Zitto amvaa Spika kuhusu posho; Asema aweza kuvuliwa uspika kwa kuvunja sheria kwa makusudi!

Jamii Africa

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CDM) Bw. Zitto Kabwe amesema kuwa uamuzi wa Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bi. Anna Makinda kuhalalisha kupanda kwa viwango vya posho za wabunge ni ukiukwaji mkubwa wa sheria na anapaswa kuwajibika kwa hilo.

Akiandika kwenye ukurasa wake wa Mtandao wa Facebook Zitto amesema kuwa posho za wabunge hazipandishwi kiholela kwani kufanya hivyo ni makosa. “Spika wa Bunge anajua kwamba posho zote hulipwa Baada ya Rais kuidhinisha. Posho anazotangaza hazijaidhinishwa kwani uthibitsho wa kuidhinisha ni Masharti Mapya ya Kazi kwa Wabunge ambayo hayajatolewa na Ofisi ya Rais. Hivyo kitendo cha kuanza kulipa posho mpya bila Masharti Mapya ya kazi za Wabunge ni kukiuka sheria ya utawala wa Bunge kifungu cha 19.”

Akifafanua maoni yake hayo Bw. Zitto amesema kuwa “Wabunge wasifanye mchezo na suala la posho. Wananchi wamekasirishwa sana na kwa kweli hatuwaelewi. Wakati Bunge la Tisa lilisifika kwa kupambana na ufisadi, Bunge la kumi litabatizwa Bunge la Posho. Ni lazima tukatae kuonekana tunajijali badala ya kujali wananchi.”

Zaidi ya hayo Zitto alienda mbali zaidi na kudai kuwa  “Spika anapaswa kuheshimu sheria ambazo Bunge limepitisha na kwenda kinyume na sheria kwa makusudi ni kosa la kuvuliwa Uspika” Zitto ambaye ni mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu wa Kiongozi wa Upinzani Bungeni amesema kuwa endapo itaridhiwa kuwa posho hizo nono zitakubaliwa kulipwa kwa wabunge wa sasa itakuwaje kwa Bunge la Katiba ambalo zaidi ya nusu yake ni wabunge na wawakilishi wa CCM. “Jambo la kuzingatia kwa sasa ni kwamba, iwapo posho hizi zitalipwa kwa wabunge, nini kitazuia posho Kama hizo kulipwa kwa wabunge wa Bunge Maalumu la katiba? Huo mzigo serikali itaubeba namna gani na Hali hii ya uchumi?”

Bw. Zitto alitoa wito kwa uongozi wa Bunge kuwajibika na kukataa posho hizo kwani ni kinyume na maslahi ya wananchi na kuwa badala ya kujiongezea posho hizo tamu Bunge na serikali ijitahidi katika kuinua uchumi ili kila Mtanzania anufaike na jasho lake.

“Namsihi Spika aachane kabisa na suala hili la posho. Tukazane kukuza uchumi wa nchi ili wananchi wapate ajira, kodi iwe nyingi na tuongeze mishahara kwa wafanyakazi wote. Hoja ya ugumu wa maisha ni kwa wananchi wote sio wabunge peke yao.”

Suala la ongezeko la posho siku chache kabla ya maadhimisho ya miaka hamsini ya uhuru limewagusa vibaya wananchi wengi ambao wameona kuwa kitendo hicho cha wabunge kujiongezea posho wakati taifa liko katika hali mbaya ya kiuchumi huku tofauti ya wanufaika wa kisiasa na maskini ikizidi kuwa kubwa kila siku. Ongezeko la posho liliibuliwa na gazeti moja nchini na baadaye kupingwa na Katibu wa Bunge Dr. Kashilillah kuwa hazikuwa na ukweli wowote na kuwa zililenga kuwachonganisha wabunge na wananchi wao.

Spika Anna Makinda akiapa kulinda Katiba

Hata hivyo, masaa machache baadaye Spika wa Bunge hilo Bi. Anna Makinda alilizungumzia suala hilo wakati akipokea taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Watu  ambapo alikubali kuwa ni kweli ongezeko hilo limetokea kwa zaidi ya asilimia 170 toka shilingi elfu 70 kwa siku hadi shilingi 200,000 kwa siku. Spika Makinda amedai kuwa ongezeko hilo linaakisi kupanda kwa gharama za maisha huko Dodoma na hivyo fedha hizo zitawasaidia wabunge kuhudumia wananchi vizuri zaidi. Hata hivyo, hakueleza kama huko Dodoma gharama hizo zimepanda kwa wabunge tu au kwa walimu, polisi, madaktari na wananchi wa kawaida wa Dodoma vile vile ambao serikali haikuwapa ongezeko lolote la posho au mishahara.

 

Na. M. M. Mwanakijiji

7 Comments
  • Kwakweli sitakikuamini kuwa Anna Makinda na wenzake walioshauriana kufanya na kutoa tamko hilo wanahitaji kupelekwa haraka INDIA kwa matibabu ya akili”kweli hata mtoto wa darasa la sita anaweza kuuliza hivi maisha kupanda yamepanda kwa wabunge tu?na je walala hoi,mahausi geli,mabaa medi,walimu na madaktari,maaskari gharama za maisha kwao hazijapanda?nakama zimepanda wao mishahara yao imepanda?au hivi hizo sababu za kufanya gharama za maisha kupanda zimetokea Dodoma tu?
    Hata kiwango hicho kupanda kwa kiasi kikubwa namna hiyo ni ajabu mno”spka ni spika watumbo c wawananchi’

  • Ncha ya sindano kwenye Jicho….Watanzania tuamke sasa,wanasiasa wanahisi hii nchi tumewakodishia.

  • Hapo mkuu hoja binafsi ni muhimu
    kitendo cha kuanza kulipa posho mpya bila Masharti Mapya ya kazi za Wabunge ni kukiuka sheria ya utawala wa Bunge kifungu cha 19.”ni suala ambalo hatuwezi kuliacha lipite tu kama upepo.Tunaomba wabunge wetu wa upinzani wasimame kidete kwa hili.

  • Kama kweli wabunge ni watetezi wa wanyonge kinachopelekea wao kulala 5 star hotels hadi kulipa pango la shs 100,000 na zaidi kwa siku ni nini? Sidhani kama gharama za maisha ya Dodoma zimekuwa juu kiasi hicho.

  • Makinda na wenzake wana ajenda ya siri.
    Impossible katibu aseme hajui kuwepo ongezeko la posho na siku moja badaye sipika aseme posho ni mazingatio ya kupanda maisha katika eneo la bunge hapo Dodoma!
    Hapana shaka pana kitu! Ama
    Kuihujumu serikali ya kikwete,
    kikwete anahujumiwa waziwazi!!

  • Anne Makinda,
    the honerable speaker of National assembly of Tanzania proved failure!!
    She is a great conspirant to jakaya kikwete’s leadership!
    She is deeply undermining this government in indirect way.
    Unbelievable manner Makinda way goes,
    Sitting allawance increment without abide needed procedures is a sufficient evidence that Anne Makinda is an enemy of His exellence the head of the state,
    no more, that is all.

  • Sasa jaman si maisha yamepanda kwenye ma supermarket? wao wapo juu bwana hawawez kununua vitu kwa walala hoi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *