Chakula kipo cha kutosha Rukwa – Stella Manyanya

Jamii Africa

MKUU mpya wa Mkoa wa Rukwa, Bi. Stella Manyanya, ametoa rai kwa mikoa yote yenye njaa nchini kwenda mkoani kwake kununua chakula kwani kipo tele. Bi. Manyanya amesema kwamba mkoa huo una hazina kubwa ya chakula mwaka huu kinachozidi tani 400,000, hivyo akawataka wafanyabiashara wakanunue chakula huko ili kupeleka kwenye mikoa iliyokumbwa na baa la njaa.

 

“Rukwa kuna chakula kingi na sioni sababu ya serikali kuhangaika kutafuta chakula kwingine wakati kinaweza kununuliwa hiki na kusambaza kwenye mikoa yenye uhaba wa chakula. Waje wanunue huku ili Watanzania wasife na njaa,” alisema Mkuu huyo wa Mkoa ambaye ameteuliwa kushika wadhifa huo. Bi. Manyanya pia ni Mbunge wa CCM – Viti Maalum.

 

Taarifa zinasema kwamba, takriban Watanzania milioni tatu wanakabiliwa na baa la njaa huku mikoa ya Arusha hasa wilaya ya Ngorongoro, na Kaskazini Pemba katika wilaya ya Micheweni zikiwa katika hali mbaya zaidi.  Hata hivyo,Bi. Manyanya amewaonya wafanyabiashara kutowapunja wakulima na kununua kwa bei nzuri mazao hayo ili wakulima hao waweze kunufaika na jasho lao.  Amesema pamoja na serikali yake kuwakaribisha wafanyabiashara wanunue mazao, lakini hatavumilia kuona wakulima wanapunjwa kwani lengo la serikali ni kuona kilimo kinamkomboa mkulima.

 

“Lazima wafanyabiashara wanunue kwa bei ya serikali na tutasimamia kuona wakulima hawapunjwi, lakini pia tutafanya jitihada za kuwaelimisha wananchi wasiuze chakula chote ikiwa bei itakuwa nzuri, kwa sababu kufanya hivyo kunaweza kusababisha uhaba mwingine wa chakula kwa tamaa ya fedha,” alisema.

 

Wilayani Ngorongoro, tarafa zilizokumbwa na uhaba mkubwa wa chakula ni Sale, Loliondo na Ngorongoro ambapo zinahitajika takriban tani 2,500 za chakula.  Kwa upande wa Wilaya ya Micheweni, zaidi ya watu 7,000 wanakabiliwa na uhaba wa chakula na ukosefu wa mazao katika vijiji kadhaa, hali iliyodumu kwa zaidi ya miezi mitano sasa.  Manyanya amebainisha kwamba, mkoa wa Rukwa unaweza kutoa chakula cha kutosha kwa ajili ya kukabiliana na uhaba wa chakula katika maeneo kadhaa ya nchi yenye uhaba huo na kuipunguzia mzigo serikali kuagiza chakula nje ya nchi.

 

“Hivi ni lazima tuagize chakula kutoka nje? Njooni Rukwa muone kulivyo na chakula cha kutosha. Waje wafanyabiashara wanunue chakula na kupeleka kwenye maeneo yenye uhaba, wananchi wangu hawawezi kukimaliza chakula chote hiki, ni kingi mno,” alisisitiza.  Hata hivyo, tangu serikali ilipozuia uuzwaji wa chakula nje ya nchi, wakulima wa mkoa wa Rukwa wameonekana kukata tamaa kwamba mazao yao yataharibika kwani wafanyabiashara wengi waliokuwa wakinunua chakula hicho ni kutoka nje ya nchi, hasa Zambia, Malawi na Zimbabwe.

 

Mariam Swita, mkulima wa kijiji cha Kalambanzite wilayani Sumbawanga, anasema walikata tamaa baada ya serikali kuzuia uuzaji huo wa chakula nje ya nchi ambapo walikuwa wakiuza kwa bei nzuri, lakini tangu serikali izuie na kupanga bei, wafanyabiashara wengi kutoka nje wameondoka.  “Hao (wafanyabiashara wa nje) ndio walikuwa mkombozi wetu, kwa sababu serikali hainunui mazao yetu na ikinunua kwenye Ghala la Taifa (SGR) ni kwa bei ndogo. Tunataka faida, lakini kwa hali hiyo tunawezaje kujikwamua?” alihoji Mariam.

 

Aliongeza kusema kuwa, wafanyabishara wa kutoka mikoa mingine wanashindwa kwenda Rukwa kununua mazao kwa sababu ya umbali na ukosefu wa barabara za uhakika, hivyo kujikuta wanatumia gharama kubwa kuliko faida watakayokwenda kupata huko.

Naye Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Sabas Katepa, anasema suala la kununua mazao ya wakulima limepewa kipaumbele baada ya kuzuia kuuza mazao nje ya nchi ambapo tayari wametenga vituo kadhaa wilayani humo kuhakikisha mazao yananunuliwa kwa haraka na wananchi wananufaika na jasho lao. Anasema, vituo vilivyotengwa viko karibu na wananchi na kuvitaja vituo vya Laela na Matahi ambavyo kwa kiasi kikubwa vimekuwa msaada kwa wakulima na kuondolea usumbufu wa kusafirisha kupeleka kwenye ghala kubwa ya taifa ya mkoa.

 

Naye msemaji wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Issa Sabuni, alikaririwa hivi karibuni akisema kwamba halmashauri zenye uhaba wa chakula zinapaswa kutoa taarifa mapema kwa wizara ili chakula kiweze kupelekwa kwani kipo kingi katika ghala la taifa la chakula.  “Halmashauri zenye upungufu wa chakula nchini zitoe taarifa kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu ili ziweze kupatiwa chakula hicho haraka. Kipo kingi cha kutosha, tatizo baadhi ya halmashaurizinauchelewa kutoa taarifa hizo za uhaba wa chakula hadi hali inakuwa mbaya,” alisema Sabuni.

 

Mwezi Julai 2011, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika wa Tanzania, Prof. Jumanne Maghembe, atangaza kuzuia uuzwaji wa chakula nje ya nchi hasa kwa njia za magendo, lakini akakiri kwamba nchi nyingi za Pembe ya Afrika zinakabiliwa na uhaba wa chakula kutokana na ukame.  Kwa hali hiyo, alisema badala ya kuuza chakula kwa magendo, nchi jirani ambazo zinakabiliwa na baa la njaa zinatakiwa kujadiliana na serikali ya Tanzania moja kwa moja na wala si wakulima, wafanyabiashara au mawakala kwa ajili ya kununua chakula.

 

“Tanzania ina ziada ya tani milioni 1.7 za chakula na serikali imekuwa ikifikiria kuuza ziada hizo kwa nchi jirani za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinazokabiliwa na uhaba wa chakula,” alisema.  Hivi karibuni, Tanzania iliuza kiasi cha tani 10,000 kwa nchi jirani ya Kenya ili kukabiliana na njaa nchini humo.

Na. Daniel Mbega

1 Comment
  • Ndiyo..! maana nami nimejionea huko, lakini nani wa kwenda Sumbawanga kununua mahindi wakati barabara zenyewe mbovu,Ndiyo haya tunayolaumu kuwa serikali haikuwa makini kuandaa barabara mikoa ya kusini ambako ndiko chakula kingi kinazalishwa,sasa nani akanunue mahindi sumbawanga aache kuishia Mbeya na Iringa. Je wananchi wa Katavi,Rukwa na Kigoma watauza wapi mahindi yao?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *