Wazee wa Songea watozwa pesa za Matibabu licha ya kuwa na Daftari lenye Muhuri wa kutibiwa bure!

Mariam Mkumbaru

Wazee wa kijiji cha Ifinga kata ya Ifinga wilaya ya Songea mkoa wa Ruvuma, wanatozwa pesa za matibabu, licha ya serikali kuwafutia gharama za matibabu wakienda katika vituo mbalimbali vya afya, pamoja na kupewa daftari lililogongwa muhuri wa kutibiwa bure.

Hali hiyo imebainika katika kijiji cha hicho kwa wazee hao kuendelea kutozwa pesa za matibabu wakienda kutibiwa katika, zahanati, kituo cha afya na hospitali ya Peramiho.

"Nimetoka kufanyiwa upasuaji wa Ngiri katika hospitali ya peramiho, lakini mara ya kwanza nilipofika kwa ajili ya kupatiwa huduma hii, nikaaambiwa nilipie sh. 100,000 nikasema sina pesa waliniacha hawakunipa huduma yoyote huku nikiwaonesha daftari la kutibiwa bure,mpaka nikaamua kurudi nyumbani,"alisema Mzee Ladslaus Rwanda (65)

 

wazee-songea

Baadhi ya Wazee wa Ifinga wanaotuzwa pesa za matibabu katika vituo vya afya Songea

Rwanda alisema kuwa alikaa nyumbani kwa muda wa miezi miwili huku akiwa na maumivu makali ya ugonjwa huo, watoto wake baada ya kuuza mazao na kufanya shughuli za kibarua katika mashamba mbalimbali ndio wakampatia ya kwenda kufanyiwa upasuaji.

"Niliporudi tena na pesa mkononi walinipokea na kunifanyia upasuaji vema na kunipatia dawa za kutuliza maumivu za kutumia kwa muda wa siku saba, kama huna pesa unakufa huku unajiona, wakati serikali imetueleza wazee kama mie unatakiwa kutibiwa bure ukienda katika vituo vya afya mbalimbali sasa sielewi kwa nini bado wanatutoza pesa za matibabu," Rwanda.

Dafroza Komba (75) alisema kuwa, akiumwa anatibiwa katika zahanati ya Ifinga ambayo ndio ya karibu katika kijiji hiki,lakini akifika katika zahanati hiyo lazima alipie gharama za matibabu.

"Nikienda kutibiwa kama sina pesa wananiacha hawanipi huduma  narudi nyumbani kuwaomba watoto wangu pesa ya matibabu wakinipa nikirudi zahanati ndio napata huduma ya matibabu,"alisema Dafroza.

daftari-wazee

Moja ya Daftari liligongwa mhuri wa kutibiwa bure waliopewa wazee wa Songea

Gharama za matibabu katika zahanati ya Ifinga kama unaumwa malaria kupima ni sh. 500, kung'olewa jino sh. 3,000, dripu sh. 4,000, Qunin sh.3,000, dawa ya kifua sh. 2,000 na dawa za maumivu sh. 1,000.

Mkurugenzi wa wilaya ya Songea Beatrice Msomisi alisema kuwa, tatizo hilo analifahamu kwa wazee kulipia gharama za matibabu katika zahanati 14 zilizokuwa chini ya Kanisa Katoliki na hospitali ya peramiho.

"Tumeandika mkataba wa makubaliano kati yetu serikali na Kanisa Katoliki ambao utaanza kutumia hivi karibuni, mkataba huo utasaidia kupunguza gharama za matibabu kwa wazee, wajawazito na watoto wa chini ya miaka mitano,"alisema Msomisi.

Msomisi alisema kuwa, kuna changamoto kubwa sana katika suala zima la upatikanaji wa huduma za afya kwa wilaya ya hii, kwa sababu wilaya haina hospitali ya wilaya na hospitali wanayoitegemea kwa sasa kutoa huduma ni peramiho ambayo iko kibiashara zaidi.

Aidha alisema kuwa, tatizo la kuchangia huduma za afya kwa wazee sio kwa Ifinga pekee, bali nitatizo katika zahanati zote zilizojengwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Songea, sehemu ambazo serikali imeshindwa kujenga zahanati Kanisa wamejenga ila huduma zake lazima mgonjwa alipie.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *