Maaskofu wahimiza watawala kulinda misingi ya demokrasia nchini

Jamii Africa

Viongozi waandamizi wa serikali wametakiwa kudumisha na kulinda amani  ya nchi kwa kuruhusu uhuru wa kutoa maoni na kuhimiza uvumilivu wa kisiasa miongoni mwa jamii.

Wito huo umetolewa kwa nyakati tofauti na watumishi wa Mungu wakati wa kusherekea siku kuu ya kuzaliwa kwa Yesu (Christmas) ambayo inasheherekewa Disemba 25 kila mwaka na wakristo wote duniani.

Askofu Mkuu wa kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe akihubiri katika ibada ya Krismasi jijini Dar es Salaam, amesema viongozi wa serikali wanapaswa kutafakari misingi ya amani iliyowekwa na waasisi wa taifa kwa kuheshimu utawala wa sheria na kujiepusha na matendo yote yanayoweza kuitumbukiza nchi katika machafuko.

“Leo ni siku ya watawala wa Tanzania kutubu, tumeanza kuona misingi ya amani ya nchi yetu ikitikiswa, amani iliyojengwa kwa gharama kubwa na waasisi wetu; tumeanza kuona nchi hii ni ya chama kimoja, na huu ni uovu”, amesema Askofu Kakobe.

Amesema misingi ya demokrasia ni pamoja na kuruhusu wananchi kutoa maoni yanayolenga kuboresha mstakabali wa maisha yao. Pia viongozi wanapaswa kukubali lawama na mawazo tofauti na kuiga mfano wa  Yesu  Kristo ambaye alistahimili matukano na maudhi kutoka kwa  watu ambao walikuwa hawaikubali huduma yake akiwa duniani.

“Mungu  ana nguvu kuliko majeshi yote ya nchi, lakini anatukanwa na bado hatumii majeshi yake, hata wewe unaweza ukawa mvumilivu”, amesema.

Ameongeza kuwa nchi ya Tanzania iko kwenye mfumo wa vyama vingi ambao unaruhusu vyama vyote kufanya shughuli zao bila kuingiliwa na mamlaka husika na kuwataka watawala kuheshimu sheria zilizopo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutokuruhusu migogoro ya kisiasa inayoweza kuvuruga amani ya nchi.

“Mungu mwenyewe anaheshimu sheria basi kama na sisi tumeweka sheria tunapaswa kuheshimu sheria tulizo jiwekea wenyewe”, amesema Askofu Kakobe na kuwaasa watawala kutoirudisha nchi kwenye mfumo wa chama kimoja unaopingana na misingi ya kujieleza kwa uwazi.

 Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kardinali Polycarp Pengo akihubiri wakati wa mkesha wa Krismasi katika Parokia ya Mtakatifu Maurus iliyopo Kurasini amesema ili kudumisha misingi ya amani, wananchi wafanye kazi kwa bidii na kujiletea maendeleo.

“Wakati umefika watu kufanya kazi usiku na mchana, hilo likifanyika nchi itaendelea kuwa na amani. Muda wote uwe wa kufanya kazi, tupumzike kidogo kwa ajili ya kupata usingizi”, amesema Askofu Pengo.

Amebainisha kuwa amani ya nchi haijengwi na viongozi waliopo madarakani bali na wananchi wenyewe kwa kufanya kazi na kuachana na uvivu na malalamiko. Pia amewataka wananchi kuwaombea viongozi ili waongoze kwa hofu ya Mungu na kulifikisha taifa kwenye kilele cha maendeleo yaliyokusudiwa.

Naye Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Zanzibar Mhashamu Augustino Shao amesema ipo haja kwa serikali na vyama vya siasa kuelewa dhana ya demokrasia kutokana na mchango wake katika maendeleo ya taifa.

“kwa kiasi kikubwa vyama hivi vimeleta mwanga na uwazi serikalini. Chaguzi ndogo za madiwani huko bara ni ishara tosha kwamba hatujafahamu maana ya demokrasia yaani kutofautiana lakini bado kubaki wamoja”, amesema Askofu Shao.

Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Zanzibar Mhashamu Augustino Shao

 

Sherehe ya Krismasi

Krismas ni sherehe ambayo huwaunganisha wakristo wote duniani kuazimisha siku ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo mwokozi wa ulimwengu ambayo hufanyika Disemba 25 kila mwaka. Siku hii imekuwa ikiwakutanisha wakristo mbalimbali katika nyumba za ibada na kutafakari maisha yao ya kiroho. Lakini viongozi wa dini wanaitumia kutoa matamko mbalimbali yanayolenga kuishauri na kuionya jamii juu ya mwenendo usiofaa.

Misa ya kitaifa imefanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Minara Miwili lilipo Zanzibar ambapo wakristo na viongozi mbalimbali wa serikali walijumuika pamoja katika kumbukumbu hiyo muhimu duniani.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *