‘Wasiojulikana’ waitia doa Tanzania. Jumuiya za Kimataifa zaingilia kati utekaji, mauaji ya raia wasio na hatia

Jamii Africa

Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) imeitaka serikali ya Tanzania kudumisha amani, utulivu na misingi ya demokrasia kwa kuhakikisha inawachukulia hatua za kisheria wale wote wanaohusika na utekaji na mauaji ya raia wasio na hatia.

Tamko hilo limetolewa jana na Mabalozi wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Ulaya wenye uwakilishi Tanzania na kuungwa mkono na Mabalozi wa Norwei, Kanada na Uswisi ambapo wameshtushwa na matukio ya hivi karibuni ya raia na viongozi wa kisiasa kutekwa, kuteswa na kuuawa na watu wanaodaiwa ‘wasiojulikana’.

"Tunashuhudia kwa wasiwasi muendelezo wa matukio ya hivi karibuni yanayotishia nidhamu ya kidemokrasia na haki za Watanzania, katika nchi iliyojizolea umaarufu mkubwa duniani kwa utulivu, amani na uhuru”, imeeleza taarifa ya EU.

Wito huo wa EU unakuja siku chache baada ya kifo cha mwanafunzi wa Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline aliyeuawa kwa kupigwa risasi akiwa kwenye daladala wakati wa maandamano yanayodhaniwa yaliwakuwa ya wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) siku ya ijumaa ya Februari 15 mwaka huu.

Mabalozi hawa wamemwomba rais John Magufuli kuanzisha uchunguzi wa matukio yote ya kushambuliwa na kuuawa kwa raia na wahusika wafikishwe kwenye vyombo vya sheria mara moja.

"Tumesikitishwa na kifo cha mwanafunzi aliyepigwa risasi mwisho wa juma lililopita Akwilina Akwilini Bafta, anayeombolezwa nchi nzima. Tunakaribisha wito wa Rais Magufuli wa uchunguzi wa haraka. Vilevile, tunatoa wito wa uchunguzi wa kina katika vifo vyote vya wanaharakati wa kisiasa na haki za binadamu.

"Tuna wasiwasi na ongezeko la ripoti za ukatili katika miezi ya hivi karibuni, kama vile: jaribio lililohatarisha maisha ya Mbunge Tundu Lissu; kupotea kwa watu kama mwandishi wa Habari Azory Gwanda; pamoja na mashambulio yaliyopoteza uhai wa viongozi wa serikali, wawakilishi wa vyombo vya usalama na wananchi yaliyotokea Mkoa wa Pwani ndani ya miaka miwili iliyopita”. wamesema Mabalozi hao katika taarifa yao.

Wakati bado watanzania wakiomboleza juu ya kifo cha Akwilina, Diwani wa Kata ya Namwawala Wilayani Kilombero, Godfrey Luena (CHADEMA) ameuawa nyumbani kwake kwa kukatwakatwa kwa mapanga na watu ‘wasiojulikana’.

                                                                 Maandamano ya wafuasi wa vyama vya siasa

Kabla ya kifo cha Akwilina na Luena, kumekuwa na mfufululizo wa matukio ya maiti za watu kukutwa kwenye fukwe za Coco  jijini Dar es Salaam zikiwa zimefungwa kwenye viroba ikiwemo ya aliyewakuwa Katibu wa CHADEMA kata ya Hananasif, Daniely John.

Lakini bado jamii ya kitanzania inashuhudia idadi ya raia wasio na hatia na waandishi wa habari kupotea katika mazingira yasiyoelezeka. Mpaka sasa waliopotea kusikojulikana ni mwanachama wa CHADEMA, Ben Saanane, Mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda na Emmanuel Kibiki (Raia Mwema).

EU imebainisha wazi kuwa, "Tunaungana na watanzania katika kuziomba mamlaka husika, kutunza amani na usalama wa michakato ya kidemokrasia, nchi, watu wake na kuheshimu utawala wa sheria bila udhalimu."

Kwa upande wake, Umoja wa Mataifa kupitia  gazeti la Inner City Press umesema unafuatilia kwa karibu matukio yanayoendelea nchini na wameitaka serikali kuheshimu uhuru wa kujieleza na  haki ya kukusanyika.

Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania siku za hivi karibuni ulitoa tamko la kulaani matukio yanayoendelea nchini na kueleza kuwa, ‘’Tunatoa wito kwa vyama vyote kulinda amani na usalama wa mchakato wa kidemokrasia, taifa na wa watu wa Tanzania’’,

 ‘’Tunaungana na Watanzania katika kutoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wenye uwazi ili kuwawajibisha wale wote wanaohusika na vitendo hivi vya kikatili kwa mujibu wa sheria za Tanzania’’

Hata hivyo, Kwa nyakati tofauti serikali imekuwa ikisisitiza kuwa inaendelea na uchunguzi wa matukio yote na watekaji na wauaji wote lazima wafikishwe mahakamani lakini mpaka sasa ripoti za uchunguzi hazionyeshi juhudi za wazi kumaliza tatizo hili ambalo limeanza kuota mizizi katika jamii.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *