UKIFUATILIA takwimu za wanawake waliokwenda kwa hiari katika hospitali ya mkoa wa Dodoma kujaribu kuona nini kinawasibu katika miili yao, utakubaliana na taarifa kwamba kansa ya shingo ya kizazi inashika kasi mkoani Dodoma.
Dk Hinju January ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake katika hospitali ya mkoa wa Dodoma anafafanua kuwa katika kipindi cha mwaka 2012 waliodhaniwa kuwa na saratani ya shingo ya kizazi walikuwa ni 156, lakini baada ya kuwapima wagonjwa 116 waligundulika kuwa na tatizo hilo.
Aidha ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2013 wanawake 168 waliodhaniwa kuwa tatizo hilo baada ya kuwafanyia vipimo 126 waligundulika kuwa na saratani ya shingo ya kizazi.
Daktari huyu bingwa anasema takwimu hizo kwa miaka miwili kuanzia 2012 hadi 2013 zinafanya idadi ya wanawake wenye tatizo hilo kufikia jumla ya 242 .
Ameeleza kuwa tatizo kubwa ni wanawake wengi mkoani Dodoma kuchelewa kufika hospitalini ili kuchunguza afya zao hali ambayo inasababisha wengi wanafika wakiwa katika hali mbaya na hivyo kupoteza maisha.
Dalili na chanzo
Dk Hinju anasema kuwa dalili za ugonjwa huu,mwanamke kutokwa na damu pale anaposhiriki tendo la ndoa,nyingine ni mama kutokwa maji yenye harufu kali sehemu zake za siri,maumivu wakati wa tendo la ndoa na kutokwa mkojo bila ya kujitambua.
Anasema kuwa ugonjwa huu unatokana na virus vinavyoitwa H.P.V ambavyo mwanamke anavipata kutoka kwa mwanaume, mtaalamu huyo anasema kuwa ugonjwa huu kwa asilimia 90 unatokana na tabia ya mwanamke kuwa na wanaume wengi.
Amesema mwanamke anapokuwa na wapenzi wengi huweza kupata virusi hivyo vya H.PV kwa kuwa baadhi ya wanaume wanavyo hasa wale ambao bado hawajatahiriwa.
Dk Hinju anasema kuwa asilimia kubwa ya wanaume hasa maeneo ya vijijini katika mkoa wa Dodoma,hawajafanyiwa tohara hii inatokana na kukosekana kwa elimu ya kutosha kwa wakazi wa maeneo hayo juu ya umuhimu wa kutahiri lakini sio mila au utamaduni wa wakazi wa mkoa wa Dodoma.
Hata hivyo alisema kuwa kampeni ya tohara kwa wanaume inayoendelea katika baadhi ya mikoa pia inafanyika katika mikoa ya kanda ya kati ikiwemo Dodoma Vijijini hivyo itasaidia wanaume wengi wa maeneo hayo kufanyiwa tohara.
Mila ya mbuya
Uchunguzi wa mwandishi wa makala hii umebaini kuwa ,ipo mila inayojulikana kwa jina la mbuya hasa kwa watu wa kabila la wagogo,ambayo,inaruhusu mwanamke kuwa na rafiki wa kiume wa nje mbali na mume wake wa ndani.
Katika mila hiyo mwanamke wa kigogo mbali na kuwa na mume wake pia anaweza kuwa na rafiki wa kiume wa nje,hivyo kutokana na hali hiyo pia ni chanzo kingine maambukizi ya Saratani ya shingo ya kizazi.
Dk Hinju alifafanua kuwa Saratani ya shingo ya kizazi matibabu yake yanahusisha dawa za kukabili bakteria, mionzi, pamoja na mgonjwa kuongezewa damu wakati akiendelea kutumia dawa.
Mtaalamu huyo anaeleza kuwa mtu mwenye saratani ya shingo ya kizazi akiwahi matibabu katika hatua ya kwanza huweza kupona ugonjwa huo ila tatizo kubwa kwa mkoa wa Dodoma, wanawake wengi wanapobainika kuwa na tatizo hili na wanapotakiwa kwenda taasisi ya saratani Ocean Road wanaogopa kwenda kwa fikra potofu kuwa wanakwenda kufa.
Dk Hinju amewataka wanawake wa mkoa wa Dodoma,na Tanzania kwa ujumla kuwahi hospitali na katika vituo vya afya pale wanapoona wana dalili za saratani ya shingo ya kizazi kwani wakiwahi kuna uwezekano wa kupona.
Anasema kwa sasa mkakati wa mkoa ni kila kituo cha afya katika mkoa wa Dodoma,kimepewa jukumu la kutoa elimu kwa akina mama ambayo inahusisha semina ,kupewa majarida yanayoelezea tatizo hilo,lakini Redio za kijamii za mkoa Dodoma zina vipindi maalumu vinavyozungumzia Saratani ya shingo ya kizazi,Dk Hinju anaeleza kuwa kampeni hii itasaidia kupunguza maambukizi ya maradhi hayo.
Wagonjwa wanasemaje?
Baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma wanaoendelea kupatiwa matibabu,wanakiri kuwa kukosekana kwa elimu ya juu ugonjwa huo ndio chanzo cha wao kuchelewa kufika hospitali .
Mgonjwa Sarah Mazengo mkazi wa Kijiji cha Mkonze anasema kuwa yeye alianza kujisikia maumivu wakati akifanya tendo la ndoa na mume wake,lakini hakuweza kujua chochote hadi pale alipoanza kuona damu zikimtoka kwa wingi sehemu zake za siri.
Sarah anasema kuwa alipofika Hospitali baada ya kufanyiwa vipimo aligundulika kuwa na saratani ya shingo ya kizazi,lakini kwa kuwa aliwahi matibabu anaendelea na tiba na afya inaendelea kuimarika.
Mgonjwa mwingine Ashura Juma mkazi wa Mpwapwa anaelezea kuwa maradhi hayo yanamsababishia maumivu makali na mpaka sasa ameshindwa kushika ujauzito,kutokana na kuathirika na ugonjwa huo .
Aidha uchunguzi wa mwandishi wa makala hii umebaini wanawake wengi wenye Saratani ya shingo ya kizazi wanatoka Wilaya za Kongwa,Mpwapwa,Bahi,Kondoa na Chemba.
Dk Ntuli Kapologwe aliyekuwa mganga mkuu wa wilaya ya Bahi wakati wa mahojiano haya alisema kuwa ,tatizo la saratani ya shingo ya kizazi limewaathiri wanawake wengi,kiasi kwamba amekuwa akitoa rufaa nyingi za kwenda hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma.
Amesema kuwa tatizo kubwa analoliona yeye ni wanawake wengi kushindwa kuelewa dalili za ugonjwa huo,na wengi wanachelewa kufika hospitalini hali ambayo inasababisha wagonjwa wengi kufa.
Mila potofu
Kwa upande wake mganga mkuu wa wilaya ya Kongwa, Gatete Mahava alisema kuwa mila potofu ya kuwa na wapenzi wengi,hasa maeneo ya vijijini inapaswa kupigiwa kelele sana ili watu wabadilike kwa kuwa tatizo hilo ndio chanzo cha saratani ya shingo ya kizazi
Amekiri kuwa hata katika wilaya yake amekuwa akipata wagonjwa wenye dalili hizo na anawapa rufaa waende Hospitali ya mkoa wa Dodoma kwa uchunguzi zaidi.
Naye Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dk Rehema Nchimbi ameeleza kuwa atahakikisha anashikiana na taasisi na wadau wote wa afya ili kuongeza nguvu katika kuhakikisha tatizo hilo linapungua na kunusuru maisha ya akinana mama wa mkoa wa Dodoma.
Amesema kuwa tayari amepewa ripoti ya mpango kazi wa Idara ya afya mkoa hapa unaoonyesha mikakati ya kupambana na maradhi hayo ili kupunguza au kumaliza tatizo hilo kwa wanawake wa mkoa Dodoma.