Tanzania yazidi kuwa ngumu kutawalika; Wamachinga, wanafunzi wachachamaa

Jamii Africa

Kuzimwa kwa maandamano ya CHADEMA jijini Arusha mwanzoni mwa wiki na kuzuiwa kwa maandamano ya aina yoyote ya vyama vya siasa nchini kulitarajiwa kuwa kungezima harakati za kudai haki mbalimbali nchini. Kinyume na matarajio ya serikali na watawala mwamko wa kudai haki mbalimbali na kupinga ufisadi zimezidi kupamba moto baada ya vijana sehemu mbalimbali nchini kuingia mitaani kwa mara nyingine tena huko Dar-es-Salaam na Mbeya.

Mapema leo wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam waliamua kuhamia na kukaa kwenye maeneo ya chuo hicho wakidai mambo mbalimbali yenye kuhusiana na maisha yao kama wanafunzi na hususan suala la mikopo ya elimu ya juu. Makundi ya vijana yalikutana katika eneo lijulikanalo kama Uwanja wa Mapinduzi ambapo waliamua kukaa hapo lakini hawakuachiwa nafasi hiyo.

Jeshi la Polisi kwa kutumia kikosi cha kutuliza ghasia walilishukia eneo hilo kuwatawanya vijana hao kwa kutumia mabomu ya machozi na virungu. Hatimaye polisi walifanikiwa kuwatawanya vijana hao ambao nao wameendelea kukaidi na kuhaidi kuwa wataendelea kurudia hili hadi matatizo yao yatakaposhughulikiwa.

Hata hivyo tukio kubwa zaidi ni lile lilitokea Mbeya leo likifanana kwa kiasi kikubwa na tukio jingine lililotokea wiki chache huko Mwanza ambapo wafanyabiashara ndogondogo wa mitaani maarufu kama Wamachinga walipoamua kutolea uvivu uongozi wa mkoa. Katika hali ya kufanana kwa masuala yale yale ya “kusafisha jiji” wafanya biashara wa Mbeya nao waliamua kuingia mitaani na kuanzisha vurugu ambazo zilifunga kabisa magari kuingia kati ya jiji.

Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika ndani ya Jiji la Mbeya, wananchi walikuwa wamechoka kusubiri ahadi ambayo haikutekelezwa ya Mkuu wa Mkoa mpya bw. Kandoro ambaye alikuwa ameanzisha zoezi la kusafisha jiji. Bw. Kandoro alikuwa ameahidi kuwa wananchi wangeweza kurudi kwenye shughuli zao siku ya Alhamisi lakini Alhamisi ilipofika hakukuwa na dalili zozote za watu kurudi kwenye shughuli zao na matokeo yake ni wananchi kuingia mitaani kushinikiza serikali.

Vurugu hizo katika jiji la Mbeya zilianza mapema asubuhi na kudumu kwa zaidi ya masaa kumi na kusababisha usafiri kati Mbeya na miji mingine iliyo katika barabara ya kwenda Dar na ile ya Tunduma kushindwa kufanyika kama ilivyo kawaida. Vyanzo vyetu kutoka Uyole vimedokeza kuwa kuwa jeshi la polisi liliweka vizuizi njiani ambavyo vilizuia mabasi makubwa na magari kuingia yakitokea Uyole na kulazimisha watu kutelemka na kuanza kutembea kwa miguu kuelekea mjini huku wengine wakidandia bodaboda na vibajaji na kutumia njia za panya wakitokezea maeneo ya Forest na Block T.

Kutokana na jeshi la polisi kuzidiwa na wamachinga maafisa wa Magereza nao waliitwa kuongeza nguvu lakini hilo nalo halikufua dafu na baadaye taarifa zimedokeza kuwa JWTZ nalo lilialikwa kutoa nguvu zaidi. Hata hivyo hali iliendelea kuwa tetea na hatimaye kusababisha Mkuu wa Mkoa huo Bw. Abbas Kandoro kukatisha ziara yake huko Mbozi na kurejea jijini Mbeya ili kujaribu kukutana na wananchi hao hapo kesho kitu ambacho yawezekana kisifanikiwe baada ya Wamachinga kukataa kuonana naye hapo awali.

Mgogoro wa sasa wa Wamachinga na ule wa wanafunzi hauhusiani moja kwa moja na siasa bali zaidi na suala la raslimali na mgawanyo wa nafasi za kufanikiwa. Kama ambayo baadhi yetu tumekuwa tukiangaliza huko nyuma mgogoro huu utaendelea kuwa mkubwa hasa utakapoanza kuhusisha wakulima na hususan kwenye suala la ardhi. Tayari kuna maeneo nchini ambayo yameanza kugubikwa na migogoro ya ardhi ambapo wananchi wamejikuta wananyang’anywa maeneo yao ya jadi na kulazimika kutafuta maisha sehemu nyingine kabisa. Hili limetokea kwenye maeneo mbalimbali kama huko Morogoro, Rufiji, Bonde la Usangu na maeneo ya Kanda ya Ziwa Victoria.

Maoni ya watu wengi ni kuwa matumizi ya nguvu, risasi au vifungo yataweza tu kutuliza vurugu lakini kamwe hayatotatua tatizo la msingi ambalo Watanzania wanakabiliana nao leo hii yaani asilimia 1 ya Watanzania kuwa na madaraka na nafasi kubwa zaidi ya kufanikiwa kimaisha kuliko asilimia 99. Ni migogoro hii ya nafasi, na raslimali ndio ambayo imeibuka sana mwaka huu huko Nchi za Afrika ya Kaskazini, Marekani, Ulaya, Marekani ya Kusini na Mashariki ya kati.

Kwa kila dalili bado serikali ya Tanzania na vyombo vyake vinaamini kuwa matatizo haya ya msingi ambayo yanahusiana na utu wa wananchi wake yanaweza kumalizwa kwa vitisho, risasi au maji ya kuwasha. Hawajui tu kwa kadiri serikali inavyozidi kutumia nguvu ndivyo hivyo hivyo inazidi kuwafanya watu wazidi kuona kuwa hawana zaidi ya cha kupoteza isipokuwa utu wao. Wanasahamu maneno ya kina ya Mwalimu Nyerere kuwa kama watu hawatoweza kuishi kama binadamu watakuwa tayari kufanya kila wawezalo ili hatimae wafe na kuheshimiwa kama binadamu.

Ni wazi kuwa matumizi ya nguvu na kuogopa njia za mazungumzo yenye kushughulikia kwa kina tatizo la msingi ni mwanzo tu wa kuendeleza mgogoro wa kudumu kati ya watawala na watawaliwa na matokeo yake ni kuzidi kuongeza chuki ya wananchi dhidi ya serikali yao na hivyo kuzidi kukiweka Chama tawala matatani.

Na. M. M. Mwanakijiji

Picha zote kutoka Mbeya Yetu Blog

PICHA ZAIDI KUTOKA MBEYAYETU.BLOGSPOT.COM

 

Raia wema wakivukishwa barabara eneo la mapambano maeneo ya kabwe
Moja ya gari lililopasuliwa kioo na baruti
Wamachinga wakishangilia baada ya kuwazidi polisi nguvu
Nivurugu tupu maeneo ya soweto jijini mbeya
Wamachinga wakichochea moto wa matairi katikati ya barabara ya mbeya na tunduma 

PICHA ZAIDI KUTOKA MBEYAYETU.BLOGSPOT.COM

 

1 Comment
  • Kiwete ajifunze kwa gadafi kuwa nguvu ya umma inauwezo wowote kuliko askari wote”Serikali hii legelege na ya kifisadi inatakiwa isome alama za nyakati,kwa kutatua matatizo ya wananchi yaliyopo nayanayo tabiriwa kuwapo’isijidanganye kutumia mabomu,risasi na virungu,kwani mtu aliye na njaa anaweza kula hata udongo au simba kula majani ili aishi hivyo masikini tupo tayari kufa kwa kutetea haki’kikwete nchi immemshinda kwa kweli hili limeshaonekana toka miaka minne iliyopita.Kikwete hana maono.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *