MATUKIO ya ujambazi wa kutumia silaha nzito za kivita, yameanza kurejea kwa kasi kubwa mkoani Mwanza, ambapo safari hii watu 12 wanaosadikiwa kuwa majambazi yamevamia na kuteka Kisiwa cha Kome Wilayani Sengerema mkoni hapa, kisha kupora mamilioni ya fedha na kutokomea nayo.
Uvamizi huo ambao unaelezwa kufanywa kwa siku mbili mfululizo kati ya Jumamosi na Jumapili kisiwani humo, umesababisha wavuvi wengi wakiwemo wafanyabiashara kadhaa kuporwa mali zao na majambazi hayo yaliyokuwa na silaha za kivita.
Taarifa kutoka kisiwani humo, zinaeleza kwamba, majambazi hayo yaliendesha uvamizi huo kwa kutumia mapanga na bunduki yaliyokuwa nazo, hivyo kufanikiwa kupora idadi inayokadiriwa zaidi ya sh. milioni 20.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, ambazo zimethibitishwa na jeshi la polisi wilayani Sengerema, zinaongeza kwamba, siku ya Jumamosi majambazi hayo yalivamia katika eneo la Nyakasasa na Isenyi Kata ya Nyakasasa, na siku iliyofuata yaliteka kisiwani Kome.
Akizungumza leo na mwandishi wa habari hizi kutoka eneo la tukio, Diwani wa Kata ya Lugata kisiwani humo, Adrian Tizeba (CCM), alisema kati ya majambazi yao 12, majambazi mawili yalikamatwa na kuuawa na wananchi wenye hasira kali, na kwamba baadhi ya watu wamejeruhiwa vibaya na majambazi hayo.
“Haya majambazi yamevamia kwa siku mbili huku kisiwani kisha kupora wafanyabiashara fedha nyingi sana. Majambazi mawili yameuawa na wananchi.
“Kwa kweli hili ni tukio baya sana. Watu wamekatwa mapanga na haya majambazi, na inavyoelezwa yamepora zaidi ya sh. milioni 10, lakini taarifa nyingine zinasema yamechukuwa milioni 20 hivi”, alisema Diwani Tizeba kwa njia ya simu yake ya kiganjani.
Tukio hilo ni mfululizo wa matukio mengine ya ujambazi, ambapo hivi karibuni majambazi matano yalivamia katikati ya jiji la Mwanza majira ya saa 2 asubuhi, ambapo yalijibizana kwa risasi za moto na askari polisi kabla ya kuuawa.
Mbali na matukio hayo, tukio jingine la jaribio la kutaka kupora lilifanyika maeneo ya Liberty katikati ya jiji majira ya jioni, ambapo polisi walisema majambazi hayo yalikuwa yakijiandaa kwenda kufanya uhalifu maeneo ya Nyegezi.
Imeelezwa kwamba, majamabzi yaliyoshiriki katika uvamizi wa Kisiwani cha Kome kati ya Jumamosi na Jumapili wiki hii, baadhi yao ni wenyeji wa nchi jirani za Burundi, Rwanda na mkoani Kigoma.
“Kuna majambazi 10 yametoroka na bunduki pamoja na fedha yaliyopora. Kuna askari polisi huku wamemwagwa na OCD yupo huku. Uvamizi huu umefanyika kwa sababu hakuna hata vituo vya polisi”, alisema Diwani huyo wa Lugata, Tizeba.
Hata hivyo, Ofisa mmoja wa jeshi la polisi wilayani Sengerema ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa vile si msemaji wa jeshi hilo, alithibitisha kwa kusema: “Ni kweli majambazi yamevamia na kupora fedha nyingi huko Kome siku mbili mfululizo. OCD kaenda huko na timu ya askari polisi”.
Vituo vya Polisi kwa kweli vinahitajika haraka kupelekwa huko. ni mji unaochipukia tena uko mbali na makao makuu ya Wilaya hivyo huduma za kijamii pamoja na usalama wa jamii na mali zao wahitajika pia!