Wataalamu wa Uzamiaji kutoka nchini Afrika ya Kusini, leo wameanza zoezi la kutafuta miili ya watu waliokwama kwenye meli ya MV Spice Islander iliyozama kwenye eneo la Nungwi nje kidogo ya mji wa Zanzibar mwishoni mwa wili iliyopita.
Afisa Habari wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, amesema kuwa Wataalam hao wanafanya operesheni hiyo kwa pamoja na Wazamiaji kutoka Jeshi la Wananchi JWTZ, Jeshi la Polisi na KMKM pamoja na Wadau wengine wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama hapa nchini.
Inspekta Mhina amesema kuwa hata hivyo, Wazamiaji hao bado hawajatoa taarifa za kuonekana kwa mabaki ya meli ama mwili wa mmoja wa watu waliozama katika kina hicho kirefu cha bahari na zoezi limeahirishwa kutokana na hali mbaya ya hewa na limepangwa kuendelea tena kesho.
Nayo Ofisi ya Ubalozi mdogo wa Tanzania uliopo Mombosa nchini Kenya, leo umetoa taarifa ya kuoneka kwa miili ya watu watano kwenye fukwe za Bahari ya Hindi eneo la Shimoni nchini humo ikiwa imeharibika kiasi cha kutotambulika. na kufanya idadi ya watu walibainika kufariki katika ajali hiyo kufikia 201.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Zanzibar, Makamu wa Raisi wa Serikali ya Zanzibar, balozi Seif Iddi, amesema kuwa Serikali ya Tanzania imetoa ithini kwa Serikali ya Kenya kuiizika miili hiyo huko Mombasa kutokana na kuharibika kiasi cha kutowezekana kusafirishwa kurejeshwa hapa nchini kwa mazishi.
Balozi Iddi, amesema miili ya watu hao ambayo haikuweza kutambuliwa kutokana na kuharibika vibaya imepatikana jana usiku katika eneo hilo la Shimoni na kuzikwa kwa taratibu zote za kibinadamu.
Awali Serikali ya Tanzania kupitia kwa Waziri wan chi Ofisi ya makamu wa Pili wa rais wa SMZ Mh. Mohammed Aboud, alitoa wito kwa nchi jirani za mwambao wa Bahari ya Hindi kutoa taarifa za kuonekana kwa miili ikielea baharini.