tamaa wadau wa soka wa nchi hii wanaowapenda kwa dhati.

9 Comments
  • Tatizo la YANGA ni kuajiri makocha wa kigeni na kuwapa madaraka makubwa ya kusajili anachoangalia ni maslahi yake binafsi na siyo tija.kama kocha anaulizwa na uongozi atoe taarifa ya usajili na yeye kuamua kujiondoa hauoni kuwa hapo kuna jambo?.

  • Ni kweli hilo pia linadhihirishwa na mchezaji fulani wa Simba aliyekuwa akisakata soka Sweden akidhubutu kuacha kuendelea na ajira yake kwa madai anakatwa kodi kubwa katika mshahara wake kitu ambacho si kweli kwani fungu hilo lingerudi pindi mkataba unapoisha. Je,wataweza kufika walipo kina Etoo,Drogba,etc.

    • nikweli nduguyangu hudanganywa na watu ambao maisha yao yashatoka yeye ndio kwanza anajenga maisha yake hukubali kudanganywa achilia nidhamu ndogo hata upeo wa akili ni mdogo jambo ambalo hawalioni nikwamba hawajali heshima yao kama pua inavyotizama chini huangalia maslshi ya wakati ule tu NO FUTURE.

  • Ni kweli kabisa ,umeeleza mambo ya msingi, hasa ukizingatia tupo katika wakati muafaka,na kama mwanahabari na mzalendo ,umenitimiza wajibu wako hongera kaka,tatizo ni wachezaji wetu wengi hawajitambui, na hii imetokana na kutokuwa na msingi mzuri ili kujua thamani zao ndio maana mpk leo bado wanaishi maisha ya kitumwa mwingine yuko tayari akaue kiwango kwa kukaa benchi yanga au simba kuliko kucheza akiwa Mtibwa, Hatufiki kwa staili hii.

  • Ni kweli kabisa ,kama viongozi wa TFF wangekuwa na upeo wangewafungulia ofsi wachambuzi hawa kama Edo kumwembe na wenzake na kulipa mishara waachane na shughuli nyingine wabaki kuwashauri wachezaji wetu wawe na upeo mpana hata baadhi ya viongozi wa TFF na VILABU vyetu

  • Tatizo la wanasokawengi tulionao hapa kwetu ni kwamba, akianza kusifiwa kidogo tu kwa mafanikio yake aliyopata naye anavimba kichwa na kujiona hakuna wa kumfikia. Hii ni moja ya sababu kubwa zinazofanya wanasoka wetu kushindwa kufikia viwango vya kimataifa kama wenzetu wa Afrika Magharibi, Kaskazini na hata Ulaya. Kwa kifupi vitendo vya namna hiyo ni utovu wa nidhamu maana wanakuwa hawaambiliki/hawashauriki.

  • Mastaa wa kibongo ni ngumu sana ku behave kama profesiona na ukizingatia hawakusoma na hakuna wanachotegemea maishani..

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *