Biharamulo: Wananchi wajiandaa kuandamana kwa Mkuu wa Wilaya kudai shule yao

Jamii Africa

BAADHI ya wananchi wa Kitongoji na Kijiji cha Busiri, Kata ya Nyakahura wilayani Biharamulo mkoani Kagera, wametishia kuandamana hadi Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, kudai ujenzi wa shule baada ya uongozi wa kijiji kudaiwa kutafuna michango yao.

Wananchi hao wamesema wako tayari kufika hata kwa mkuu wa mkoa ili kupata haki zao za utawala bora na uhuru wa kidemokrasia kwa mujibu wa sheria.

FikraPevu ilishuhudia wananchi hao wakizungumza leo Machi 29, 2017 katika mkutano wa kijiji hicho ambapo wameutuhumu uongozi wa kijiji kutafuna fedha walizochangishwa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi ili kuwanusuru wanafunzi kutembea zaidi ya kilometa 10 kwenda kusoma katika Shule ya Nyamalagara, Kata ya Lusahunga wilayani humo.

Wananchi wa Kitongoji na Kijiji cha Busiri, Kata ya Nyakahura wilayani Biharamulo mkoani Kagera, wakiwa mkutanoni.

Mmoja wa wananchi hao, Tandu Mniko, alisema kila kaya ilitoa Shs. 25,000 pamoja na kusomba mawe, mchanga na kufyatua matofali, lakini mpaka sasa bado watoto wao wanaendelea kuteseka kwa kukosa shule.

Alisema anashangaa kuona miaka miwili imepita tangu walipochangishwa fedha hizo pamoja na kufyatua matofali, huku kukiwa hakuna hata dalili za ujenzi katika eneo lenye rasilimali misitu inayotoa mbao ambazo zinazouzwa kwa magendo.

Tuhuma zaidi

Aliongeza kusema kwamba, Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Enock Kulindwa, anayetakiwa kusimamia maendeleo ya wananchi na Ofisa Mtendaji wake wametelekeza kijiji na akawatuhumu kuwa walarushwa na wanauza mali za wananchi. 

“Miaka miwili iliyopita wananchi walikusanya matofali 45,000 na tangu Agosti 2016 hakuna taarifa za mapato na matumizi ya michango inayokusanywa licha ya kuona magari yakisomba mbao na mkaa kwenye misitu,” alisema Mniko. 

FikraPevu ilishuhudia mwananchi mwingine, Yakobo Thomas, akisema Mwenyekiti wa Kijiji hawashirikishi wananchi na akautaka uongozi kurejesha fedha za wananchi walizochanga ili kujenga madarasa katika shule ambayo ujenzi wake umekwama kwa zaidi ya miaka miwili.

Alisema wanafunzi 140 wa kijiji hicho huamka alfajiri kwenda Shule ya Msingi Nyamalagara ambapo wengi wao ni wadogo na huomba usafiri kwenye magari ya abiria yatokayo Wilaya ya Ngara hadi Kahama na wasipochukuliwa na magari hayo hufika shuleni kati ya saa 3 au saa 4 na kukosa vipindi vitatu vya kwanza.

“Watoto wetu wanateseka, wanatakiwa kuwa na shule ya kujengwa na sisi wazazi na serikali itasaidia nguvu zetu zilipofikia, misitu hii imejaa miti na jamii ya hapa wanaikata kwa mkaa na kuuza mbao kinyemela,” alisema Thomas. 

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Busiri, Shaban Yusufu Kazimoto, amekiri kuchangisha takriban Sh. 2,957,000 ambazo kuwa alizikabidhi kwa Mtendaji wa Kijiji na kupelekwa benki kwenye akaunti ya kijiji, lakini akasema kuna mvutano wa matumizi ya fedha hizo. 

Alisema kijiji hicho kimekuwa na migogoro kutokana na itikadi za kisiasa na kwamba wananchi wanalo tatizo la wanafunzi kusomea mbali ambapo mwanzo walisomea kwenye Jengo la Kanisa ambalo sasa sheria hairuhusu hadi wawe na shule iliyosajiliwa. 

Mabati yachangwa

Akinamama na watoto nao walihudhuria mkutano huo.

FikraPevu imeelezwa kwamba, kilio cha ujenzi wa shule kijijini hapo ni cha muda mrefu ambapo aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Fabian Masawe, na viongozi wa kamati ya siasa ya CCM walichangia mabati 200  ili kuanza ujenzi wa shule ya kijiji. 

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Enock Kulindwa, ambaye analalamikiwa kukwamisha ujenzi wa shule na shughuli nyingi za maendeleo, hakuweza kufika katika mkutano huo.

Aidha, FikraPevu ilipomtafuta kwa njia ya simu kujibu tuhuma hizo, alisema alikuwa safari wilayani akishughulikia haki za wananchi kupata fedha za TASAF na akasema mkutano uliotishwa haukuwa halali kisheria ambapo umeitishwa na kundi la wapinzani wake kisiasa wakilenga kumdhalilisha kupitia vyombo vya habari.

Uongozi wanena

Diwani wa Kata ya Nyakahura wilayani Biharamulo ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Apolinary Mugalula, alipoulizwa kuhusu mgogoro wa uongozi wa Kijiji cha Busiri alikiri kuwa na taarifa zake na kwamba kila wakifanya mikutano ya maendeleo wananchi hawakubaliani.

Hata hivyo, aliahidi kuhudhuria vikao vitakavyoitishwa na serikali ya kijiji kuondoa kero zinazowakabili wananchi ili kuwaletea maendeleo na kwamba wakazi wa kijiji hicho ni wagenui wa makabila mbalimbali ambao wameingia kuchimba madini na sasa wanahitaji huduma bora za kijamii.

Mkutano huo umeahirishwa hadi Jumanne ijayo ili mwenyekiti huyo aweze kujibu juu ya ujenzi wa shule hiyo na changamoto nyingine zinazokikabili Kijiji cha Busiri ambacho kimesajiliwa miaka mitatu iliyopita ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *