Mjadala wa kumalizia mchakato wa katiba mpya umeibuka katika siku za hivi karibuni. Asasi na makundi mbalimbali ya kijamii yameanza kujaribu kupaza sauti zao wakishauri na kuomba tuweze kukamilisha mchakato wa katiba mpya na tuwape Watanzania katiba mpya ambayo, kwanza waliahidiwa na utawala uliopita wa Chama cha Mapinduzi, pia katiba ambayo itakidhi mazingira mapya na changamoto za sasa.
Dhumuni la andiko hili ni kujaribu kujadili uhusiano wa katiba yetu tuliyo nayo sasa na Uchaguzi ‘Huru na wa Haki’. Swali kubwa la msingi ambalo naomba Watanzania wote tulitafakari kwa makini bila ushabiki wa itikadi za vyama.
Je, tutaweza kuwa na uchaguzi huru na wa haki kwa katiba yetu kama ilivyo sasa? Mimi sina jibu la wazi la swali hilo. Naomba nijaribu kuangalia na kujadili maeneo kadhaa ambayo yanaweza kutupa picha kama tunaweza kuwa na uchaguzi wa bora kwa kutumia katiba iliyopo.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, inataja sifa za kuchaguliwa kugombea Urais, Ubunge na Udiwani. Moja ya sifa hizo ni kuwa ili uweze kugombea nafasi hizo ni lazima uwe mwanachama, na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa.
Huwezi kuomba kupigiwa kura na wananchi wenzako iwapo wewe si mwanachama wa chama cha siasa na uliyependekezwa na chama cha siasa. Katiba yetu ndio inasema hivyo.
Haki ya kugombea kwenye uchaguzi wamepewa wale tu ambao ni wanachama wa vyama vya siasa na wameteuliwa kuwa wagombea wa vyama vya siasa pekee. Je, katika nchi yetu ya Tanzania, wanachama wa vyama vya siasa ni wangapi? Naweza kubashiri kuwa hawazidi milioni kumi. Hivyo hawa ndio wana haki ya kugombea nafasi mbalimbali za siasa.
Watanzania wote waliobaki wamenyimwa haki ya kugombea kama wagombea binafsi. Inakadiriwa kuwa Watazania sasa wanakaribia takribani milioni 54, ukitoa hao wanachama wa vyama mbalimbali na ambao hawajatimiza miaka 18, wote waliobaki hawana haki ya kugombea.
Nakuachia msomaji upige hesabu ni Watanzania wangapi wamenyimwa haki yao ya Uraia. Watanzania hawa, wanalazimishwa kuwa wanachama wa vyama vya siasa. Pia tukumbukuke kuwa katiba yetu hiyo hiyo inasema ni hiari ya mwananchi kujiunga au kutojiunga na chama chochote cha siasa.
Ningetamani haki ya kugombea kwenye uchaguzi isiwe kwa wagombea walioteuliwa na vyama pekee. Wagombea binafsi wawe na haki ya kugombea kwenye uchaguzi wowote wa Muungano au wa Zanzibar, kama ilivyoaninshwa kwenye makubaliano ya kimataifa kuhusu Haki za Kiraia na Kisiasa pamoja na Hati ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu. Hili eneo mojawapo ambalo yatupasa kulitazama kama tunataka kuwa na uchaguzi bora na wa haki. Rasimu ya Warioba pia ililiona hili na ilipendekeza wagombea binafsi waruhusiwe.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inasema: ‘Hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza jambo lolote lililotendwa na Tume ya Uchaguzi katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya katiba hii.’ Aidha katiba pia inasema kuwa:
‘Iwapo mgombea ametangazwa na Tume ya Uchaguzi kwamba amechaguliwa kuwa Rais kwa mujibu wa ibara hii, basi hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kwake.’
Vipengele hivi vya katiba navyo hatuna budi kuvitazama kwa makini. Kwa maneno mengine, katiba zote mbili, ya Muungano na ya Zanzibar, kwa sasa hazitoi haki ya kupinga matokea ya uchaguzi wa Rais.
Ni vyema katiba zetu zote mbili zikatoa haki ya kulalamikia matokeo ya uchaguzi wa Rais. Haki hii inapaswa kuwepo kisheria kulingana na kanuni za kimataifa za uendeshwaji uchaguzi wa kidemokrasia. Suala hili katika Tume ya Jaji Warioba katika rasimu yao pia walikuja na hitimisho la kuruhusu matokeo ya Urais yaweze kupingwa.
Kama mtakavyokumbuka kuwa Rasimu ya Warioba ilipendekeza tuwe na Tume Huru ya Uchaguzi. Na ilipendekeza namna ya kuipata tume huru ya uchaguzi. Hivyo, ni wazi kuwa Katiba yetu ya sasa haiwezi kutupa Tume Huru ya uchaguzi ambayo si tu itaaminika bali itaonekana inatenda haki.
Katiba yetu ya sasa inampa mamlaka Rais wa nchi kuteua Mwenyekiti wa Tume, Makamu Mwenyekiti wa Tume na Makamishna wote wa Tume. Hali hii imekuwa ikilalamikiwa na vyama vingine kuwa utaratibu huu hautupi Tume Huru. Tume ya uchaguzi imekuwa ikilalamikiwa sana kuwa haitendi haki kwa vyama vyote. Ni wakati muafaka sasa kulitazama hili hili ili tuweze kuwa na uwanja sawia wa ushindani.
Mapendekezo yaliyomo katika rasimu ya Warioba yanaweza kujaribu kutibu tatizo hili. Pia ni vyema Tume hii ikawa na watendaji wake katika ngazi zote hadi ngazi ya chini kabisa badala ya kuwa na mfumo katika ngazi ya kitaifa tu. Tume isiendelee kuwatumia Wakurugenzi katika majimbo ambao ni wateule wa Rais na wanawajibika kwake. Ili tuwe na uchauzi bora, tunahitaji Tume Huru ya Uchaguzi.
Jitihada za dhati zinapaswa kufanywa ili kuhakikisha kuwa taasisi za utendaji wa serikali kama vile Jeshi la Polisi, ofisi ya msajili wa vyama vya siasa na shirika la habari la Utangazaji zote zinatoa haki sawa kwa vyama vyote na kwa wagombea wote. Vyama vyote vipate nafasi sawa ya kuwafikia wapiga kura na kunadi sera zao. Wapate muda sawa katika vyombo vya habari. Muhimu zaidi kuwe na mijadala ya kina kuhusu changamoto zetu na utatuzi wake na pia wananchi wapewe fursa ya kuuliza maswali, kuomba ufafanuzi na kutoa maoni yao.
Katika uchaguzi uliopita tuliona Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) uliweza kumsimamisha mgombea mmoja. Lakini bado hatujawa na utaratibu mzuri wa kisheria unaoruhusu vyama vya siasa kuunda na kusajili umoja wa kiuchaguzi na kuwa na wagombea wa pamoja.
Kama tunakumbuka mgombea mwenza alilazimika kutoka katika chama chake na kujiunga na chama kingine ili kukidhi matakwa ya kisheria. Ili tuwe na uchaguzi usiokuwa na mawaa, ni vyema sheria ikaruhusu na ikaweka bayana, hususani kwa uchaguzi wa Urais ambapo wagombea wawili wanateuliwa kwa tiketi moja kwa nafasi za Rais na Makamu wa Rais.
Hata hivyo, tufanya rejea ya baadhi ya sheria na matumizi ya baadhi ya vipengele vya makosa ya kimtandao ambavyo wadau wengi wamekuwa wakipiga kelele kuwa vinapunguza uhuru wa kuongea na kutoa maoni yao. Tukiyarekebisha haya na mengine uchaguzi wetu utakuwa wa kidemokrasia zaidi.
Mwandishi: Selemani Rehani