‘Washirika wa maendeleo’ kuiwezesha Tanzania kiuchumi

Jamii Africa

Serikali ya Tanzania imekubaliana na Washirika wa Maendeleo kurejesha uhusiano wa karibu na wenye tija ili kusaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka Mitano pamoja na Mkakati wa Kukuza Uchumi Zanziba (MKUZA III).

Hayo yamebainishwa mjini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James, wakati akifungua mkutano wa Mazungumzo ya kimkakati kama ilivyobainishwa kwenye Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo.

James amesema kuwa Mwongozo huo ni wa miaka 7, kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018 hadi 2014/2025, umelenga kuipa Serikali nafasi ya kuongoza mchakato wa maendeleo na kuijengea serikali uwezo wa kukusanya mapato yake ya ndani, kuchambua fursa muhimu za uwekezaji na kutumia masoko ya kikanda na kimataifa kupata faida.

"Tumekubaliana kwamba tutasimamia mchakato mzima wa maendeleo sisi wenyewe kama nchi, matumizi mazuri ya rasilimali, kuimarisha uwajibikaji, kukuza biashara na uwekezaji wa ndani na nje" amesema James.

Amesema kuwa nchi inajivunia hatua kubwa iliyofikiwa kiuchumi na kijamii ambayo Tanzania imefikia, ikiwemo kutambuliwa kimataifa kuwa kinara wa masuala ya ukuaji wa uchumi wa Taifa na uchumi jumuishi miongoni mwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Akizungumza katika mkutano huo uliowashirikisha Washirika wa Maendeleo kutoka nchi mbalimbali duniani, Mratibu wa Umoja wa Mataifa na kiongozi wa washirika hao, Alvaro Rodriguez, ameahidi kuwa watashirikiana na Tanzania ili malengo ya maendeleo yaweze kufikiwa kwa kuimarisha ushirikiano ambao hapo awali ulianza kulegalega.

Ameeleza kuridhishwa na hatua zinazochukuliwa na serikali zote mbili za Tanzania Bara na Zanzibar katika kufanikisha malengo yake ya kukuza uchumi kama ilivyoainishwa katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo (FYDPII) na Mkakati wa Kukuza Uchumi Zanzibar (MKUZA III).

Meza Kuu ikiongozwa na Mwenyekiti wa Mkutano kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (wa tatu kulia), anaefuata kulia ni Mwenyekiti Mwenza na Mratibu wa Umoja wa Mataifa na kiongozi wa washirika hao wa Maendeleo Bw. Alvaro Rodriguez, mjini Dodoma.

Amesema ili mipango hiyo iweze kufanikiwa kuna umuhimu wa kuishirikisha kikamilifu Sekta Binafsi pamoja na washirika wa maendeleo kwa kuweka mazingira ya kuongeza uzalishaji, kukuza ajira kwa vijana wa kike na wa kiume na hatimaye kufanya mapinduzi ya kiuchumi.

"Vijana takribani milioni moja wanaingia katika soko la ajira kila mwaka, hivyo ni muhimu kuweka mazingira ya upatikanaji wa ajira tena zenye staha katika kipindi hiki ambacho nchi inafanya mapinduzi makubwa ya viwanda na uchumi" alisisitiza Rodriguez.

Amesema kuwa uwekezaji katika masuala ya elimu, afya, hifadhi ya jamii, kutoa fursa sawa kwa wote (wanaume na wanawake) ni muhimu katika masuala ya uzalishaji.

Ameahidi kuwa Wadau wa Maendeleo wako tayari kusaidia jitihada hizo ili kuhakikisha kuwa Tanzania inafikia malengo hayo kwa kuwezesha miundombinu ya ukusanyaji mapato yake ya ndani, usimamizi na matumizi mazuri ya fedha za umma, kuiwezesha sekta binafsi kushiriki katika miradi ya maendeleo pamoja na kusaidia kuibua sera bora na kufadhili miradi yenye tija kwa taifa.

Serikali na Washirika wa Maendeleo wamekubalina kukutana mara mbili kwa mwaka ambapo kikao kingine kinatarajiwa kufanyika mwezi Novemba, 2018.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *