Tafsiri, utata wa rais Magufuli kuzuia maandamano

Jamii Africa
CHATO, GEITA: Rais Magufuli ametoa onyo kali kwa Mtanzania yeyote atakayejaribu kuandamana. Amesema kitakachowakuta watahadithia - Rais amesema kuwa wapo Watu wameshindwa kufanya siasa za kweli wamebakia kuandamana - Asisitiza kama wapo Baba zao wanaowatuma kuandamana wataenda kuwasimulia

Rais John Mgufuli amepiga marufuku maandamano yanayoratibiwa na baadhi ya watu na amewataka wananchi kufanya kazi ili kuiletea nchi maendeleo.

Marufuku hiyo inakuja wakati kukiwa na mipango ya kufanyika kwa maandamano nchi nzima siku ya Muungano April 26 mwaka huu ambapo yanadaiwa kuikumbusha serikali kuheshimu utawala wa sheria na kupinga matukio ya kutekwa, kuteswa na kuuawa kwa raia wasio hatia yanayoendelea maeneo mbalimbali nchini.

Maandamano hayo yanadaiwa kupangwa na kuratibiwa na mwanadada na Mwanaharakati wa mtandaoni, Mange Kimambi ambaye anaishi nchini Marekani na kuungwa mkono na baadhi ya wanasiasa na wananchi ambao wanafikiri baadhi ya mambo hayaendi sawa na ipo haja ya kuchukua hatua kulinda amani na utulivu wa taifa.

Akizungumza leo wakati wa ufunguzi wa tawi la Benki ya CRDB mjini Chato mkoa wa Geita, rais Magufuli amesema hawezi kuruhusu watu wachache waharibu amani kwa kuandamana barabarani na kwamba kitendo hicho ni tafsiri kuwa wameshindwa kufanya siasa za kweli.

“Wapo watu ambao wameshindwa kufanya siasa za kweli wangependa kila siku tuko mabarabarani tunaandamana. Watu wao wanahamia huku wao wanataka wabaki wanaandamana kule,

 “Nimeshasema ngoja waandamane wataniona. Kama kuna baba zao wanawatuma, watakwenda kuwasimulia vizuri. Niliapa kwa Katiba kwamba nchi hii lazima iwe ya amani”, amesema rais Magufuli.

Amebainisha kuwa kinachofanyika sasa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo watanzania waliipigia kura mwaka 2015 na hatakubali mtu yoyote azuie utekelezaji wake na kuwataka watanzania kuvumilia wakati mabadiliko mbalimbali yakifanyika kuelekea Tanzania bora.

“Tunataka tujenge uchumi wa kweli watanzania watajirike, hali ya watanzania imeanza kwenda vizuri. Tuvumiliane mwanzo ni mgumu lakini nataka niwaambie tuko kwenye right track (njia sahihi) tufike kwenye nchi ya asali”, amebainisha rais Magufuli.

Hata hivyo, rais Magufuli hajawataja watu ambao wanapanga maandamano lakini amewaonya kwa ukali kwamba hataacha kuwachukulia hatua za kisheria.

“Tunatekeleza ilani ya chama cha mapinduzi. Wenzetu hawa watuache tutekeleze watakuja watuulize baada ya miaka mitano”, amesema rais Magufuli.

                                       Rais John Magufuli akitoa hutuba leo katika uzinduzi wa tawi la Benki ya CRDB, Chato mkoa wa Geita

 

Jeshi la Polisi launga mkono kauli yake

Katika kile kinachotajwa kuwa ni kutumia nguvu kubwa kuzima mipango yoyote ya maandamano siku ya Muungano, Jeshi la Polisi limeunga mkono kauli ya rais na kuwaonya wale wale wote wanaotaka kuandamana kuwa litawachukulia hatua kali za kisheria na halitabeba lawama zozote.

Akitoa tathmini ya matukio ya watu kuuawa mbele ya wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo, CP Nsato Marijani amesema wanafanya jitihada kuzuia kikundi cha watu wanaoratibu maandamano kwa njia ya mtandao ili kisitimize hazma yao.

“Jeshi la polisi tutafanya kila lililo ndani ya uwezo wetu na sheria inaturuhusu kuzuia kikundi hiki kinachopanga maandamano kupitia Telegram tusije tukalaumiana baadaye”, amesema CP Marijani

 Ameongeza kuwa  matukio ya mauaji yamepungua hadi kufikia matukio 235 kwa kipindi cha Januari 2018, kutoka matukio 288 Januari 2017 pungufu ya matukio 53 sawa na 18.%

 

Uhalali wa kuandamana

Kuandamana ni haki ambayo inatambulika na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo  katika Ibara ya 20 (1) inasema, kila mtu anao uhuru wa kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine.

Kwa muktadha huo, kukutana  na kuchanganyika ni sehemu ya maandamano ambayo watu wanaelezea fikra na maoni yao juu ya jambo lolote lile kwa masharti ya kulinda amani na sheria za nchi.

Haki ya kuandamana inaenda sambamba na uhuru wa kujieleza na kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 1977 ibara ya 18 (a), kila mtu ana uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake.

Kadhalika, sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2002 ibara ya 11 inatambua maandamano na mikusanyiko kama sehemu ya demokrasia na watu kufurahia uhuru wao bila kuingilia na mamlaka yoyote.

Sambamba na hilo Mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia inatoa jukwaa (Civic Space) la watu kukusanyika kutoa maoni au kuelezea yale wanayoyaamini bila kutishwa au kuzuiwa kwa namna yoyote ile.

 

Utafiti juu ya uhuru wa kujieleza
Ripoti mpya iliyotolewa na taasisi huru ya Freedom House (2018) imeeleza kuwa misingi ya demokrasia ikiwemo uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kukusanyika imeendelea kudhoofika nchini Tanzania na hali hiyo isiporekebishwa itaingia kwenye kundi la nchi zisizo na uhuru kabisa duniani.

Tanzania imewekwa kwenye nchi 88 ambazo zina uhuru kiasi lakini inatahadharishwa kuwa inaweza kuingia kwenye nchi zisizo na uhuru kabisa. Tahadhari hiyo inatokana na mwenendo wa viongozi wa serikali kufungia vyombo vya habari, kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, kushtakiwa kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii kwa tuhuma za uchochezi na kukamatwa kwa wapinzani wa kisiasa ambao wanakosoa na kutoa mawazo yanayotofautiana na serikali.

Pia utekelezaji wa Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015, Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016 na Sheria ya Makosa ya Mtandao  ya mwaka 2015 umekuwa ukilalamikiwa na wadau wa maendeleo kuwa ni mkakati wa kudhoofisha uhuru wa kutoa maoni, uwazi na uwajibikaji.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *