Wasafirishaji wa kahawa, chai, samaki na ngozi kutokana Tanzania kufaidika na soko la Afrika Mashariki baada jumuiya hiyo kuanzisha mfumo wa pamoja wa forodha mipakani unaolenga kuimarisha biashara.
Mfumo huo unalenga kupunguza urasimu na kuchelewa kwa mizigo kwenye mipaka kunakotokana na ukaguzi wa bidhaa hizo kabla hazijaingia kwenye nchi nyingine. Mfumo huo pia utapunguza gharama za kuvusha bidhaa kwenye mipaka kwasababu wasafirishaji hawatakaguliwa kwenye kila mpaka.
Taarifa ya Kamati ya forodha ya Afrika Mashariki imesema mfumo wa pamoja wa forodha mipakani kwa bidhaa 5 ulianza Mei 10 mwaka huu, na kwa bidhaa zote utaanza rasmi June 1.
Kamati ya Forodha inatekeleza maelekezo ya Kikao cha 19 cha Afrika Mashariki kilichofanyika Februari. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hadi kufikia Disemba mwaka huu, mfumo huo utahusisha bidhaa zinazosafirishwa na meli na biashara zote zinazofanyika ndani ya mipaka ya jumuiya hiyo.
Tanzania kama zilivyo nchi zingine za Afrika Mashariki hazifanyi vizuri biashara ya mipakani ukilinganisha na vigezo vya kimataifa. Ripoti ya Benki ya Dunia ya Biashara 2018 inaeleza kuwa nchi za Afrika Mashariki zilipata alama za chini kwenye viashiria vya biashara ya mipakani.
Kwa mfano, Rwanda ilishika nafasi ya 87, ikufuatiwa na Kenya nafasi ya 106, Uganda (127), Burundi (164) na Tanzania (182) miongoni mwa nchi zote duniani.
Wataalamu wa biashara wanaeleza kuwa kuondoa vikwazo visivyo vya ushuru mipakani kutasaidia kupunguza gharama za kusafirisha bidhaa kati ya asilimia 12.5 na asilimia 17.
Malori yakisubiri kuvuka mpaka
Hata hivyo, hatua kubwa imepigwa ambapo bidhaa zinachukua siku 3 hadi 5 kutoka katika bandari za Mombasa na Dar es Salaam kuelekea Kampala, Kigali na Bujumbura. Mfumo huo pia umepunguza gharama za ziada kwa wasafirishaji ambazo walikuwa wanatozwa kwa malori yao kukaa muda mrefu bila kupakuliwa mizigo. Gharama za roli ambalo halijashusha mzigo ni Dola za Marekani kati ya 200 na 400.
Pamoja na changamoto za uchukuzi, wadau mbalimbali wamendelea kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa kukuza biashara katika ukanda wa Afrika Mashaki na nchi nyingine ili kukuza kiwango cha uchumi na maendeleo kwa wananchi wa kawaida.
Kwa kutambua hilo, taasisi ya Alama ya Biashara Afrika Mashariki (TMEA) kwa kushirikiana na nchi za ulaya wameanzisha mfuko maalumu utakaosaidia kutatua changamoto mbalimbali za uchukuzi kwa kutumia utafiti na ugunduzi wa njia bora za kuimarisha sekta ya uchukuzi ili kukuza biashara barani Afrika.
Mfuko huo unajulikana kama Ufumbuzi katika Sekta ya uchukuzi na Usafirishaji (Logistic Innovation for Trade (LIFT) Fund) unalenga kuibua mbinu mbadala za kisayansi zitakazosaidia kutatua tatizo la usafiri wa mizigo ambalo limekuwa kikwazo cha kukua kwa biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.
“Tumepiga hatua kubwa katika kupunguza gharama za uchukuzi na usafiri katika ukanda huu kwa njia za ufumbuzi. Mfuko unatarajia kutafuta njia mbadala zitakazoinua ushindani wa biashara ambao utachangia mafanikio ya jumuiya ya Afrika Mashariki”. inaeleza ripoti ya mfuko huo.
Malengo ya mfuko ni kupunguza mda mwingi unaotumika kusafirisha bidhaa katika milango mikuu ya Afrika Mashariki na kuchangia katika malengo ya TMEA ambayo yanakusudia kupunguza mda wa usafiri katika milango mikuu ya usafirishaji kwa asilimia 15 ifikapo mwaka 2016.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa ikiwa sekta ya uchukuzi na usafiri ya Afrika Mashariki haitapatiwa ufumbuzi wa kudumu mafanikio ya biashara katika nchi hizo hayatafanikiwa na kukua katika viwango vya kimataifa na kuchangia kukuza uchumi wa nchi mojamoja za ukanda huu ambazo zinakabiliwa na changamoto nyingi za umaskini.