Maendeleo ya jamii yanachangiwa na mambo mengi ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama. Kwa Tanzania maji yanayozalishwa na Mamlaka za Maji Mjini hayakidhi mahitaji yote ya wakazi, changamoto iliyopo ni Mamlaka hizo kukabiliwa na tatizo la upotevu wa maji kabla ya kumfika mtumiaji
Kupotea kwa maji yanayozalishwa kumeongeza tatizo la uhaba wa wa maji katika maeneo mengi nchini. Hali hiyo hulifanya jiji la Dar es Salaam kupata maji ya bomba kwa mgao katika maeneo yake ili kukidhi mahitaji yote ya wakazi ambao wanaongezeka kila mwaka.
Inaelezwa kuwa Mamlaka za Maji Mjini (UWSSA)na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) hazijafanya juhudi za kutosha kuzuia na kupambana na tatizo la upotevu wa maji ikizingatiwa kuwa kiasi cha maji kinachopotea kinazidi kiwango kilichowekwa cha chini ya asilimia 20.
Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2012 juu ya Usimamizi na Usambazaji wa maji mjini, inaeleza kuwa licha ya kuwa na viashairia vinavyoonyesha kiwango kikubwa cha upotevu wa maji kwenye Mamlaka za Maji, Wizara ya Maji na mamlaka hizo hazija chukua hatua muhimu kuzia na kutafuta njia mbadala dhidi ya tatizo.
“kwa miaka 3 mfululizo katika ukaguzi huu kulikuwa hakuna juhudi za kuridhisha katika kupunguza mwenendo wa maji yanayopotea kwa Mamlaka za Maji zilizokaguliwa. Mamlaka zote zilijiwekea malengo ya chini ya kiwango cha 20%”. Inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.
Kutokana na kutokuwa na mifumo imara ya kudhibiti upotevu wa maji, inakadiliwa kuwa Mamlaka za Maji Mjini zinapoteza zaidi ya bilioni 2.5 kwa mwezi kwasababu ya ukosefu wa vifaa vya kupima maji yanayozalishwa, yanatumika na yale yanayopotea.
Sheria ya Maji (2009) inazitaka mamlaka za maji kuwa na mita za kupimia maji yanayozalishwa na kusambazwa kwa wateja ili kuwa na takwimu sahihi juu ya maji yanayotumika na kuihakikishia serikali mapato ili kuendelea kutoa huduma hiyo kwa wananchi.
Sababu za upotevu wa maji
Kulingana na ripoti ya CAG inaeleza kuwa maji yanayozalishwa kwa sehemu kubwa yanapotea kabla ya kumfikia mtumiaji, jambo ambali linabaki mikononi mwa Mamlaka kushindwa kuwajibika katika uendeshaji wa shughuli zao.
Sababu mojawapo inayotajwa ni kutokuwepo kwa usimamizi mzuri wa mifumo ya usambazaji maji kutoka kwenye vyanzo hadi katika nyumba za watumiaji, ambapo katika baadhi ya maeneo hasa Dar es Salaam mabomba yanavuja kwasababu ya uchakavu na kutoboreshwa kwa muda mrefu.
Pia bajeti ndogo inayoelekezwa katika sekta ya maji hasa kwenye maboresho ya miundombinu na kukabaliana na uchakavu wa matanki ya kutunzia maji. Hili linakwenda sambamba na kutokuwepo kwa timu rasmi ya kuhakiki ubora wa vifaa vinavyonunuliwa na kutumika katika shughuli za maji, ambapo baadhi ya vifaa huaribika mapema pasipo wataalamu hao kujua.
Wizi wa miundombinu unaofanywa na watu wenye nia ovu. Pia Taarifa za kuharibika kwa miundombinu ya maji zinapotolewa bado hazifanyiwi kazi kwa wakati hasa pale ambapo muda wa kufanya kazi unakuwa umemalizika.
“ Kuvuja kwa maji kunakotokea baada ya saa za kazi, wakati wa mwisho wa juma na siku za sikuu haziwekwi kwenye kumbukumbu. Inachukua zaidi ya masaa 24 kurekebisha bomba lililopasuka”, inaeleza ripoti ya CAG.
Udhaifu huo unatajwa kuwakosesha wananchi huduma muhimu ya maji na kudidimiza juhudi za kukuza uchumi. Mathalani mwaka 2008/2009 Mamlaka ya Maji Dar es Salaam (DAWASCO) ilipoteza asilimia 54 ya maji yake yaliyozalishwa huku Mamlaka zingine za mikoani zilipoteza asilimia 36.2 ya maji yake. Kwa mamlaka zote nchini zilipoteza maji kwa asilimia 44% ambayo inakaribia nusu ya maji yaliyozalishwa.
Nini Kifanyike
Wizara ya Maji na Umwagiliaji inashauriwa kutekeleza matakwa ya Sheria ya Maji ya mwaka 2009 kwa kusimamia kikamilifu utendaji wa Mamlaka za maji hasa ufuatiliaji wa maji yanayopotea. Kuwa na mfumo mzuri wa mawasiliano kati ya wateja na mamlaka ili taarifa za kupashuka na kuvuja kwa mabomba ya maji zifanyiwe kazi ndani ya masaa 24.
Mamlaka zinashauriwa kuunda kikosi kazi ambacho kitakuwa mahususi kusimamia miundombinu ya maji katika maeneo yote na kuhakikisha iko salama na maji yanawafikia wateja kwa wakati.
Mkakati wa serikali
Katibu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo wakati akizungumza hivi karibuni katika kipindi cha runinga alisema serikali inaendelea kutekeleza matakwa ya Sera ya maji ili kuhakikisha maji ya uhakika yanapatikana kwa watu wote waishio mjini.
Akielezea tatizo la maeneo mengi ya Dar es Salaam, mabomba kuvuja maji, amesema mindombinu hiyo iliwekwa zamani na wanafanya juhudi za kuboresha na kuweka upya, “Miundombinu ya maji jiji la Dar es Salaam imechakaa kwa kuwa imewekwa zamani, sasa hivi tunafanya kazi ya kuunganisha upya”.
Amesema wanachukua tahadhari za muda mfupi na mrefu ili kutoa huduma bora kwa wananchi. Katika baadhi ya maeneo ambako miundombinu ya maji imeharibika, wanatumia magari kuwapelekea maji wananchi wakati ukarabati wa mabomba ukifanyika.
“Tumeagiza DAWASCO kupeleka maji kwa magari yake maeneo ambayo maji hayafiki na tayari kuna mradi mkubwa wa kuchimba visima”, amesema Prof. Mkumbo.
Katika nchi zilizoendelea kama Ujerumani, kiwango cha upotevu wa maji kilichowekwa ni asilimia 5 tu ya maji yanayozalishwa, lakini katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania kiwango cha juu cha upotevu wa maji hakitakiwi kuzidi asilimia 20.