Wanafunzi wanasoma kwa kugeuziana migongo Ruvuma

Jamii Africa

WANAFUNZI 201 kuanzia darasa la tatu hadi la sita  katika shule ya msingi Kidugalo kata ya Rwinga wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wanasoma katika vyumba viwili vya madarasa kwa kugeuziana migongo hali ambayo inachangia kushusha taaluma katika shule hiyo.

Wanafunzi wa darasa la tatu na la nne katika shule ya msingi Kidugalo kata ya Rwinga Namtumbo mjini mkoani Ruvuma wakisoma katika chumba kimoja kwa kugeuziana migongo

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Owini Mpangala alibainisha kuwa  wanafunzi 51 wa darasa la tatu na wanafunzi 56 wa darasa la nne wanasoma katika chumba kimoja kwa kugeuziana migongo na wanafunzi 62 wa darasa la tano na wanafunzi 32 wa darasa la sita wanasoma katika chumba kimoja kwa kugeuziana migongo.

“Madarasa mawili kusomea katika chumba kimoja kunasababisha kila darasa kufundishwa vipindi vinne tu kati ya vipindi nane vinavyotakiwa kufundishwa kwa siku,walimu wawili hawawezi kuingia kwa wakati mmoja kufundisha kwenye chumba kimoja,vipindi vinne vinapotea  darasa halifundishiki’’,alisisitiza.

Kwa mujibu wa mwalimu Mpangala shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007 yenye wanafunzi 453 ina vyumba vinne tu vya madarasa kati ya mahitaji ya vyumba nane na kwamba shule hiyo haina ofisi ya walimu hali ambayo inasababisha mwalimu mkuu na walimu kutumia ofisi moja ambayo hata hivyo haitoshi kutokana na idadi ya walimu 13 waliopo katika shule hiyo.

Kutokana na hali hiyo baadhi ya walimu wanakaa nje ya ofisi wakati wa kiangazi huku wakiendelea kufanyakazi za kusahihisha madaftari ya wanafunzi wakipigwa na jua hali ambayo inaleta kero kubwa kwa walimu na wanafunzi.

Mkuu wa shule hiyo alisema amechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na matatizo hayo ikiwa ni pamoja na kuyapeleka katika kamati ya shule na Baraza la madiwani ambayo wameahidi katika msimu ujao wa fedha wanatarajia kulipatia kipaumbele hasa kero ya upungufu wa vyumba vya madarasa,samani na ofisi ya walimu.

“Hapa kwangu uongozi wa serikali ya kijiji umekataa kujenga vibanda vya nyasi kama ilivyo katika shule nyingine kwa madai kuwa hapa ni mjini hawawezi kujenga vibanda vya nyasi ni aibu,wamefyatua tofali zipo kwenye tanuri’’,alisema.

Baadhi ya walimu wanaofundisha katika shule hiyo wamesema wanatamani kuacha kazi au kuhama katika shule hiyo kutokana na changamoto nyingi ambazo hazijapatiwa ufumbuzi kwa muda mrefu na kuchangia kushusha elimu katika shule hiyo ambayo ipo mjini.

Mratibu elimu kata ya Rwinga Thomas Komba amekiri shule za msingi katika kata yake inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo shule ya msingi Kidugalo ambapo hivi sasa uhamasishaji unafanyika ili kumaliza kero ya upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa.

Baadhi ya walimu katika shule ya msingi Kidugalo wakisahihisha madaftari ya wanafunzi nje baada ya shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007 kukosa ofisi ya walimu

Aliongeza kuwa wananchi wa eneo la Kidugalo mwaka jana wamefyatua na kuchoma tofali kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na kwamba hivi sasa kinachosubiriwa ni nguvu toka serikalini kutoa vifaa vya kiwandani ili kuweza kufanikisha kupunguza kero hiyo ya muda mrefu.

Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo ina shule za msingi 107 kati ya hizo shule 105 zinamilikiwa na serikali na shule mbili ni za watu binafsi na mashirika ya dini.

Imeandaliwa na Albano Midelo,Namtumbo

7 Comments
  • Ingependeza sana kama Waandishi wa Habari na Wanajamii wangeacha kuimba nyimbo za kisanii za mafanikio hewa na badala yake waibue na kupigia kelele matatizo makubwa ya kijamii kama haya. Tunawahukumu Ujinga na Umaskini wa milele watoto hao kwa kuwanyima Elimu bora na mazingira bora ya upatikanaji wake. Nafikiri huko hakuna hata Madiwani wa kuyaona mapungufu hayo!!

  • HEko na pongezi kwa mwandishi wa habari hii. Ni heri na wengine kuihabarisha jamii kuhusu matatizo kama haya katika jamii.

    Ni matumaini yangu kuwa si Ruvuma tu kwenye matatizo haya bali hata na mikoa mingine pia.

    Hvyo wito kwa jamii tuibue na kuyaweka hadharani matatizo huenda wahusika watasikia na kuyafanyia kazi. Kisha eti tunalalamika kuwa Elimu inashuka!!!! Itapanda vipi kama watoto wanasoma katika mazingira magumu namna hii???

    Serikali inia fanya tathmini ya mafanikio ya Kielimu kwa kuziangalia shule zilizo maeneo ya mijini tu; kumbe kuna watoto wenye akili na uwezo wa kusoma wapo pia vijijini lakini wanakosa fursa hii.

    Chonde chonde Serikali tuwasaidie watoto wa vijijini kupata elimu bora na siyo bora elimu.

    MIZAMBWA
    INANIUMA SANA!!!

  • Vita Kawawa upo kimyaaaaa….inaonekana vitu hivi huvijui au kwasababu hujaishi Namtumbo ulienda tu kuchukua Ubunge kwa umaarufu wa marehemu baba yako au hutembelei kujua hali ktk jimbo lako ikoje. SHAMA ON YOU.

    Lakini hilo jimbo lina madini nyingi sana ila watu wanaishi kwa kuotea sana

  • Hii si aibu kubwa? kwa taifa lenye miaka 50! kazi ipo. Hapa tuombe tu MUNGU aingilie kati.Lakini pia tuchukue ya kutafuta mabadiliko ya kweli.CHADEMA wanaweza tuwape tuone.

  • Hongereni sana kamati ya shule hii kwa kukataa kujenga vibanda vya nyasi. Shule inapendeza sana na hata kama atatokea mfadhili lazima afuate masharti yenu kamati ya shule Hongera

    Elimu lazima itolewe kwenye madarasa bora yenye madawati mazuri kama niliyoyaona tatizo vyumba ni vichache

    Lakini tujipe moyo kwani ushindi ni kesho kwasasa wekeni partition za plywood kugawa madarasa hayo kwa muda wakati mnakusanya nguvu

    Serikali kuu imeshaona hii ni aibu kwao kutoa liseni ya kufungua shule kwa wanafunzi 403 kwa madarasa 4 darasa la kwanza hadi la saba maana yake bora liende na itakapofika darasa la saba wanasema wamemaliza shule hawajui kusoma na kuandika watajuaje kwa mazingira haya

    Elimu ni gharama mimi kama mzazi najitahidi sana nimrishishe mtoto wangu elimu kwa kila hali kwani ndiyo baba yangu marehemu alinipa ikanipeleka hadi ulaya

    Sikusoma shule ya matajiri nilisoma shule kama hii hii kwa shida hizi hizi lakini wazazi msikate tamaa kwani mkikata tamaa watoto wenu watakuwa homeless baadaye wasiokuwa na elimu ya kutosha.

    Semeni kwa sauti kwenye halmashauri zenu kwenye chama tawala kama hawasikii onyesheni kwa vitendo kwamba hamuwahitaji kwani watoto wenu hawapati elimu ya kutosha

    Siyo mbali uchaguzi ni mwaka 2015 mchague kiongozi yule ambaye anaweza kweli kulisimamia tatizo hili la madasara na elimu kwa ujumla

    Mungu ibariki Tanzania

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *